Msanii maarufu wa Bongo Fleva, Rajab Abdul maarufu ‘Harmonize’ na uongozi wake wa Konde Music Worldwide umeingia mitini baada ya kutakiwa kufika Baraza la Sanaa (Basata) kwenye kikao cha kujadili kuhusiana na sakata la kuwatimua wasanii wao Killy na Cheed kwenye lebo yao.
Tukio hilo limetokea leo Jumatano, Oktoba 12, 2022 katika ofisi za Basata Kivukoni jijini hapa ambapo kikao hicho ilikuwa kifanyike.
Hilo linatokea ikiwa imepita siku moja tangu uongozi wa lebo hiyo utangaze kuachana na wasanii hao kwa sababu ambazo hawakuziweka wazi.
Kutokana na hilo, wasanii waliotimuliwa walifikisha malalamiko yao Basata na kulitakiwa kikae kikao cha pande zote mbili kulizungumzia hilo taarifa ambayo inaelezwa walitaarifiwa kwa njia ya barua pepe (email) lakini mpaka inafika saa nane mchana sio Harmonize wala meneja wake waliotokea katika kikao hicho ambacho kilipaswa kuanza saa sita mchana.
Hata hivyo chanzo kimoja kiliiambia Mwanaspoti sababu zilizotolewa na kina Harmonize kushindwa kufika kikaoni ni kwamba hawana nafasi kwa kuwa wanasafari leo kwenda nchini Afrika Kusini kwa ajili ya ku ‘shoot’ na kuahidi kwamba wangeweza kufika kikaoni kuanzia Novemba 18, jambo ambalo Basata hawajakubaliana nalo na kutoa amri ya kufika kikaoni wiki ijayo bila kukosa kwa kile walichodai ni kulidharau baraza hilo.
“Haiwezekani email waipokee tangu Oktoba 6 na kukiri kupata taarifa halafu inafika siku ya kikao wanasema hawawezi kuja na kutaja sababu nyepesi ” kilisema chanzo hicho.
Kwa mujibu wa Mwananchi, Meneja wa wasanii hao aliyejitambulisha kwa jina la Sats Sembe, alisema sababu ya wao kufikisha malalamiko yao Basata ni kupinga utaratibu wa kuvunja mkataba na wasanii hao ambapo alieleza kuwa hakuna barua yoyote ya maandishi waliopewa mpaka sasa.
Sembe alisema kwa kuwa waliingia lebo ya Konde kwa maandishi basi hata kuondoka wanapaswa kuondoka kwa maandishi, ili kesho isije kutokea sintofahamu katika masuala ya kisheria.
“Huko mbeleni hatujui hili suala litafika hapa, lakini kwa kuanzia tumeanzia kwa walezi wetu na wazazi wetu Basata ambao katika hali ya kawaida tusingeweza kuwaruka.
“Lakini kama ikishindikana hatua hii tutaeda hata mahakamani ambapo kote huku barua ya maandishi ni muhimu kama ushahidi kwamba wameachana na wasanii wetu,” amesema Sembe