Kila mmoja kwa nafasi yake, kocha, wachezaji, viongozi na hata mashabiki wanatakiwa kutekeleza vema majukumu yao kwenye mchezo huo ili kuishangaza Afrika kitu ambacho kinawezekana. Kama ambavyo iliwezekana kwa Al Hilal kupata bao kwa Mkapa basi Yanga nayo inaweza kuliamsha Sudan.
Zikiwa zinahesabika saa kabla ya dakika nyingine 90 ngumu za Sudan kwenye Uwanja wa Al Hilal, haya ni mambo matano ambayo yanaweza kuibeba Yanga kwenye mchezo huo ambao wanahitaji ushindi wa aina yoyote au sare ya kuanzia mabao mawili ili kutinga hatua ya makundi.
BAO LA MAPEMA
Al Hilal itakuwa na presha ya kusaka japo suluhu kwenye uwanja wao wa nyumbani kwa kusukuma mashambulizi mfululizo, hivyo Yanga inaweza kutumia mwanya huo kama faida kwao ya kutafuta bao la mapema ambalo linaweza kuwafanya wenyeji wao kupaniki na kushindwa kucheza kwenye kiwango chao.
Bao la mapema linaweza kuvuruga utulivu wa wapinzani wao, hivyo kuanzia hapo, Yanga inaweza kuwageuzia kibao Al Hilal na kuwashambulia kwa mashambulizi mfululizo. Ukikitazama kikosi cha Nasreddine Nabi pamoja na kwamba wapo wachezaji ambao bado hawajaonyesha thamani zao, unaweza kubaini kuwa ni kundi lenye nyota wenye viwango vya juu.
Kila mmoja akiamua kupigania rangi ya kijani na njano za klabu hiyo kwa dakika zote 90 za mchezo ni wazi wanaweza kupata matokeo chanya.
KUTUMIA NAFASI
Hivi karibuni Yanga imekuwa na changamoto ya kutumia nafasi ambazo wamekuwa wakizitengeneza kwenye michezo yao iliyopita, rejea mechi dhidi ya Zalan kutoka Sudan Kusini, Nabi anatakiwa kuwajenga wachezaji wake kwa maana ya kuongea na mmoja baada ya mwingine ili kuongeza umakini.
Kadri unavyozidi kupiga hatua kwenye michuano mikubwa kama Ligi ya Mabingwa ndivyo unapokutana na timu ngumu hivyo unaweza kupata nafasi tatu hadi nne kwenye mchezo mmoja kama unakuwa huna wastani mzuri wa kutumia nafasi zinazotengenezwa ni hatari kwa afya ya timu kufanya vizuri.
Akiongelea hili, nyota wa zamani wa Yanga, Sunday Manara kabla ya mchezo dhidi ya Zalan, alisema,”Ni kweli kuwa Yanga huwa inashambulia sana lakini ikija kwenye kufunga huwa wanakosa mabao mengi, na hata wakipata huwa machache, huwa naumiza sana kichwa kwanini tupoteze sana nafasi vile, unajua kwenye mashindano ya kimataifa unaweza usipate nafasi za namna ile.”
UMAKINI KUJILINDA
Hakuna eneo ambalo limekuwa likimpasua kichwa Nabi kama safu yake ya kujilinda, kumekuwa na mabadiliko mengi hasa eneo la beki ya kati ambapo kuna muda amekuwa akianza Yannick Bangala na Dickson Job, Bangala na Mwamnyeto na muda mwingine Job na Mwamnyeto.
Yanga inatakiwa kucheza kitimu zaidi kwa maana kila mmoja anatakiwa kuwa msaidizi wa mwingine ili kuwa salama, hilo linaweza kuwapa wakati mgumu Al Hilal na kushindwa kuona mianya ya kuwashambulia. Umakini kwa kila mchezaji unahitaji ili kuwa salama zaidi, makosa yanaweza kuwagharimu.
MPANGO MBADALA
Nabi anapaswa kuwa na mbinu mbadala kwenye mchezo wa marudiano, ili kwenda kuwachanganya wapinzani wake, Al Hilal ambao watakuwa wanajiamini zaidi na bao la ugenini.
Uzuri ni kwamba Nabi analijua hilo na alihidi kwenda ugenini kwa ajili ya kwenda kusaka matokeo. “Najua siyo kazi nyepesi, kikubwa nitakwenda kwa mbinu ya kushambulia zaidi ili kuweza kupata matokeo kwenye mchezo wa marudiano.”
SAIKOLOJIA
Wachezaji wanatakiwa akili na mawazo yao yawe kwenye mchezo. Mambo ya nje ya uwanja yasiathiri kiwango chao, kama wanavyoshauriwa na mwanasaikolojia, Charles Nduki.
“Kama Yanga inataka ikawavuruge wapinzani wao, wanapaswa wachezaji akili zao kuwaza ushindi na siyo jambo lingine, waende wakijiamini bila kujali wanacheza ugenini na hilo litawafanya kazi kwao iwe rahisi, maana hofu siyo nzuri katika maisha ya mtu yeyote,” anasema.