JUZI jioni kulikuwa na timu mbili kubwa nchini zinacheza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. Mmoja aliingia akijivunia historia yake ya mechi za karibuni, mwingine alikuwa anajivunia fomu yake ya siku za karibuni. Wote wakakutana njiani wakatupa sare.
Kabla ya mechi, Yanga walikuwa wanawaza bao la Fei Toto pale Mwanza, halafu wakawaza mabao mawili ya Fiston Mayele pambano la ufunguzi wa Ligi. Kabla ya mechi Simba walikuwa wanawaza fomu yao siku za karibuni, hasa baada ya kushinda mechi nne za kimataifa dhidi ya Nyasa Big Bullets na Premiero de Agosto nyumbani na ugenini.
Yanga waliona wanakwenda kushinda mechi. Walijiamini pengine kuliko wakati wowote ambao walikuwa wanakwenda kucheza na Simba katika miaka ya karibuni. Hapa mitaa ya katikati ingawa walikuwa wanashinda au kutoka sare lakini hawakuwahi kujiamini kama juzi.
Simba waliingia wakiwa vizuri kisaikolojia kwa maana ya kuamini kwamba Yanga walikuwa wa kawaida baada ya kutolewa na Al Hilal. Lakini pia walikuwa wanajiamini baada ya wao kufanya vizuri zaidi katika mechi za kimataifa.
Walikutana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na Simba ndio ambao walianza kucheza pambano kwa kasi. Ni pambano ambalo kabla ya mechi, na wakati wa mechi tulilitazama kwa hisia kali lakini kwa wakati huu tulikuwa tumetulia tutagundua kwamba ni pambano ambalo halina mambo mengi ya kukumbukwa.
Simba walicheza vizuri kuliko ilivyotegemewa lakini ni pambano ambalo tutalikumbuka kwa pasi maridadi ya Clatous Chotta Chama kwenda kwa mfungaji wa bao la kwanza la pambano, Augustine Okrah. Halafu tutalikumbuka pambano kwa shuti kali la mpira wa adhabu kutoka kwa Aziz Ki. Basi.
Bao la Okrah lilikuja kama matunda ya kazi nzuri ambayo Simba waliifanya katika kuupitisha mpira haraka kutoka nyuma kwenda mbele. Walifanya hivyo mara nyingi kabla na baada ya bao la Okrah. Hapa ndio muda pekee ambao walipatia.
Chama, utazungumza nini kingine kuhusu yeye? Pasi yake iliwakumbusha Yanga kwamba ana macho katika kisogo chake. Yanga na uwanja mzima ulidhani angepiga pasi ya nyuma au upande wa pili lakini akaupitisha mpira uvunguni ukaenda kwa Okrah.
Makosa pia anayo Kibwana Shomari. Alipaswa kurudi katika mstari ambao wenzake walikuwa wanakabia na Okrah angeweza kuwa ameotea. Hata hivyo, wakati mwingine kujituma kwingi bila ya kuwa na maarifa mengi ni jambo ambalo lilimtokea Shomari. Alitaka kuwa wa mwisho kwa ajili ya kufuta makosa ya wenzake lakini kumbe ule haukuwa wakati mwafaka.
Halafu likaja bao la Aziz Ki. Lilikuwa bao maalumu kutoka kwa mchezaji maalumu. Aishi Manula aliupanga ukuta wake vema, akajiridhisha, kisha akarudi katikati ya lango. Lengo lake lilikuwa kuibia kama Aziz angeupiga mpira nyuma ya ukuta au katika upande ambao ulikuwa wazi.
Aziz aliamua kupiga katika upande ambao ulikuwa wazi zaidi. Aishi aliuona ule mpira lakini kasi yake ilikuwa kubwa. Sio David de Gea, Alisson Becker, Peter Schmeichel wala Manuel Neuer ambao wangeweza kuudaka mpira ule. Aziz alipiga kwa nguvu zaidi na kasi ya mpira ni tofauti na kasi ya mwili.
Mpira ulipokwenda mapumziko nilikuwa nawaza kwamba ilikuwa siku nyingine ya Simba kufungwa. Mechi iliyopita, Ousmane Sakho aliitanguliza Simba lakini Mayele akasawazisha na kufunga bao la kuongoza pia.
Zamani Yanga walikuwa wanakata pumzi katika kipindi cha pili lakini siku hizi tumeshuhudia Yanga wakicheza vizuri zaidi katika kipindi cha pili. swali lilikuwa kama Simba wangeweza kuubeba moto wa Yanga katika kipindi cha pili. Ukweli ni kwamba waliweza.
Yanga waliingia kwa kasi kidogo lakini baadaye Simba wakaukamata moto wao. Mara chache walibadilishana mashambulizi lakini Simba walionekana kuwa vizuri zaidi. Nataka kuwazungumzia mastaa wawili hapa ambao kwa nyakati mbili tofauti waliimbwa na mashabiki wao.
Sakho. Mchezaji wa kawaida tu ambaye alicheza vema mechi mbili tatu za Kombe la Mapinduzi kule Zanzibar halafu akaifungia Simba bao bora la msimu la CAF. Vinginevyo sasa imedhihirika ni kwanini Msenegal mwenye miaka 25 yupo Afrika Mash ariki.
Sakho anataka kufanya kila kitu mwenyewe. Anacheza kwa ajili yake na sio timu. Anajaribu kucheza na jukwaa badala ya kufanya mambo mengi ya msingi uwanjani. Hawa ndio ambao waliifanya Simba ya msimu uliopita ishindwe kuifukuza Yanga.
Kilichonishangaza ni kwamba baada ya kutolewa na kocha wake, Juma Mgunda akaanza kulalamika. Sijui alikuwa analalamika nini. Kama ningekuwa Mgunda nadhani ningempatia Sakho mkanda wa pambano la juzi aeleze kwanini hakupaswa kutolewa.
Halafu kule Yanga kuna Tuisila Kisinda. Yanga wameanza kujuta kwanini walishangilia wakati anarudi. Na hapo hapo nusura awagombanishe na TFF wakati walipogoma kumruhusu acheze Yanga kwa madai kwamba Yanga walikuwa wametimiza idadi ya wachezaji husika.
Kisila ana mbio ambazo haziisaidii timu na wala hazimsaidii mwenyewe. Kwa kasi yake, kama angekuwa na akili nadhani angekuwa mbali. Sidhani kama angekuja kucheza Tanzania na badala yake angekuwa katika nchi za Ufaransa au Ubelgiji ambazo zililitawala taifa lake la DR Congo.
Wakati Mayele alikuwa anategemea mbio zake ili apikiwe mabao, Tuisila alikuwa ajaribu kufunga katika eneo ambalo ni vigumu kwake kufunga. Tuisila hawezi kufanya vitu rahisi kwa ajili ya timu. Anafanya vitu kwa ajili yake na bado uamuzi wake unakuwa mbovu.
Kwa upande wa Simba tena, zamani nilikuwa namsifia Okrah lakini kumbe na yeye ameanza kuvimba kichwa. Ameinyima Simba mabao kutokana na tamaa ya kutaka kufunga mwenyewe tena na tena. Ushindi wa Simba ulipaswa kutokana na yeye lakini akaamua kuwa mchezaji mchoyo uwanjani. Asije akaanza kuwa Sakho mwingine.
Mwamuzi Ramadhan Kayoko? Alichezesha vizuri pambano hili. Kwa umri wake ni pambano lenye presha kubwa zaidi ukanda huu. Alichokosea ni kutoa kadi nyingi za njano bila ya kuanza utaratibu wa kuwaonya wachezaji.
Nilijua kwamba kipindi cha pili ambapo wachezaji wengi wangekuwa wamechoka wangeweza kuanza kucheza rafu za kijinga ambazo zingemuweka wakati mgumu Kayoko kutoa kadi za pili za njano. Mfano ni rafu ya Fei Toto kipindi cha pili kumkumbatia Moses Phiri. Alipaswa kutolewa nje kwa kadi ya pili ya njano lakini Kayoko hakufanya hivyo.