Kikosi Kazi chapendekeza hatua sita kupata Katiba Mpya



Rais Samia Suluhu Hassan
KIKOSI kazi cha kukusanya maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi nchini Tanzania,  kimependekeza hatua sita zitakazosaidia mchakato wa kupata Katiba mpya licha ya kubainisha uwepo wa maoni tofauti ya wananchi kuhusu suala hilo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hatua hizo ni pamoja na uwepo wa mjadala wa kitaifa kuhusu masuala ya msingi, kuhuishwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Sheria ya Kura ya Maoni, kuundwa kwa jopo la wataalamu watakaoratibu masuala ya msingi na kuja na rasimu, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujadili rasimu na kuja na Katiba Pendekezwa, elimu ya uraia na kura ya maoni.

Hayo yamebainishwa leo Ijumaa tarehe 21, Oktoba 2022, na  Mwenyekiti wa Kikosi Kazi, Profesa Rwekaza Mkandala, wakati akiwasilisha ripoti kwa Rais Samia Suluhu Hssan Ikulu jijini Dar es Salaam.

Prof. Mkandala amefafanua kuwa katika hatua ya kwanza ya mjadala wa kitaifa, yapo masuala muhimu wanayopendekeza yajadiliwe ikiwemo; Muundo wa Muungano, Madaraka ya Rais, masuala ya uchaguzi na mengineyo yatakayobainishwa.


Katika hatua ya pili ya kurekebisha Sheria amesema zitasaidia kubainisha mchakato mzima ikwemo muda wa mchakato wa Katiba, kutambua kuanzishwa kwa jopo la wataalamu na kuanisha misingi ya kuzingatiwa katika mchakato.

Kikosi Kazi
Kuhusu kuundwa kwa jopo la wataalamu, ambayo ni hatua ya tatu wamependekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar aunde jopo litakalopitia na kuoanisha Katiba Pendekezwa na Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya ili kuandaa Rasimu itakayopelekwa bungeni kujadiliwa kabda ya kupitishwa kwaajili ya kura ya maoni.

Prof, Mkandala amesema wamekuja na hatua hizo baada ya kupokea maoni mchanganyiko kutoka kwa watanzania kupitia wadau wa siasa nchini.


Mwenyekiti wa Kikosi Kazi, Profesa Rwekaza Mkandala amesema Watanzania wamegawanyika katika makundi mawili wakiwemo wanaotaka marekebisho ya katiba iliyopo na wale wanaotaka kuwepo kwa Katiba mpya.

Aidha amesema watanzania wamegawanyika katika makundi matano kuhusu njia ya kupata katiba mpya wakiwemo wanaopendekeza mchakato kuanza upya na kwamba utekelezaji wa mchakato huo unahitaji muda na gharama.

Amesema baadhi ya wadau walipendekeza kuwa mchakato uendelee pale ulipoishia na kwamba mtazamo huo ungeweza kupunguza gharama.

“Lakini mtazamo huu una changamoto kwamba ni takribani miaka minane tangu Katiba inayopendekezwa upitishwe na huenda ikawa imepitwa na wakati,” amesema.



Amesema wapo waliopendekeza Katiba pendekezwa ifanyiwe marekebisho ili iendane na wakati uliopo kwani tangu ipatikane kumefanyika uchaguzi mara mbil ambazo zimetoa uzoefu wa aina mbalimbali unaoweza kuboresha Katiba Pendekezwa.

Ameongeza kuwa baadhi ya wadau walipendekeza kuwa mchakato uendelee kwa rasimu ya pili ya Katiba kupigiwa kura ya maoni na wananchi. Kwa maoni ya kikosi kazi amesema mtazamo huo hautekelezekeki kwani unakiuka utaratibu ulioanishwa na Sheria ya mabadiliko ya Katiba ambayo inaelekeza rasimu hiyo kuwasilishwa katika Bunge maalum la Katiba.

Prof. Makandala amebainisha kuwa baadhi ya wadau walipendekeza kuundwa kwa jopo la wataalam watakao oanisha Katiba Pendekezwa na Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya ili kupunguza gharama na kwamba jopo hilo liandae rasimu mpya.

Aidha amesema wapo waliosema hakuna haja ya katiba mpya bali katiba iliyopo ifanyiwe marekebisho ili iendane na wakati uliopo.





Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad