WACHEZAJI wa soka wengi hupenda kuwa na alama zao zinazowatambulisha kirahisi ama kuwatofautisha kimwonekano na wenzao, kama kunyoa mtindo fulani wa nywele, kuchora tatoo na hata namna ya uvaaji wa jezi uwanjani, hivyo ndivyo ilivyo pia kwa mshambuliaji wa Simba Queens na Timu ya Taifa ya Tanzania
Mchezaji wa Simba Queens Fatuma Issa 'Fetty Dansa'
Fetyy Densa, ambaye huwezi kuacha kutaja jina lake pindi unapozungumzia soka la wanawake nchini, yeye amejizolea umaarufu mkubwa si tu uwanjani, bali pia kutokana na uvaaji wake wa hijab akiwa anatandaza soka dimbani.
Fetty Densa ambaye ni nahodha wa Simba Queens iliyopo mkoani Iringa ikijiandaa na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake, anasema awali alikuwa hacheze na hijab na kwa kwamba mara ya kwanza alipoamua kuanza kuvaa ilikuwa shida, lakini kwa sasa haoni tatizo lolote.
"Kwangu haina shida yoyote kucheza nikiwa nimevaa ushungi ni kawaida na ninaamini kupitia mimi kuna watu wengine watajifunza kupitia hichi ninachokifanya kwa kuona ni kitu kizuri."
Ligi ya Mabingwa
Fetty Densa ambaye alikiongoza kikosi hicho kutwaa ubingwa wa Cecafa mapema mwezi wa nane kwa kuifunga She Corporate FC ya Uganda kwenye mechi ya fainali na Simba Queens kuweka rekodi ya kushiriki michuano ya Ligi Mabingwa Afrika ikiwa timu ya kwanza ya wanawake kutoka Tanzania kufanya hivyo, anasema wamejipanga vema kufanya makubwa katika michuano hiyo.
Katika michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Oktoba 30 hadi Novemba 13, mwaka huu, Simba Queens imepangwa Kundi A na Green Buffaloes ya Zambia, Determines ya Liberia pamoja na wenyeji, ASFAR ya Morocco.
Alipoanzia soka
Fetty Densa ambaye ni mzaliwa wa Morogoro, anasema alianza kucheza soka tangu akiwa mdogo wakati huo akisoma shule ya msingi na kisha kucheza mitaani kabla ya kuanza kucheza soka la kulipwa baada ya kuja Dar es Salaam.
"Nilikuja Dar es Salaam mwaka 2010, kisha nikajiunga na timu ya Eva Green ya Temeke ambayo niliichezea kwa kipindi cha miaka tisa kabla ya kujiunga na Simba mwaka 2019," anasema.
Sapoti kwa wazazi
"Kwa upande wa wazazi wangu walinisapoti kwa kiasi kikubwa hadi kufikia hapa nilipo, ila kipindi cha nyuma bibi yangu alikuwa na mashaka kuona mimi nacheza soka.
"Ilikuwa tabu sana kwa sababu yeye ndiye aliyekuwa akinilea, siunajua tena malezi ya bibi? Lakini baadaye alikuja kunielewa baada ya kuona kuna kitu nakitafuta na kukihitaji, hivyo akaona si mbaya kuniachia kupambana katika soka la wanawake.
"Kwa hiyo nimeendelea kupambana hadi leo na ndio maana wazazi wangu wameona kuna matunda yanaonekana na kuendelea kunitia moyo jambo ambalo linanifanya daima nipambane zaidi kwa sababu wao ndio wanaonipa nguvu sana."
Changamoto ndani ya Simba
"Nimekutana na changamoto nyingi baada ya kutua Simba kwa kuwa hii ni timu kubwa kila mmoja anataka kupambana ili kuweza kupata namba.
"Ninaamini kila mmoja anacheza kwa kujituma ili apate namba na kufikia malengo yake na ya timu kwa jumla, changamoto ni za kawaida ambazo kila mmoja anazipitia ila naamini kila mmoja anapambana ili kuipeleka mbali timu yetu."
Changamoto katika soka
"Changamoto zipo nyingi, wengi wanaamini mpira huu wa miguu ni kwa wanaume tu na si kwa watoto wa kike, lakini nakabiliana nazo hivyo hivyo kwa sababu ndio kipaji changu na mpira ndio kazi yangu ninayoipenda.
"Nafanya hivyo kwa kuwa nina malengo ya kufika mbali, hivyo naendelea kupambana ili nitimize ndoto yangu licha ya baadhi kuuona mpira wa miguu kwa wanawake ni kama ni uhuni."
Mafanikio katika soka
"Mafanikio niliyoyapata hadi sasa kwanza ni kujuana na watu mbalimbali, pili makombe niliyofanikiwa kuyapata nikiwa katika timu ya Taifa, Twiga Stars na Simba Queens.
"Pia napata pesa kupitia kipaji changu cha mpira vilevile nasaidia familia yangu kupitia kazi hii, kuna mafanikio yangu binafsi niliyoyapata ambayo sipendi kuyaweka hadharani, ni kitu kikubwa sana kwangu ambacho kila mtu anatamani kukipata katika maisha yake.
Ushindani Ligi ya Wanawake
Anasema kwa sasa umekuwa mkubwa na ligi hiyo imekuwa na mvuto tofauti na huko nyuma.
Ahadi kwa Wanasimba
Fetty Densa anasema kufanya vizuri katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ndicho kitu anachowaahidi.
Ushauri kwa wazazi
"Naomba wazazi na walezi kuwaruhusu watoto wao kwani mpira ni ajira pale wanapoona wanavipaji na si kuwafungia ndani.
"Mpira wa miguu ni mchezo kama michezo mingine, wasiwabeze watoto wao naupenda kwa kuona uhuni, waendelee kuwaunga mkono ili tuweze kulifikisha soka la wanawake mbali zaidi."