Jaji Chande atia Neno Kesi Kama za Kina Mdee



Lushoto. Jaji Mkuu mstaafu, Chande Othman amewataka majaji wa Mahakama Kuu kumaliza haraka kesi wanazopangiwa, ili kuondoa wasiwasi kwa jamii na wao kujiweka huru.

Amesema ucheleweshaji wa kesi zikiwamo zenye mvuto huku akiitolea mfano kesi ya wabunge- Halima Mdee na wenzake 18 wanaopinga kuvuliwa uanachama wa Chadema, mbali na kuwapa wasiwasi wananchi, pia zinatoa nafasi kwa vyombo vya habari kuandika mengi.

Alitoa rai hiyo juzi wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi ya majaji 22 wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Zanzibar inayofanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).

Alisema kutokana na muundo wa Mahakama, jaji ndiye anayejipangia ratiba ya usikilizaji wa mashauri aliyopangiwa, kwa hivyo hana sababu ya kuchelewesha utoaji wa hukumu na kuwapa nakala ya hukumu walalamikaji ili kama hawajaridhika wakate rufaa .


“Jambo la msingi ni kuwa kila jaji wa Mahakama Kuu anajiendesha mwenywe kwa mashauri aliyopangiwa na siyo mawakili au wenye mashauri,” alisema Jaji Chande.

Alisisitiza kitu ambacho kinaweza kuwaacha huru majaji ni kutoa hukumu kwa haraka katika kesi au mashauri yenye mvuto ikiwamo kesi ya wabunge 19.

“Kesi yenye mvuto kwa jamii kama ya wabunge 19 ikisikilizwa haraka, hukumu ikatolewa na nakala ya hukumu ikaharakishwa, itatoa nafasi kwa upande ambao haujaridhika kukata rufaa,” alisema.

“Hii inaondoa wasiwasi kwa wananchi na presha kwa jaji aliyepangiwa kuisikiliza inaondoka,” aliongeza Jaji Chande.

Alichosema Balozi Mpungwe

Katika mafuzo hayo, Balozi mstaafu Ammi Mpungwe ambaye pia ni mkufunzi wa mafunzo hayo, alisema ongezeko la majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani Tanzania, litachochea uharakishaji shughuli za uwekezaji uchumi na biashara kwa kuwa mashauri yahusuyo migogoro ya kibiashara yatasikilizwa na kutolewa hukumu haraka.

“Tanzania siyo kisiwa, imeanza kufungua milango ya uwekezaji, hivyo ni wazi kuwa inaweza kujitokeza migogoro ya kibiashara zikiwamo za kimataifa hivyo ni jambo la busara kwa Mahakama Kuu nchini kuwaweka tayari majaji wake ili wasiwe sehemu ya ukwamishaji.

Alisema chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kimejitokeza kuwa taasisi pekee ya kimahakama kwa Afrika Mashariki, kuendesha programu zenye kuboresha utendaji kazi wa watendaji katika mahakama.


Naye, Jaji wa Mahakama kuu Zanzibar na Mahakama ya Biashara, Muumin Khamis Kombo alisema mafunzo hayo yataimarisha uchumi wa buluu kwa upande wa Zanzibar.

“Majaji kutoka Zanzibar tuliohudhuria mafunzo haya tutaweza kuchochea uharakishaji wa mashauri yatakayokuja ya kibiashara kusikilizwa kwa haraka, alisema Jaji Muumin.

Mkuu wa chuo hicho, Dk Paul Kihwelo, alisema mafunzo hayo elekezi yanahusisha majaji 22 wapya walioapishwa hivi karibuni, 18 wakitoka Tanzania Bara na wanne kutoka Zanzibar.

Kesi ya kina Mdee na wenzake

Mdee na wenzake 18, wamefungua shauri Mahakama Kuu Masjala Kuu, dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chadema.


Katika shauri hilo namba 36 la mwaka 2022, wanaiomba mahakama hiyo ipitie mchakato na uamuzi huo wa Chadema kuwafukuza kisha itoe amri ya kuutengua na kulazimisha Chadema kuwapa haki ya kuwasikiza.

Uamuzi huo wa Baraza Kuu ulitokana na rufaa walizozikata kina Mdee kupinga uamuzi wa awali wa kuwavua uanachama uliotolewa na Kamati Kuu, Novemba 27, 2020.

Walitiwa hatiani na chama hicho wakituhumiwa kwa kosa la kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum, bila ridhaa ya chama.

Licha ya kufunguliwa chini ya hati ya dharura tangu hatua za awali za kuomba ridhaa ya kufungua shauri la mapitio ya mahakama kupinga uamuzi wa Chadema kuwavua uanachama, shauri hilo limedumu kwa takribani miezi mitano sasa bila kuamriwa.

Hali hiyo inatokana pamoja na mambo mengine mapingamizi yaliyokuwa yanaibuliwa na wadaawa.


Kwa mara ya kwanza, Mdee na wenzake walifunga shauri hilo Mei 12, mwaka huu siku moja baada ya Baraza Kuu la Chadema kutupilia mbali rufaa zao kupinga uamuzi wa Kamati Kuu

Walikuwa wanaomba ridhaa ya kufungua shauri ya kupinga uamuzi huo wa Chadema kuwavua uanachama, kwa njia ya Mapitio ya Mahakama

Hata hivyo, maombi hayo yalitupiliwa mbali na Jaji John Mugeta Juni 22, mwaka huu baada ya kukubaliana na hoja za pingamizi la awali la Chadema, kuwa yalikuwa na kasoro za kisheria.

Juni 23, walifungua upya maombi hayo baada ya kurekebisha kasoro zilizoanishwa na mahakama, huku wakiyafungua chini ya hati ya dharura sana.

Maombi hayo yalisikilizwa na Jaji Mustapher Ismail Juni 30 na Julai 8 alitoa uamuzi ambapo aliwaruhusu kufungua shauri rasmi la kupinga kuvuliwa uanachama, ndani ya siku 14 ndipo Julai 21 wakafungua kesi hiyo rasmi.

Nyongeza James Magai
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad