KOCHA Mkuu wa Manchester City raia wa Hispania Pep Guardiola mara baada ya mchezo wa Ligi ya Mbingwa dhidi ya FC Copenhagen ameibuka na kutoa ufafanuzi juu ya taarifa zinazoenea mitandaoni kuhusu mshambuliaji wa klabu hiyo Erling Braut Haaland kuwa na kipengele katika mkataba wake kinachomruhusu kujiunga na Real Madrid mwishoni mwa msimu wa 2023/2024.
Taarifa zilizo ripotiwa na Gwiji wa zamani wa Real Madrid na Rais wa zamani wa Klabu ya Malaga, Fernando Sanz zimebainisha kuwa katika mkataba alisaini Erling Haaland na Manchester City unamruhusu mshambuliaji huyo hatari kwa sasa Duniani kujiunga na Real Madrid mwishoni mwa msimu wa 2023/2024.
Mshambuliaji wa Manchester City Erling Braut Haaland
Aidha Kocha wa Man City Pep Guardiola wakati akijibu swalki la mwandishi wa Habari baada ya mchezo dhidi ya Copenhagen alisema:
“Siyo kweli, hana kipengele cha kumruhusu Kwenda Real Madrid au timu nyingine yoyote ile, Napata hisia kuwa na furaha sana hapa tutajitahidi pamoja nay eye na wengine kumfanya awe na furaha hapa.”
Akiongea na Kituo cha Luninga cha El Chiringuito nchini Hispania Fernando Sanz alinukuliwa akisema:
Gwiji wa zamani wa Real madrid Fernando Sanz
“Taarifa nilizonazo ni kwamba kuna kipengele kinachomruhusu kuondoka na kujiunga na Real Madrid mwishoni mwa msimu wa 2023/2024 na cha kushangaza zaidi ni kwamba kipengele hicho kina upendeleo mkubwa kwa klabu ya Real Madrid kuliko vilabu vingine vyote.”
Kwa upande mwingine gazeti maarufu la michezo nchini Hispania Gazeti la Marca limeripoti kuwa kwenye mkataba wa Haaland kujiunga na Man City kuna vipengele vingi vyenye thamani tofauti tofauti kulingana na mwaka.
Marca imebainisha kuwa katika moja ya vipengele ni kwa mchezaji huyo kuruhusiwa kuondoka Ethad kwa ada ya Euro Milioni 200 mnamo mwisho wa msimu wa 2023/2024 na Euro Milioni 150 mnamo mwaka 2025.