JUZI Kocha Juma Mgunda alikuwa na kazi ndogo tu ya kuiondoa Primeira de Agosto katika michuano ya Mabingwa wa Afrika na kisha kuiweka Simba katika hatua ya makundi. Subiri kwanza, ni kazi yake au kazi ya wachezaji au kazi ya viongozi? Tanzania swali hili lina majibu mengi.
Kuna mabosi hawataamini kama ni kazi yake. Wataamini ni kazi ya wachezaji zaidi. Ndivyo tulivyo. Haishangazi kuona mpaka sasa hivi mkataba wa Mgunda na Simba haupo wazi. Amesaini mkataba wa miaka mingapi Simba? Hatujui. Na kama hajasaini mkataba wowote je, Simba itampa mkataba? Hatujui.
Ninachofahamu mabosi wa timu tatu kubwa nchini, Simba, Yanga na Azam hawawezi kumpa mkataba mrefu kocha wa Kitanzania. Walishaondoka katika suala la imani ya kumfanya kocha mzawa awe kocha mkuu wa kudumu katika klabu zao. Wanachoweza kufanya ni kumpa nafasi ya usaidizi kwa ajili ya kuwa mkalimani wa wachezaji au kwa ajili ya kuwa mpelelezi wao dhidi ya mipango ya kocha.
Kwa nini? Haijulikani. Kwanza kabisa klabu hizi zina pesa. Zina uwezo wa kuwalipa makocha wageni. Hata kama hazina uwezo wa kuwalipa makocha kiasi cha pesa kama Dola 30,000 kwa mwezi kama wanavyolipwa kina Pitso Mosimane lakini wana uwezo wa kuwalipa makocha wa Dola 7,000.
Kama klabu zetu zingekuwa hazina pesa kiasi hiki zingebaki katika zama za wazawa. Wakati mwingine tunapata hisia kumbe umaskini wao tu ndio uliwafanya wawaamini kina Abdalah Kibadeni miaka hiyo. Kwa sasa pesa zinawawasha kiasi wanaamini makocha wageni ndio wenye uwezo zaidi kuliko wazawa.
Lakini imani ya kumpa timu Mgunda ina vikwazo vingi. Jaribu kufikiria kabla hawajamwamini Mgunda kumbuka kuwa hawawezi hata kumwamini kocha kutoka Uganda au Kenya. Kwamba kwa sasa kuna pengo kubwa la imani kati ya wazungu na makocha wazawa wa Bara la Afrika. Ni Yanga na Azam tu ndio ambao kwa miaka ya karibuni wamejaribu kuwaamini makocha kutoka Bara la Afrika.
Yanga walijipapatua kwa Mwinyi Zahera wakati ule walipokuwa hawana pesa. Wakaenda kwa Cedric Kaze na sasa wana Mohamed Nabi ambaye katika hisia zao wanamwona kama Mzungu tu. Azam walikuwa na George Lwandamina. Baada ya hapo wamepiga kona na kurudi Ulaya.
Lakini tukirudi kwa rafiki yetu Mgunda ukweli mpira wetu una mambo mengi na ndio maana kuna asilimia kubwa anaweza asipewe kiti cha ukocha moja moja. Ni kweli viongozi wanaamini yeye ndiye anayeshinda mechi? Tatizo hili wanalipata hata makocha wa Kizungu wanaofundisha klabu zetu kubwa.
Endapo timu zinashinda basi wanaomiminiwa sifa ni wachezaji. Ni kama sasa hivi tunavyowaimba kina Moses Phiri, Clatous Chotta Chama na Augustine Okrah. Timu ikifungwa tatizo litakuwa la Mgunda. Ni kama kelele za kumsakama Suleiman Matola zilivyotulia kwa sasa. Mgunda yupo katika fungate kwa sababu Simba inashinda.
Kuna viongozi ambao wanaamini Simba inashinda kwa sababu ya ubora wa wachezaji. Hawa ni kundi kubwa. Nawafahamu. Endapo Simba itapoteza mechi moja tu, hasa dhidi ya Yanga Oktoba 23 basi kelele dhidi ya Mgunda zitaanza. Uharaka wa kusaka kocha mpya utaanza kwa kasi kubwa.
Kuna viongozi pia ambao wataamini Simba inashinda kwa sababu wao wanafanya mambo mengi nje ya uwanja. Inanikumbusha mwaka fulani ambao watani wao waliwahi kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu lakini bado wakaacha wachezaji 14 na kisha wakamtimua na kocha. Mpira wetu ni mgumu.
Sioni pia Mgunda akipewa mkataba mrefu kama kocha wa kudumu wa Simba kwa sababu nyingine tofauti. Nadhani pia hana makeke. Hizi klabu zimeshazoea kuishi na makocha wengi wenye makeke ambayo kwao huwa yanawathibitishia mhusika ni kocha mkubwa mwenye mipango mikubwa.
Wanapenda kocha ambaye atakuwa na Kiingereza kingi, mikwara mingi ya ufundishaji lakini ambaye pia ni mkali hata kwa viongozi. Mgunda hawezi kuwa mtu wa namna hiyo na kama hauwi mtu wa namna hiyo wakati mwingine ni ngumu kwa viongozi kukuelewa.
Katika hili makocha wa Kitanzania huwa wamejitakia wenyewe. Wapo wengi ambao wanakubali kufanya kazi katika mazingira magumu kwa sababu inaonekana kama vile wamepewa nafasi zao kwa hisani tu. Kocha wa mzawa anaweza kukubali kufundisha timu akiwa na mipira mitatu tu. Kocha wa kigeni hawezi kukubali.
Kocha wa mzawa anaweza kukubali kufundisha huku mshahara ukiwa umechelewa. Kocha wa kigeni hawezi kukubali. Kufikia hatua hii mabosi wa timu wanamchukulia kocha wa mzawa kama mtu ambaye anazuga katika kazi yake. Wanaamini kocha mkali ndiye ambaye anaijua kazi yake vema.
Sioni Mgunda akienda katika makundi kama kocha mkuu wa Simba. Utaangaliwa pia wasifu wake wa kwamba hakuwahi kuipatia Coastal Union mafanikio yoyote zaidi ya kutinga fainali za Azam Sporst Federation Cup (ASFC) ambapo ilipoteza kwa matuta dhidi ya Yanga. Haitaangaliwa kwamba huenda angefanya vema zaidi kama angekuwa amekaa katika benchi la Yanga.
Haitaangaliwa alifanya juhudi kubwa akiwa katika timu ambayo haina bajeti kubwa kama Coastal Union. Labda kwa wachezaji hawa alionao Simba anaweza kufanya makubwa zaidi kwa sababu ni wachezaji wakubwa zaidi ya wale ambao alikuwa nao Coastal Union. Nani anaweza kuwa na imani hii?
Hata hivyo, licha ya kila kitu, bado hatuwezi kuacha kuwapongeza viongozi wa Simba kwa kumpa Mgunda timu katika kipindi hiki.
Hii nayo bado ni imani kubwa kwake. Hawa wakubwa wasingeshindwa kuvunja mkataba wa kocha yeyote wa kigeni aliyepo nchini na kumkabidhi timu. Hata hivyo, hawakufanya hivyo na wakamchukua Mgunda.
Labda hiyo dalili ya kuanza kuwaamini makocha wetu wa ndani lakini bado usicheze kamari ya kuwaamini viongozi wa Simba kama wataenda katika hatua ya makundi wakiwa na Juma Mgunda. Imani hiyo unaweza kuiweka kiporo mpaka wakati mwingine ujao. Sio sasa hivi.