Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) amemfutia mashtaka mfanyabiashara Hamisi Luongo (41) aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya mauaji, baada ya kueleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hilo.
Luongo maarufu kama Meshack anakabiliwa na shtaka moja la kumuua mke wake, Naomi Marijani.
Uamuzi wa kumfutia kesi hiyo, umetolewa leo Jumatatu, Oktoba 24, 2022 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Yusto Ruboroga baada ya upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa Serikali Mwandamizi Mwasiti Ally, kuieleza Mahakama hiyo hawana nia ya kuendelea na shauri Hilo dhidi ya mshtakiwa.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya kumfutia shtaka hilo, mshtakiwa huyo alikamatwa na kufunguliwa kesi mpya yenye shtaka linalofanana na hilo na kisha kusomewa kwa hakimu mwingine ambaye ni Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rhoda Ngamilanga.
Akimsomea shtaka lake, Wakili Ally amedai mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo, Mei 15, 2019 katika eneo la Gezaulole, wilaya ya Kigamboni, Dar es Salaam ambapo alimuua mkewe Naomi Marijani.
Siku hiyo ya tukio, mshtakiwa anadaiwa kumuua mke wake wa ndoa Naomi Marijani, wakati akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria
Hata hivyo, mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote mahakamani hapo kwa kuwa shtaka la mauaji linalikukabili, Mahakama hiyo haina Mamlaka ya kusikikiza isipokuwa kwa kibali kutoka kwa DPP.
Hata hivyo, upande wa mashtaka baada ya kumsomea shtaka lake, walidai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kwamba wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Ngimilnga ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 7, 2022 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shtaka la mauaji linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Hii ni mara ya pili kwa Luongo kufikishwa mahakamani hapo kwani katikati ya Mwaka 2019, mshtakiwa alifikishwa mahakamani hapo kwa kosa la mauaji.
Oktoba 2020, upelelezi wa shauri hilo ulikamilika na mshtakiwa kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo na kisha Mahakama hiyo kumhamishia Mahakama Kuu, kwenda kusubiri tarehe ya kuanza usikilizwaji wa mashahidi wa upande wa mashtaka.
Hata hivyo, kwa kipindi chote hicho hadi leo Jumatatu, mshtakiwa huyo alikuwa anakaa gerezani kutokana na shtaka la mauaji kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.
Itakumbukwa kesi hiyo ni miongoni mwa kesi zilizovuta hisi kwa jamii na hiyo ni kutokana na kuongezeka kwa matikio ya mauaji.