Machi 20, 1925, mchungaji wa Kanisa la Anglikana, UK, Frederick Donaldson, aliandika falsafa kuhusu maovu saba yaliyopitiliza kijamii. Kwa ajili ya matumizi mapana ya utoaji elimu ya kijamii, ilibadilishwa na kuitwa dhambi saba za kijamii.
Imekuwa ikitokea kwa watu wengi kuamini kuwa ‘Seven Social Sins’ ni falsafa iliyoletwa na mwanaharakati mashuhuri duniani, aliyekuwa raia wa India, Mahatma Gandhi. Historia inaonesha kuwa Gandhi aliandika orodha hiyo kwenye jarida lake la Young India, Oktoba 22, 1925. Miezi saba baada ya Mchungaji Donaldson.
Dhambi hizo zimeorodheshwa kama ifuatavyo; Utajiri bila kazi, furaha bila dhamira, biashara bila maadili, elimu bila uhusika, sayansi bila ubinadamu, dini bila sadaka na siasa bila misingi. Hayo yalikuwa maono ya takriban miaka 97 iliyopita. Karne moja kasoro miaka mitatu.
Kuomba uongozi wa kisiasa kwa sababu tu unataka kutamkwa ni kiongozi au kutafuta umaarufu. Unaamua kugombea nafasi kwa sababu unaona ni mtindo (fashion) katika maisha. Hiyo ni dhambi ndani ya kipengele cha “siasa bila misingi”.
Uongozi unahitaji wito wa kutumikia watu. Kiongozi wa kisiasa ni lazima abebe misingi ya utumishi wa umma. Maono yake ya kutaka uongozi lazima yajengwe na sababu mahsusi za kuchagiza matokeo chanya kama ataipata nafasi anayoomba. Na anapoipata, athibitishe kwa vitendo kwamba kweli alikuwa na wito.
Mahubiri ya Mwalimu Nyerere
Machi 1968 na Oktoba 1969, Rais wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, alikabili na kushinda jaribio la pili kumwondoa madarakani. Awali, mwaka 1964, Mwalimu “Baba wa Taifa”, alinusurika jaribio la kwanza.
Kwa mujibu wa nyaraka za kimahakama, kuanzia Mahakama Kuu ya Tanzania hadi Mahakama ya Rufaa ya Afrika Mashariki, jaribio la pili lilikuwa mpango wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Tanu, Oscar Kambona, kurejea na kutwaa madaraka. Kambona alikimbia nchi mwaka 1967 na kwenda kuishi Uingereza.
Baada ya kushinda jaribio la pili la mapinduzi, Mwalimu Nyerere aliwafananisha baadhi ya wanasiasa na wanajeshi wa kukodi ambao huangalia pesa tu ili watumike kwenye jeshi lolote. Huwa hawatazami misingi. Msingi wao ni fedha.
Mwalimu alisema, wanasiasa wana tabia za ‘kimalaya’, kwamba wao hununulika kwa fedha kisha hutumiwa. Ujumbe ambao Mwalimu alitaka ufike ni kwamba kuna wanasiasa ndani ya Serikali aliyoiongoza walinunuliwa na Kambona.
Alichokizungumza Mwalimu Nyerere ndio kilekile alichonena Mchungaji Donaldson na kurejewa na Gandhi; siasa bila misingi!
Mwanasiasa aliyekosa msingi wa kufanya kazi ya siasa hununuliwa au kutumika kwa kuumiza jamii. Mtoa pesa ndiye humwongoza.
Dhambi ya “siasa bila misingi”, sio tu mwanasiasa kununuliwa, bali pia hata kununua cheo au kujali masilahi binafsi kuliko sababu na malengo ya kisiasa.
Masomo yote ya siasa, kihistoria na nadharia zote za sayansi ya siasa, yanaelekeza wito na huduma.
Kuanzia mafundisho ya Plato mpaka Aristotle, unachoweza kuvuna kutoka kwa wanafalsafa hao ni kuwa siasa lazima ziwe na misingi. Maadili, uaminifu, utu na utumishi ni sehemu misingi ya kisiasa.
Tofauti na tafsiri ya Mwalimu Nyerere kuwa wanasiasa aliowaita malaya wapo kama wanajeshi wa kukodi, miaka 23 baada ya kifo chake, inakuwa rahisi kupanua wigo wa tafsiri. Fedha ni sababu kubwa ya migogoro ya kisiasa ndani ya vyama.
Mathalan, hivi sasa Chadema wana kesi mahakamani dhidi ya wanachama wao 19 waliowafukuza uanachama. Mgogoro ni kwa nini walikwenda bungeni na kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalumu wakati chama kilipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu 2020?
Masuala ya kesi yatashughulikiwa mahakamani. Hapa tuguse kilichozungumzwa na kupewa sauti kubwa nje ya mahakama; ubunge na fedha. Hoja hii ni ya pande zote mbili. Wanaotuhumiwa na wao wanatuhumu. Ndani ya mahakama mengi yatawekwa dhahiri.
Hali kama hiyo ni mgogoro uliopo NCCR-Mageuzi. Tayari James Mbatia ameshafukuzwa uanachama. Shauri limeshafika mpaka mahakamani. Kinachojadiliwa kwa sauti kubwa nje ya mahakama ni pesa na madaraka!
Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad na Profesa Ibrahim Lipumba, walikigawa Chama cha Wananchi (CUF) vipande kwa sababu ya mgogoro uliopambwa na maneno mawili; fedha na madaraka. Ni mara chache itasikika migogoro ya kisiasa bila fedha.
Mwenyekiti wa ADC, Hamad Rashid, aliondoka Cuf baada ya mnyukano na Seif. Mgogoro wa Hamad na Seif angalau ulikuwa na msingi, lakini tafsiri za washindani ikaleta fedha kwenye mjadala.
Hamad alijenga hoja kuwa Seif kwa kuwa alishakuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, angeachia ukatibu mkuu wa CUF, kwa sababu kuwa na vyeo viwili kuliumiza chama, maana muda mwingi alikuwa na shughuli nyingi za Serikali. Waliompinga Hamad walidai alinunuliwa.
Hata mgogoro wa Chadema mwaka 2014 na 2015, uliosababisha kufukuzwa uanachama kwa Zitto Kabwe, Profesa Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba, hoja ya waliofukuzwa ilikuwa Mwenyekiti Freeman Mbowe siyo kiongozi sahihi, lakini ikasemwa walinunuliwa.
Ndivyo ilivyokuwa miaka ya 1990 kwenye mgogoro mkubwa wa NCCR-Mageuzi, uliomwondoa kwenye chama marehemu Augustino Mrema na kuzika urithi (legacy) ya Mabere Marando. Vilevile aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Chacha Wangwe, harakati zake za kutaka uenyekiti zilipingwa kuwa alihongwa.
Lisemwalo lipo
Kama nilivyotangulia kueleza kuwa ya mahakamani yatapatiwa ufumbuzi na uamuzi ndani ya chombo hicho cha kutafsiri sheria. Hapa nahitaji kupita na na msemo kuwa “lisemwalo lipo”. Tuhuma za fedha na kununua kwenye vyama vya siasa, zinakaribisha hisia kuwa haya mambo yapo.
Ikiwa tutafika mahali na kukubaliana kwa sauti moja kuwa kelele nyingi kwamba siasa zinafanywa biashara zinashawishi kuamini yanayosemwa, tutakuwa kwenye wakati mzuri wa kujenga sauti ya pamoja kuwa dhambi ya siasa bila misingi inatesa mno vyama.
Wanasiasa wanapaswa kutofautiana mawazo ya jinsi ya kuongoza nchi au vyama. Sio wapinzani kupokea fedha (au kutuhumiana kuhongwa pesa) ili kujenga migogoro ya ndani kwa ndani. Hapa ieleweke kuwa hata kutuhumu bila uhakika imo kwenye dhambi ya siasa bila misingi.
Maisha ya kisiasa yalivyo sasa, wengi wanaona siasa ni jukwaa la kusaka utajiri wa haraka. Ubunge ni kazi inayolipa fedha nyingi. Uwaziri ni zaidi. Diwani hana mshahara lakini anakopeshwa fedha akanunue gari la kutembelea, kisha anahesabu vikao vya mavuno ya posho.
Kuna wafanyabiashara wanatumia fedha kuingia bungeni si kwa ajili ya utumishi na uwakilishi, bali kujenga ukaribu na mamlaka za nchi, lengo likiwa kurahisisha biashara zake. Inafahamika hii. Wakati huohuo, wabunge na mawaziri wanaomba fedha kwa wafanyabiashara.
Mbunge anapokuwa ombaomba anapungukiwa meno ya kung’ata au anakuwa kibogoyo kabisa. Ama atang’ata anapoona hakuna masilahi yake na kujifanya haoni makosa ya wanaompa fedha, au ananyamaza jumla. Huyo ndiye kibogoyo.
Miaka 23 bila Mwalimu Nyerere siasa zimekuwa jukwaa lenye fedha nyingi.
Wananchi wanashughulishwa mno kipindi cha kampeni, baada ya uchaguzi, walioshinda wanakwenda kupanda ngazi ndefu ya kimaisha na kuwaacha wapigakura waliokuwa na matumaini wakiwa wanakata tamaa.
Kati ya mwaka 2017 hadi mwaka 2022 zilikuwa siasa za kuwahi nafasi CCM kabla ya uchaguzi. Maana ilisemwa wapinzani wasingepata kitu 2020. Basi, wapinzani wenye kutaka kitu, ilibidi wahame wafuate kitu CCM.
Kwa vile siasa ndiyo sanaa kiranja kwenye nchi, ni mtihani mkubwa. Siasa inawezesha kupata Rais, wabunge, mawaziri, wakuu wa mikoa, madiwani na wakuu wa wilaya. Siasa inaleta utawala, utendaji na uwakilishi. Siasa inatuletea watunga sheria zenye kutafsiriwa na mahakama.
Sasa, nchi ikiwa na wanasiasa wenye kufikia daraja la ubunge au udiwani. Nao wanahama bila hoja zenye mashiko.
Nchi yenye vyama vya siasa ambavyo viongozi wake wa ngazi za juu, wanaweza kuhama kirahisi pasipo kuwa na hoja zenye ujazo, hapo lazima tukumbuke dhambi ambayo ilishaandikwa tangu muongo wa tatu wa Karne ya 20. Ni dhambi ya siasa bila misingi.
Ni dhambi iliyohubiriwa na Mchungaji Donaldson, ikawekewa mkazo na Baba wa Taifa la India, Mahatma Gandhi, kisha Mwalimu Nyerere akasema wanasiasa wasio na misingi ni malaya. Maana hufanya chochote kwa nguvu ya hongo ya fedha.