MWENYEKITI wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage anafahamika kwa kuikandia Yanga hasa linapokuja suala la watani wa jadi, jana mwamba huyo amekiri kikosi cha Jangwani kina majembe ya maana na anaiona kabisa ikiitubua Al Hilal ya Sudan.
Rage na nyota wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Said Maulid ‘SMG’ wamesema wana imani na watetezi hao wa Ligi Kuu Bara, Yanga kuitoa Al Hilal katika mechi za raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Timu hizo zinakutana kesho Jummosi Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa mchezo wa mkondo wa kwanza kabla ya kurudiana wiki ijayo na itakayopata matokeo mazuri itatinga makundi na atakayepoteza itaenda kucheza play-off ya Kombe la Shirikisho kuwania makundi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Rage aliyewahi kuwa Mbunge wa Tabora Mjini alisema Yanga ina kikosi imara chenye uwezo wa kucheza na timu yoyote Afrika kwa sasa, hivyo hana budi kuipa nafasi ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo.
“Yanga imeimarika kwani ina timu nzuri sana msimu huu, hivyo nina imani inaweza kupata matokeo chanya na kuivusha hatua ya makundi kwani Tanzania kwa ujumla tumedhamiria kuona klabu zetu zikifika hatua hiyo,” alisema Rage akisisitiza licha ya unazi wake wa Msimbazi, lakini kwa mziki wa Yanga anaamini inatoboa ikikaza buti.
Kwa upande wa SMG alisema hana shaka na ubora wa Yanga msimu huu ingawa amewataka wachezaji kujituma zaidi ili washinde mabao mengi ili kurahisisha mchezo wa marudiano.
“Nawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kujaa kwao na kuishangilia kutawafanya wapinzani wetu kuingiwa na hofu na kuwapa wachezaji wetu nguvu,” alisema.
Al Hilal imetua nchini jana jioni ikitokea DR Congo ilipoweka kambi ya siku wiki moja ikicheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Don Bosco na AS Vita Club ikiwa ni maandalizi kwa ajili ya mchezo huo.
Kikosi hicho kinachoongozwa na Kocha Mkuu, Florent Ibenge kimetua na wachezaji 23, benchi la ufundi lenye watu wanane na viongozi saba.
Yanga ilitinga hatua hiyo kwa kuiondosha Zalan FC ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao tisa, Al Hilal aliitoa Saint George ya Ethiopia kwa bao la ugenini baada ya kupoteza 2-1 ugenini na kushinda 1-0 nyumbani.
Al Hilal na Yanga hazijawahi kukutana kwenye michuano ya CAF, lakini kwenye Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), Yanga ikishinda mbili, ikipoteza moja na sare