MSHAMBULIAJI wa Yanga, Stephane Aziz KI anatamba kwa bao lake kali la pili kwenye ligi akiwafunga Simba wikiendi iliyopita kisha akadai hiyo sio kitu kipya kwake.
Akizungumza na Mwanaspoti kwenye mahojiano maalum, Aziz KI alisema amefurahishwa na hatua ya kuifungia timu yake bao muhimu la kusawazisha katika mchezo wa sare ya bao 1-1 dhidi ya Simba lakini mabao ya namna hiyo ndio zake.
Aziz KI anasema amekuwa na ubora mkubwa wa kufunga bao kama lile hata kabla ya kutua Yanga ambapo alipoona adhabu ile eneo lile aliamini atafunga kama mpira utakwenda anavyotaka kwani hata mlinda mlango Aishi Manula anamjua na ana historia nae. “Nafurahia kuifungia timu yangu bao muhimu kwenye mechi kubwa kama hii, lilikuwa ni bao ambalo timu nzima tulilisubiri,”alisema.
“Niliamini ningefunga pale hasa baada ya kuona wapi adhabu inatakiwa kupigwa nikawaomba wenzangu wanipe nafasi ili nipige ni mipira ambayo naifanyia sana mazoezi na huwa nafunga hata kabla sijaja Yanga.”
Raia wa Burkina Faso alisema licha ya sare hiyo bado Yanga ina nafasi ya kufanya vizuri ambapo wataendelea kuipigania timu yao kutafuta matokeo bora zaidi.
Alisema anawashukuru mashabiki wao waliofurika kwa wingi kuja kuwapa nguvu hasa wakitokea kupata matokeo mabaya ya Ligi ya Mabingwa Afrika
Yanga imeshacheza mechi 7 ikitoa sare 2 na kushinda 5 ambapo leo itashuka Uwanja wa Benjamin Mkapa kupambana na wabishi KMC kwenye mechi yao ya 8 ya Ligi Kuu Bara.
Endapo Yanga ikishinda itarejea kileleni ikisubiri matokeo ya kesho ya Simba na Azam. Hapa anaelezea mambo mbalimbali akiwa ndani ya Yanga na nje ya klabu hiyo.
MAISHA NDANI YA YANGA
KI anaanza kwa kuelezea jinsi maisha yake yalivyo na wenzake ndani ya timu hiyo tangu amefika akionyesha kufurahishwa na karibu kila kitu alichokutana nacho.
“Maisha ndani ya Yanga yako vizuri sana, maisha yamekuwa rahisi sana sijaona shida, nimepokelewa vizuri na wachezaji wenzangu, makocha, viongozi na hata mashabiki kama unavyoona, tumekuwa tunaishi kifamilia tunafurahi, kupanga mambo yetu na yanakwenda vizuri, hii inakufanya kama mchezaji kuona umefika sehemu salama,” anaeleza Aziz KI huku akiendelea kufafanua mambo zaidi.
“Nimekuwa rafiki wa kila mmoja, hii ni familia ya watu wacheshi kama unavyoona kina Morrison (Bernard) na wengine, nipo na watu ambao wanacheza kwa malengo na ushindani kwahiyo maisha yanaendelea kuwa na hesabu nyingi za kutafuta mafanikio.”
“Yanga ni timu nzuri, nilisema awali kwamba nilifurahia maisha wakati tu nafika hapa, najiona niko klabu sahihi kutokana na falsafa ya soka la hii klabu, wanataka kuuchezea mpira hiki ndicho napenda kufanya, nafurahia kucheza hapa, nafurahia maisha ya nje ya soka, mashabiki wa Yanga wana upendo sana kwasasa najikita zaidi kuhakikisha nazoea haraka mazingira ili kiwango changu kifanye mnakubwa kwa ajili ya hii klabu, nataika kushinda mataji yaliyo mbele yetu hii ni kiu yangu kubwa sasa.”
MASHABIKI WALIMTEKA KITAMBO
KI anaeleza kwamba wakati anakuja nchini mara ya kwanza akiwa na klabu yake ya ASEC Mimosas ikicheza dhidi ya Simba kumbe mashabiki wa Yanga walishaziteka hisia zake kitambo.
“Nakumbuka kuna wakati nilikuja hapa Tanzania tulipokuwa tunacheza na Simba kuna kitu kiliugusa moyo wangu juu ya Yanga, nakumbuka wakati nipo uwanjani niliona kikundi cha mashabiki kinatushangilia, walikuwa kama watu 30 hivi wamevaa jezi za njano, nilipofunga nikaona pia wameshangilia zaidi na mimi niliwafuata na kushangilia nao, nikajiuliza hawa mashabiki wetu wametoka wapi? Baadaye nikaambiwa wale ni mashabiki wa timu watani wa Simba wanaitwa Yanga, nilifarijika sana kuona watu wakitupa nguvu, kutoka hapo kukawa na kitu ndani ya moyo wangu kuhusu hii klabu.
DILI LAKE YANGA LILIKUWAJE
“Binafsi naweza kusema mtu aliyefanya kazi bora na naweza kusema alikuwa nyota wa mchezo kwa Yanga alikuwa ni rais Hersi (Said) alifanya kazi kwa utulivu iliyonishawishi kuwa hapa Yanga, nakumbuka mara ya kwanza alinipigia tu simu na kujitambulisha na kuniambia anataka kuja nilipo anisalimie, nikamkaribisgha kwa kuwa alishaonyesha anatokea klabu fulani
“Unajua ni ukweli kwamba hata kabla ya Hersi kunipigia nilikuwa na mazungumzo na klabu nyingi mbalimbali kila moja ikitaka huduma yangu, utofauti ulikuwa jinsi Hersi alivyokuwa anafanya mazungumzo ya karibu kwa kuamua kuwa karibu kwanza na mimi hasa kunifuata nilipo.
“Kikubwa kushinda hata pesa alionyesha kuniheshimu kwa kunifuata nilipo, tulizungumza kama mara mbili katika maeneo tofauti na naweza kusema nchi tofauti na zote akija kwa ajili yangu tu, hakuna timu nyingine iliweza kufanya ambacho alifanya au Yanga ilichofanya, akazungumza pia na mama yangu, hii ilikuwa heshima ambayo hata familia yangu iliiiheshimu nguvu yake.
Baada ya hapo tuliendelea na mazungumzo ya mara kwa mara na mwisho tulikuja kukubaliana, inawezekana kukawa na ushawishi wa fedha lakini kikubwa kilichoinufaisha Yanga kwa mimi kuja hapa ni heshima hii ambayo niliipata na mwisho nikasaini kuja hapa.
SOKA LA YANGA LAMVUTIA
“Baada ya mazungumzo na Hersi na kunieleza juu ya mradi wao kama klabu pia nilikuwa anaongea na kocha Nabi (Nasreddine), alionyesha ni kocha mzuri alinikaribisha na kunaimbia matarajio yake ya kuja kufanya nao kazi, hata soka la Yanga nilipolifuatilia lilinivutia jinsi wanavyocheza kwa kuwa mimi napenda kuchezea timu inayocheza soka la kuuchezea mpira na kutafuta ushindi kwa mipango bora.
YACOUBA KAHUSIKA HIVI
“Kuna pia Yacouba (Songne) naye ni kaka yangu alishatangulia hapa mara nyingi nilikuwa nikitaka kuongea na Hersi tunaongea naye kwa pamoja, kubwa nilikuwa pia nazungumza naye kwa kina tukiw wawili, alinithibitishia jinsi maisha yalivyo mazuri hapa Yanga, nilivutiwa na jinsi alivyosimamiwa matibabu yake mpaka sasa, hii inakupa uhakika kwamba sehemu unayokwenda ni mahala salama, nakumbuka nilipokuja hapa kucheza na Simba aliniletea jezi ya Yanga vyote hivi viliuandaa moyo wangu vyema sikukutana na wasiwasi na hata niliposikia kibaya kuhusu Yanga kuna mambo yalisafisha hayo yote.
SIMBA ILIKUWAJE
“Nilikuwa na ofa za kutakiwa na klabu nyingi lakini niliona sehemu sahihi ni kuna Yanga kutokana na jinsi walivyoheshimu kunifuata, naiheshimu Simba ni klabu nzuri lakini nafikiri Mungu alitaka nicheze hapa ndio maana hata mazungumzo yao na mimi hayakuwa yanakwenda kwa kunyooka sana, ilikuwa tunazungumza kisha tunakaa kimya kwa muda na baadaye walikuja tena mambo yalikuwa hivyo.
KUFUNGA MABAO
Kama unapenda kumuona KI anatumika nafasi nyingi ndani ya Yanga usipoteze muda jamaa anapenda kucheza nafasi moja pekee.
“Aziz KI alizaliwa kucheza namba 10 pekee, hii ndio nafasi yangu kubwa nataka kucheza nitakueleza sababu nyingi, kuna wachezaji watatu wamenifanya kucheza soka wa kwanza sijui kama watu wanamjua Riquelme (Juan Román kiungo wa zamani raia wa Argentina), kuna Messi (Lionel) na Modric (Luka), mimi napenda kufanya kazi za nafasi hiyo na hao ndio watu wanaoniongoza natamani niwe na ubora mkubwa kama wao.
“Napenda kutengeneza nafasi hasa kupiga pasi za mwisho za mabao, kwangu mimi kitu bora ni kutengeneza nafasi ili zitumike kuipatia timu mabao kuliko hata mimi kufunga, nafahamu hapa watu wanakiu ya kuniona mimi nafunga mabao lakini niwaombe wasiwe na kiu hiyo kubwa lakini nitafurahi kama nitawazalishia sana mabao washambuliaji kama nikipata nafasi ya kufunga nitaifungia timu yangu lakini kikubwa kwanza ni kuifanya timu ikapata nafasi nyingi za kufunga,”anasema huku akiongeza kuwa anahitaji muda zaidi ya kuzoeana na wenzie kiuchezaji kwani mambo yajayo ni mazuri.
UJUMBE KWA MAYELE
“Nilipokuwa ASEC nilikuwa nacheza kwa ushirikiano na mdogo wangu Karim (Konate), nilimpokea pale na ni mdogo kwangu alipofika nilikaa naye nikamwambia nataka uwe mfungaji mzuri jiandae kufunga kwa kutumia pasi zangu, tulicheza kwa ushirikiano sana sio tu uwanjani bali hata nje ya uwanja tulikuwa pamoja.
“Kwa sasa nipo Yanga, kuna rafiki yangu Mayele (Fiston) ni mchezaji bora sana napenda kucheza naye kama ilivyo Makambo (Heritier) nimemwambia Mayele kwamba najua alikuwa mfungaji bora wa klabu hii hapa msimu uliopita, lakini nataka kumfanya awe mfungaji bora wa ligi na ninavyomuona alivyoanza msimu huu atakuwa mfungaji bora, acha kwanza nizoee ligi ya hapa baada ya muda watu wataona hilo.
“Nimemwambia nitampa pasi za kufunga mabao mengi, nimekuwa nikizungmza naye na kumsoma jinsi ya kumpa mipira anayotaka na pasi gani anazitaka ili tuisaidie Yanga na mwisho yeye awe mfungaji bora.
ANAJIFUNZA KUTETEMA
“Unajua kuna kitu kikubwa Mayele amekipanda kwa sisi wachezaji na hata mashabiki ile shangilia yake kutetema, hata sisi wachezaji tunapenda kuona anafunga sana ili tushangilie pamoja na mashabiki wetu, mimi pia najifunza sana bado sijaweza sawasawa, unajua tangu nikiwa sijaja hapa nilikuwa naangalia mikanda ya mechi za Yacouba na naona ile shangilia ilikuwa inanivutia sana kuona mashabiki wote wanafanya kama yeye tena wakiona amefunga tu wanasimama tayari kwa kushangilia naye pamoja, hii ni nzuri sana inaonyesha watu wako pamoja na timu yao.
LIGI IVORY COAST vs TPL
“Tofauti kubwa ni kwamba kule kuna ufundi na mbinu sana hapa kuna ufundi kiasi na nguvu sana, hapa unatakiwa mchezaji uwe tayari sana kupambana sio rahisi kufanikiwa hata kama uhna ufundi mwingi mguuni ingawa ushindani ni mkubwa sana kila timu unayokutana nayo imekuja tayari kwa kuwazuia.
PRESHA KUBWA
“Hapana sipo kwenye presha kabisa, nafahamu kuna matarajio makubwa na hili ni suala la muda tu kama ambavyo nimeeleza lakini baada ya muda huu niliotaka watu watajua kwanini nipo hapa, kuna wakati mambo kama haya hutokea kwenye soka sio kila sehemu utakwenda na kuzoea mazingira haraka, mimi nikiwa uwanjani napenda kufurahia kazi yangu, nataka sana kuona mashabiki wanafurahia kazi yangu uwanjani.
YANGA ITACHUKUWA UBINGWA
“Tuna kikosi bora sana ingawa tunawaheshimu wapinzani wengine, kitu bora kwetu n i kuendelea kushinda, ukitazama kikosi chetu kinajieleza kwa aina ya ubora wake, watu wanaangalia kuhusu nje lakini ugumu wa kwanza Yanga ni kupata nafasi ya kucheza kutokana na kila mchezaji ana ubora, hii ndio inatupa ubora uwanjani kwa kuwa unalazimika kufanya kilicho bora ili upate nafasi ya kucheza.
“Tutachukua tena mataji hayo ni malengo yetu lakini kubwa sasa ni kutamani kuona Yanga inafanya vizuri katika mashindano ya Afrika,”anasema staa huyo ambaye hapendi kabisa mitoko wala kuzurura.
MSOSI WA BONGO UNAMSUMBUA
“Kitu ambacho sijakizoea hapa Tanzania ni chakula cha hapa, hii ni changamoto yangu kubwa nafikiri sasa nafanya mpango kuhakikisha mpenzi wangu anakuja hapa Tanzania haraka ili aweze kuniandalia chakula, nimeshindwa kabisa kula chakula cha hapa.
“Huwa nakula sana tambi na samaki labda kidogo sana huwa najaribu kula wali lakini vingine nimeshindwa, nikiwa katika mapumziko nje ya kambui huwa najaribu kupika mwenyewe chakula cha kwetu.”
MAHUSIANO KIMAPENZI
“Mimi kitu cha kwanza ni familia yangu, uliniuliza huwa nikiwa nyumbani napenda kufanya nini, jibu kubwa sana ni kuwa karibu na binti yangu Sanatha (4) nilimpa jina la mama yangu mzazi, napenda kuwa naye karibu na mama yake, bado sijamuoa lakini hilo litakuja, niliona nitangulie kwanza huku kuja kuangalia mazingira ya jinsi ya kuwaleta na wao na watakuja,.
MKATABA NA PUMA
“Mimi situmii kiatu kingine uwanjani zaidi ya Puma, hawa jamaa nina mkataba nao na hata Yanga wanajua, napenda viatu vyao.”