Homa Yapanda na Kushuka Mkeka Wakuu wa Wilaya



Rais Samia Suluhu Hassan ni kama amepandisha, lakini wakati huohuo akishusha presha kwa wakuu wa wilaya, baada ya kuwaeleza wachape kazi, kwani hana mpango wa kutoa mkeka mpya.

Mkuu huyo wa nchi amesema, tathmini ya utendaji kazi iliyofanyika kwa wateule wake hao ambao pia ni wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama ngazi ya wilaya, imemsaidia kwani imemwezesha kujua nani mzuri, nani mbaya, jambo ambalo kwa wakuu wa wilaya wengi limekuwa likiwaweka tumbo joto.

Rais Samia aliitoa kauli hiyo juzi jijini Dodoma, aliposhiriki hafla ya utiaji saini mkataba wa usimamiaji wa shughuli za lishe kati yake na wakuu wa mikoa nchini.

Alisema amekerwa na wakuu wa wilaya ambao wameacha kufanya kazi, kwa sababu wanasubiri mkeka wa uteuzi na kwamba amesikia kuwa baadhi ya wakuu wa wilaya hawafanyi kazi.

Alisema amekuwa akipata ujumbe mfupi wa maneno kuwa amalizie kazi (kazi ya uteuzi), kwa sababu wakuu wa wilaya wamekuwa hawafanyi kazi.

“Nikute mtu amepigwa ganzi. Nilishasema tulichokifanya ni performance (tathmini ya utendaji) ya utendaji wenu, sikusema kwamba nitawabadilisha leo wala kesho.

Nimesema tumefanya performance, tumejua nani mzuri, nani mbaya aliyesema anataka kuwabadilisha ni nani. Kama nataka kuwapa mafunzo je?” alihoji.

Alisema kazi ya kutoa mkeka ni ya kwake na hivyo ataifanya wakati atakapoona mwafaka, hivyo wanatakiwa waende kufanya kazi.


“Sasa wakuu wa mikoa ni nataka ripoti za wakuu wenu wa wilaya, aliyepigwa nusu kaputi, nani aliyepigwa ganzi ni nani. Ehh kama hawawezi tuwatoeni, tuweke wengine.Nataka ripoti ya wakuu wenu wa wilaya na hilo tutalizungumza jioni,” alisema.

Sababu ya ma-DC kuwa tumbo joto

Mkeka huo aliouzungumza Rais ambao unaonekana kama vile umewapiga ganzi wakuu hao wa wilaya, unatokana na hofu kufuatia mabadiliko ya wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa ambayo Rais Samia aliyafanya Julai 28 mwaka huu.


Katika mabadilikoa hayo, aliwaengua baadhi ya wakuu wa mikoa na makatibu tawala na kuteua wengine, huku baadhi wakihamishwa mikoa.

Hali hiyo ilizidisha homa kwa wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na makatibu tawala wa wilaya, kwamba huenda baada ya mabadiliko hayo na wao walikuwa njiani.

Kwa kawaida miongoni mwa majukumu ya wakuu wa wilaya ambao ni wawakilishi wa Rais ni, ni kuwa wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama, wasimamizi wakuu wa shughuli za maendeleo, sambamba na kuwa wafuatiliaji na wasimamizi wa utekelezaji wa sera mbalimbali za Serikali.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Paul Loisulie alisema wateule wajue nafasi za kuteuliwa ni kama wameazimwa katika eneo hilo, na kwamba yeyote anayeteuliwa katika nafasi yoyote ajipange kufanya kazi.

“Hata ikitokea ukaondolewa hiyo ndio nafasi ya uteuzi, mimi sioni sababu wakae wanashangaa shangaa. Kwa sababu wakifanya hivyo huenda ndio wanajiharibia badala ya kuonekana wanachapa kazi, wataonekana kuwa wanaogopa ama wameshtuka,” alisema.

Aliwataka wateule hao kuelewa kuwa kuteuliwa na kutenguliwa ni jambo la kawaida katika nafasi walizonazo na kwamba aliyewateuwa ana uwezo wa kuwatengua.

“Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum, Nustrat Hanje alisema kwa yanayotokea sasa, ndio maana wapinzani wamekuwa wakishauri nafasi hizo ziwe za kuchaguliwa na sio kuteuliwa kama ilivyo sasa.

Alitaka jambo hilo kupigiwa kelele kwa sababu hakuna hoja ya kuacha kufanya kazi kwa madai ya kusubiri mkeka.

“Watu watekeleze wajibu wao. Umepata nafasi hujapata nafasi watu wako wengi. Ni wajibu wako kutumikia wananchi,’’ alisema.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad