Mlinda Lango Juma Kaseja ametangaza rasmi kustaafu soka la ushindani baada ya kudumu kwenye Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa zaidi ya miaka 22.
Kaseja aliyetamba kwa jina la ‘Tanzania One’ ametangaza maamuzi hayo, baada ya kukosa nafasi ya kusajiliwa kwenye klabu za Ligi Kuu msimu huu 2022/23, akiachana na KMC FC iliyoitumikia kwa misimu miwili mfululizo.
Mkongwe huyo amesema amechukua maamuzi ya kustaafu soka la ushindani baada ya kuona anahitaji muda wa kupumzika, lakini amesisitiza ataendelea kuonekana katika medani ya soka katika nyanja mbalimbali.
“Bado nina uwezo wa kucheza michezo ya ushindani na kufanya vizuri lakini kwa sasa nimeamua kupumzika.”
“Pamoja na kuacha kucheza michezo ya kiushindani kwa sasa nitaendelea kuwa kwenye familia ya soka na kufanya majukumu mengine, pia nitakapohitaji kucheza nitacheza tu, kwani bado nipo ‘FIT’.” amesema Kipa huyo
Kasema ametwaa mataji saba ya Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na Klabu ya Simba SC katika misimu ya 2003, 2004, 2007 (Ligi Ndogo), 2010 na 212.
Pia amewahi kutwaa mataji mawili ya Michuano ya Tusker ‘TUSKER CUP’ mwaka 2003 na 2005.
Akiwa Young Africans aliwahi kutwaa Ubingwa wa Tanzania Bara mara moja, msimu wa 2008/09 na kuwa Mlinda Lango mwenye mafanikio zaidi nchini Tanzania.
Kaseja alianza kuonekana katika soka la ushindani mwaka 2000 akiitumikia klabu ya Moro United aliyojiunga nayo ikiwa Ligi Kuu Tanzania Bara, akitokea Shule ya Sekondari ya Makongo na kucheza kwa msimu mmoja, kisha kujiunga na Simba SC aliyoitumikia kwa mafanikio makubwa zaidi kwa miaka 10.
Kaseja pia aliwahi kuitumikia Young Africans katika vpindi tofauti kama ilivyo kwa Simba SC na baadae alijiunga na Kagera Sugar, kisha Mbeya City na kumalizia soka lake KMC FC mwishoni mwa msimu uliopoita.
Kwa sasa Kaseja ni sehemu ya jopo la makocha wanaounda Benchi la Ufundi la muda la Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ chini ya Mzambia Honour Janza akisaidiana na Mzawa Mecky Mexime