Magari yakionekana kupita katika Daraja jipya la kisasa la WAMI ambalo linaunganisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani pamoja na mikoa ya Kaskazini
DARAJA jipya la kisasa WAMI ambalo linaunganisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani pamoja na mikoa ya Kaskazini limeanza kutumika rasmi oktoba 27, mwaka huu ambapo linakwenda kuwa tija kwa takriban miaka 120 ijayo.
Aidha daraja hilo, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 96 kwa ujumla asilimia 99 kwa Maendeleo ya kazi za Daraja na asilimia 93 kwa Maendeleo ya kazi za barabara unganishi.
Akikagua daraja hilo lenye M 513.5 na barabara unganishi km.3.8 ,lililoanza kutumika na magari kuruhusiwa kutumia daraja hilo ,Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alieleza ,daraja hilo litafungua uchumi na maendeleo ya wilaya ya Bagamoyo , mkoa wa Pwani na nchi kijumla.
Hata hivyo,alieleza Daraja hili linategemewa kupunguza kwa asilimia kubwa ajali za mara kwa mara zilizokuwa zinatokea kwenye daraja la zamani ambalo lilikuwa jembamba na lenye barabara zenye miiinuko mikali.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akitembelea mradi wa daraja la Wami sambamba na viongozi mbalimbali wa serikali na chama.
Alieleza Ujenzi wa Daraja jipya una lengo la kutatua changamoto zitokanazo na daraja la zamani ambalo kwa sasa halikidhi mahitaji ya magari yanayopita kwa kuwa lilijengwa miaka 63 iliyopita (mwaka 1959) .
Mbarawa alifafanua, ujenzi ulianzishwa na Serikali ya awamu ya tano oktoba ,mwaka 2018 chini ya hayat John Magufuli na kuacha ujenzi kwa asilimia 44 ambapo Rais Samia Suluhu Hassan amekamilisha kwa asilimia 52.
“Sikuja kuzindua nimekuja kupitisha magari katika Daraja hili la WAMI ,wajibu wetu mkubwa kumshukuru Rais kwa utekelezaji wake na kujivunia Daraja kukamilika”
“Wapo waliosema miradi inasuasua ,haitaendelezwa ,Lakini leo sisi tunashuhudia utekelezaji wa mradi huu mkubwa,Mradi huu ulikuwa ikamilike Novemba mwaka huu lakini leo oktoba 27 oktoba tunashuhudia Daraja limekamilika kabla ya muda, Nani Kama Samia ,”;alifafanua Mbarawa.
Aliwataka wananchi walilinde na kulitunza daraja ili liweze kudumu kwa muda mrefu Kama lilivyosanifiwa kufikia miaka 120 ijayo.
TANROADS
Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Dorothy Mtenga alisema , maendeleo ya utekelezaji wa mradi umegharimu kiasi cha zaidi ya Bilioni 75″ , na Mkandarasi alianza kazi rasmi Oktoba 22, mwaka 2018 .
Akizungumzia faida za mradi huo alisema kiuchumi daraja hilo litaboresha usafirishaji wa bidhaa za viwandani kutoka mikoa ya Pwani na Dar es Salaam ikiwemo Bandari ya Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kaskazini ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na nchi jirani ya Kenya.
Dorothy alisema kwa upande wa ajira zilizozalishwa, jumla ya ajira 420 kati ya hizo ajira 395 zimetolewa kwa Watanzania na ajira 25 ni za wageni.
Faida nyingine ni kupunguza muda wa kuvuka eneo la daraja kutokana na uwezo wa kupitisha magari mawili kwa wakati mmoja.
“Mradi umesaidia watalaamu wazawa kuongeza ujuzi kutokana na teknolojia mpya ya ujenzi wa madaraja marefu inayoitwa Prestressed Concrete Box Girder -Free Cantilever Method, Teknolojia hiyo kwa hapa nchini bado ni ngeni, hivyo mafunzo hayo yatasaidia kujenga uwezo na ujuzi utakaolisaidia taifa letu baadae,” alibainisha Dorothy.
Alisema ujenzi wa daraja jipya la Wami unagharamiwa kwa fedha za Serikali Kuu Sh. 75, 134, 647,654.55 isiyokuwa na kodi la ongezeko la thamani (VAT). Usanifu uligharimu Sh. 852, 991,000.00, ujenzi unagharimu Sh. 67,779,453,717.55, usimamizi unagharimu Sh. 6,307,484,937.55 na fidia imegharimu Sh. 194,718,000.00.
Mradi ulifanyiwa upembezi yakinifu na usanifu wa kina na kampuni ya Intercontinental Consultants and Technocrats Pvt Ltd ya India kwa kushirikiana na Apex Engineering Co.Ltd ya Tanzania kwa gharama ya Sh. 852,991,000.00 isiyo na VAT mwaka 2016.
Dorothy alisema, pia Kwasasa mkandarasi ataendelea kukarabati Daraja la zamani ambapo baada ya ukarabati litatumika kutokana na maelekezo yatakayotolewa
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani