Jakaya Kikwete "Membe Sio Ndugu Yangu"


RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, amefunguka mazito kuhusu masuala mbalimbali yakiwamo ya siasa za Tanzania, uhusiano na uswahiba wake na baadhi ya wanasiasa mashuhuri.

Kikwete alifunguka hayo jana wakati akihojiwa na Clouds Media Group, ikiwa ni siku yake ya kuzaliwa. Kikwete jana alitimiza miaka 72 tangu kuzaliwa kwake mwaka 1950.

Katika mahojiano hayo, alisema anashangaa kusikia kwamba Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kuwa ni ndugu yake.

“La kwanza ni kwamba, Membe siyo ndugu yangu. Hatuna undugu kabisa. Membe ni Mmwela na mimi ni Mkwere. Hakuna undugu, hata wanapokuja kusema mimi ni ndugu yake wa damu.

“Unajua mengine ni maneno ya siasa, nikawa ninashangaa kweli. Sina uhakika mimi na Membe tunafanana nini? Membe nimekuja kumfahamu baadaye sana maishani,” alisema.

Katika mahojiano hayo pia, Kikwete alizungumzia kinyang’anyiro cha urais uliohusisha vyama vingi hasa wa mwaka 1995, 2005 na 2015. Miaka hiyo ilikuwa ya kutafuta wagombea wapya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na waliokuwapo kumaliza muda wao wa vipindi viwili vya miaka mitano mitano kikatiba.

Kwa mujibu wa Kikwete, mwaka 1995 walikuwa wagombea 17 waliochukua fomu kuwania kuteuliwa na chama, mwaka 2005 walikuwa 11 na mwaka 2015 walikuwapo 42.

“Kwa utaratibu uliowekwa CCM, hatuwezi kupeleka wagombea wote 42. Kazi ya Kamati Kuu ni kuwa na watu watano. Tukawa na wanawake wawili, Balozi Amina Salum Ali na Dk. Asha-Rose Migiro na wanaume walikuwa watatu ambao ni January Makamba, Membe na Dk. John Magufuli ambaye alishinda na baadaye kupeperusha bendera ya CCM hatimaye kuibuka mshindi.

“Kwenye kamati ya maadili, kila mmoja aliangaliwa kwa sifa zake, uwezo wake, afya yake, tabia, makando kando na vitu vingine vingi, hatimaye tukaja na orodha ya watu watano. Tulipokwenda kwenye Kamati Kuu kukawa na mjadala mkubwa kwa nini huyu mmemwacha huyu, kwa nini mmewachukua hawa.


“Wakati huo wanasema, Magufuli hajawahi kuwa kiongozi kwenye chama hiki, kukawa na mjadala mkali kweli. Hajawahi kuwa hata balozi, hata kuwa mwenyekiti wa chama. Nilichofanya pale kila aliyetaka kuzungumza alizungumza.

“Wale wanaomtetea huyu, kwa nini (Edward) Lowassa kaachwa, walikuwa wanasema kwa nini (Dk. Mohamed Gharib) Bilal kaachwa, kwa nini (Mizengo) Pinda kaachwa, kwa nini (Stephen) Wassira hayumo.


“Tukazungumza mpaka tukafika mwisho, nikasema jamani tupige kura. Tukapiga tukapata majina matatu, tukapeleka kule, hakuna la zaidi ya utaratibu wetu wa kawaida.

“Kama mwenyekiti ndiyo kutengeneza ile orodha ya wale watano, orodha niliitengeneza mimi ile ya wale watano, mimi ndiye mwenyekiti. Ninashukuru tulijadiliana vizuri.

USHINDI WA MKAPA

Kikwete alisema alipotangazwa Benjamin Mkapa mwaka 1995 kuwa ameshinda kinyang’anyiro cha uteuzi wa urais, mwitikio ulikuwa tofauti, hivyo yeye aliona asiposema kitu chama kitagawanyika.

“Nikaandika kwenye karatasi nikamwambia mtu kampe Katibu Mkuu, Laurence Gama, ampe mwenyekiti ninaomba kuzungumza. Gama akaisoma akaiweka chini, nikaandika ya pili nikampa mtu nikamwambia nenda kampe Mzee (Kingunge) Ngombale (Mwiru), ampe mwenyekiti.

“Ngombale akampa Mzee (Ali Hassan) Mwinyi wakajadiliana kwa sababu tulikuwa watatu, wakajiandaa Msuya aseme lakini kwa sababu alikasirika sana hata maneno aliyokuwa anayasema unaona ana hasira. Ningetoka pale bila ya kuzungumza ingekuwa ngumu baada ya hapo kukiunganisha chama.

“Maana wakati ule ndio ulikuwa unasikia huko nje vijana wamevua mashati CCM ‘bye bye’. Ilikuwa mchanganyiko kweli. Ninakumbuka hata baada ya pale tumerudi kwenye kituo chetu, ninazungumza na timu yangu, mmoja akasema (simtaji jina) nipeni Konyagi akasema bora nife, siyo siri. Anna Makinda alisema kungekuwa na utaratibu wa mgombea binafsi, haki ya Mungu tungemsimamisha mgombea binafsi,” alisema.

“Wengine wakawa wanashauri tutafute chama kimoja tukajiunge huko. Nikasema mimi huko siendi, wengine wakasema tuchukue Baraza Kuu la Vijana CCM tuitishe mkutano tutangaze wote tumeondoka ndani ya CCM tuunde chama cha siasa, nikawaambia inayosajili hicho chama ni serikali hatutasajiliwa,” aliongeza.

Kikwete alisema aliwaeleza kuwa faida waliyo nayo yeye ana umri wa miaka 45 kama uhai upo na Mungu ndiye amemwandikia kuwa Rais miaka 10 ijayo atakuwa na umri wa Mkapa. Baada ya miaka 10 alishinda kwa kishindo ndani ya chama na hatimaye kuwa mgombea na kushinda uchaguzi kisha kuwa Rais wa Awamu ya nne.

“Tulivyokuwa kule hatua ya kwanza tumeshinda na habari ikafika pale, ninakumbuka walitengeneza karatasi fulani hivi zenye kaulimbiu ‘Kikwete kiongozi ambaye wakati wake umeshafika’. Ninakumbuka (Ukiwaona) Ditopile (Mzuzuri) alikuwa nayo mengi, baba yake Mange Kimambi (sasa marehemu) rafiki yangu sana, wale ndo walikuwa mashabiki wangu.

“Tumetoka Area D tunakuja mkutanoni wamefurahi vijana, walipofika pale wakaambiwa ndio tunarudia, wakaniuliza wamekuahidi nini nikawaambia hajaniahidi chochote.

“Aliyekwenda kunisimamia kule ni Isdore Shirima, alipotoka kwenye kuhesabu kura, akapita pale akanionyesha ishara kuwa mambo huko siyo mazuri, basi nikatulia tu. Hakukuwapo na mazungumzo sijui Mwalimu (Julius Nyerere) alimwita, akamwambia ‘subiri wewe kijana’ hayo hayakuwapo. Yale yalikuwa mawazo yangu tupu pale, kama nilivyosema niliandika vikaratasi viwili, cha kwanza nikampa Katibu Mkuu na cha pili Ngombale.

“Ndipo wakaanza kujadili, walikuwa na hofu kweli ninakwenda kusema nini. Waliangalia ile hali ya vijana na hakika ingekuwa ni kitu kimepangwa huko, wangekataa nisiseme,” alisema.

MAUAJI YANAYOENDELEA

Akizungumzia kuhusu matukio ya watu kujiua, Kikwete alisema si mambo mapya kwa kuwa yalikuwapo tangu zamani.

“Si kwamba sasa hivi ndiyo yanatokea sana. Yalikuwapo tangu zamani. Hili ni suala la kuhimili, wengine wana uwezo huo ikitokea amekataliwa basi anaendelea na maisha atatafuta mwingine.

“Hata masuala ya ndoa kuvunjika ni kushindwa kuhimili kwa kuwa kila mtu ana uwezo wake katika kuvumilia na kuyachukulia mambo,” alisema.

NDOA YAKE

Kuhusu ndoa yao, mke wake, Mama Salma (Mbumge wa Mchinga kwa tiketi ya CCM), alisema pamoja na upendo kutawala maisha yao, kikubwa kinachowafanya waendelee kuwa na furaha hadi sasa ni uvumilivu na kuwasisitiza vijana suala la uaminifu.

“Mimi simu yangu anapokea mume wangu kikubwa ni kuaminiana. Jiaminishe wewe ndiyo mke au mume hakuna mwingine zaidi yako,” alisema.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad