JUZI jioni Yanga iliwatoa majumbani mwao mashabiki zaidi ya 55,000 na kuwapeleka Benjamin Mkapa, kwa ajili ya kile walichokiita ‘kutengeneza’ hali safi ya hewa katika uwanja huo wa nyumbani kwenye pambano la raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal ya Sudan.
Bahati mbaya, mashabiki waliwapa Yanga walichotaka, lakini wachezaji na benchi la ufundi halikuwapa mashabiki walichostahili. Tuanzie wapi? Labda tuanze kwa timu kwa ujumla. Sijui ni kwa sababu zipi lakini Yanga ilicheza chini zaidi.
Ilimtenga Fiston Mayele kwa muda mwingi wa mchezo. Utundu ulitoka kwa Bernard Morrison na walau Jesus Moloko, ila kwa ujumla timu ilikuwa chini zaidi. Yanick Bangala alicheza kama beki wa kati pamoja na Dickson Job.
Khalid Aucho akacheza chini ya Fei Toto ambaye katika miezi ya karibuni amekuwa akicheza mbele na kuwa na madhara makubwa langoni mwa wapinzani. Amekuwa akifunga mabao ya kuburudisha zaidi.
Mbele yao alicheza Stephane Aziz Ki. Hata hivyo, kulikuwa na pengo kubwa kati ya eneo la chini na kule mbele. Al Hilal ilikuwa bora ikiwa na mpira, pia ilitumia mwanya wa daraja lililopo baina ya viungo wa chini wa Yanga na wale wa mbele kutengeneza mashambulizi.
Licha ya utundu wa hapa na pale kutoka kwa Morrison lakini ukweli ni kwamba Al Halal ilikuwa imejaza watu wengi eneo la nyuma kiasi cha kumfanya Mayele kuwa mpweke. Ni hadi Mayele alipoamua kufanya maajabu mwenyewe katika kipindi cha pili ndipo Yanga ilipopata bao la kuongoza.
Tatizo kubwa kwa Yanga ni kwa mfumo wa Kocha Nasreddine Nabi pamoja na kushindwa kwake kuchukua maamuzi magumu. Mastaa wengi wakubwa waliletwa Yanga kwa ajili ya kazi kama hii. Msimu uliopita ilitolewa mapema na Rivers United ya Nigeria kwa sababu ya visingizio vya hapa na pale.
Msimu huu Yanga ina kila kitu. Ilikuwa na kila mchezaji iliyemhitaji. Msimu uliopita Mayele na Aucho hawakupata leseni. Pia, michuano ilianza kabla hata ligi haijaanza na maisha yakawa magumu kwa sababu wachezaji hawakuwa fiti.
Msimu huu Yanga ilikuwa na kila maandalizi ikiwemo kuongeza mastaa ambao wanaonekana kuwa na hadhi hii lakini tatizo mastaa wenyewe hawakujitokeza pale walipohitajika kushughulika na hadhi ya mechi hii.
Mmojawapo alikuwa Aziz Ki. Mechi hii alishindwa kuiamua kama alivyokuwa anaamua mechi za ASEC Mimosas. Inasemekana alipata maambukizi ya Uviko-19 wakati amekwenda kwao kuichezea Timu ya Taifa ya Burkina Faso. Ukweli ni kwamba Ki alionyesha kiwango kibovu.
Hakuweza kukaa na mipira wala kuiunganisha vema safu ya kiungo na ushambuliaji. Nabi alipaswa kufanya maamuzi magumu ya kumtoa Ki pale mbele na kisha kumuingiza kiungo mwingine ambaye angecheza chini na Aucho kisha Fei asogee mbele. Na mtu huyo alistahili kuwa Salum Abubakar!
Baadaye Job akafanya kosa ambalo liliigharimu Yanga bao la kusawazisha kutoka kwa Wasudan. Krosi iliyopigwa kutoka Magharibi mwa uwanja alimtulizia adui. Ni makosa ambayo Job huwa anayafanya kwa nadra, lakini yalinikumbusha kitu.
Katika hadhi ya michuano hii dhidi ya timu kama Al Halal hauruhusiwi kufanya kosa kama lile alilofanya. Wapinzani wanakuadhibu. Unaweza kucheza dhidi ya Polisi Tanzania ukafanya kosa kama lile na bado mshambuliaji wake akakosa bao. Hauwezi kufanya kosa kama lile dhidi ya Al Hilal, Zamalek, Al Ahly, Waydad na wengineo.
Baada ya kosa lile la Dickson, nusura Wasudan wapate mabao mengine kama si uhodari wa kipa wa Yanga, Djigui Diarra. Kwangu ndiye alikuwa Nyota wa mchezo. Na pengine Diarra, Mayele na Morisson ndio wachezaji waliofanya kile kilichohitajika katika michuano ya hadhi hii.
Diarra alikuwa imara langoni. Alicheza michomo mingi, pia usambazaji wake wa mipira ulikuwa wa daraja tofauti kabisa. Ni mtu ambaye kwa namna moja au nyingine ameipa nguvu Yanga kucheza pambano la marudiano Khartoum walau ikiwa na mtaji wa sare. Vinginevyo Yanga ilistahili kufungwa katika dakika za mwisho.
Kitu kikubwa cha kujifunza kuelekea katika mechi hii ni kwamba Yanga haikujiandaa vema kuikabili timu ya kiwango cha Al Hilal. Ingeweza kufanya kazi. Ni vile ratiba ya ligi ilikuwa ngumu, lakini ingeweza kupata mechi nyingi zaidi za kirafiki.
Tofauti ya Al Hilal na timu kubwa na ndogo za ligi yetu ni kubwa. Yanga ilizoea kucheza dhidi ya timu za ligi yetu na pia ilipata mteremko wakati ilipokabiliana na Zalan ya Sudan Kusini katika mechi ya awali. Ukweli ni kwamba Al Hilal ilikuwa maji ya kina kwa Yanga.
Nini kitatokea Khartoum? Kwanza Yanga ikubaliane na ukweli itakuwa na mechi ngumu. Mechi ya machozi, jasho na damu. Inabidi ijitume zaidi ya mara mbili ilivyofanya hapa. Itacheza katika ardhi ambayo ina chuki dhidi ya wapinzani.
Faida pekee kwa Yanga ni kwamba walau katika mechi hiyo Al Halal inaweza kupunguza umakini iliyokuwa nao juzi katika eneo la kujilinda. Ni lazima itacheza soka la kasi kuhakikisha inapata mabao ya haraka haraka katika kipindi cha kwanza na kuimaliza mechi wakati wa mapumziko.
Hilo linaweza kuwa na faida kwa Yanga katika kufanya mashambulizi ya kushtukiza ukizingatia Tuisila Kisinda, Morrison pamoja na Moloko ni wachezaji wenye kasi. Juzi hakukuwa na nafasi kubwa kwao kwa sababu Al Hilal ilikuwa imejiandaa na jambo hilo kwa muda mrefu.
Kitu kingine ambacho Nabi inabidi ajiandae nacho Sudan ni uwezekano wa kuchukua maamuzi magumu. Yupo katika michuano ambayo kila mchezaji anahitaji kuwa na utimamu wa mwili na akili. Kama Aziz Ki hayupo katika hali hiyo unaweza kumweka nje.
Kuweka matumaini hai pale Khartoum, Yanga ilipaswa kushinda kwa tofauti ya mabao mawili. Ilipaswa kuongeza bao jingine baada ya Mayele kufanya kazi yake ya bao la kwanza.
Hata hivyo, bahati mbaya Job alifanya uzembe na wao pia wakashindwa kuongeza bao jingine. Na sasa wanaweza kujiandaa na ubatizo wa moto pale Khartoum.
Mwanaspoti