Kina Mdee, Chadema kuendelea kukabana koo mahakamani



Dar es Salaam. Kesi ya wabunge19 wa viti maalumu waliofukuzwa uanachama katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) dhidi ya chama hicho inaendelea tena leo Ijumaa Oktoba 21, 2022 huku pande hizo zikitarajiwa kuendelea kukabana kwa hoja, wakati wa mahojiano.

Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea katika hatua ya mahojiano ambapo mawakili wa Chadema wataendelea kumhoji shahidi wa pili wa upande wa walalamikaji, aliyekuwa Makamu mwenyekiri wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) Hawa Mwaifunga, kuhusiana na ushahidi wake kwa njia ya kiapo.

Wabunge hao akiwemo Halima Mdee ambaye alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), na wenzake 18 wamefungua shauri hilo Mahakama Kuu Masjala Kuu, wakipinga kufukuzwa uanachama, kwa utaratibu wa Mapitio ya Mahakama (Judicial Review).

Hata hivyo jopo la mawakili wa Chadema linaloongozwa na Peter Kibatala liliomba mahakama na ikaridhia na kuwaamuru wabunge hao wanane kati yao akiwemo Mdee wafike mahakamani kwa ajili ya kuwafanyia mahojiano kuhusiana na ushahidi wao yaani malalamiko yao waliyoyato kwenye viapo vyao.


Mwaifunga alianza kuhojiwa na kiongozi wa jopo la mawakili wa Chadema, Peter KIbatala Alhamisi iliyopita Oktoba 13, lakini baadaye kabla ya kumaliza kumhoji, wakili Kibatala aliiomba mahakama hiyo ahirisho na jaji Cyprian Mkeha akapanga kuendelea leo.

Kabla ya Mwaifunga wa kwanza kuhojiwa alikuwa ni aliyekuwa Katibu wa Bawacha, Grace Tendega.

Wengine walioitwa kuhojiwa ni Halima Mdee, Nusrati Hanje, Ester Matiko, Ester Bulaya, Jesca Kishoa, na Cecila Pareso. Wabunge hao wanawakilishwa na mawakili Ipilinga Panya, Aliko Mwamanenge, Edson Kilatu na Emmanuel Ukashu.

Katika kesi hiyo wanapinga uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema wa Mei 11, 2022, kutupilia mbali rufaa zao za kupinga uamuzi wa Kamati Kuu wa Novemba 27, 2020 kuwafukuza uanachama kwa tuhuma za kuapishwa kuwa wabunge bila ridhaa ya Chama.

Hivyo wanaiomba mahakama itengue mchakato na uamuzi huo, iamuru Chadema kutimiza wajibu wake kisheria, yaani kuwapa haki ya kuwasikiliza na itoe zuio kwa Spika na Nec kuchukulia hatua yoyote mpaka malalamiko yao yatakapoamuriwa.

Mbali na Chadema kupitia Bodi yake ya  Wadhamini, wadaiwa wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambaye pia anasimama niaba ya Bunge la Tanzania; na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad