Beki wa Kulia wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Djuma Shaban amelalamikiwa kwa kushindwa kujitunza na kuruhusu mwili wake kuongezeka uzito kupita kiasi.
Lawama hizo kwa Beki huyo kutoka DR Congo zimetolewa na Mwinyi Zahera aliyewahi kuwa Kocha Mkuu wa Young Africans, alipohojiwa na EFM kupitia Kipindi cha Sports HQ, mapema leo Jumanne (Oktoba 18).
Zahera ambaye amewahi kufanya kazi na Djuma Shaban mara kadhaa wakiwa timu ya taifa ya DR Congo amesema, amewahi kumshauri Beki huyo kupunguza uzito, ili aweze kurejea katika umbo lake lililozoeleka lakini imeshindikana.
Amesema wakati akimshauri hivyo, aliwahi kumwambia hataweza kucheza michezo mikubwa yenye ushindani kama ya Ligi ya Mabingwa ama Kombe la Shirikisho hasa atakapokutana na Kiungo Mshambuliaji wa timu pinzani mwenye kasi kubwa.
“Namwambia mara kwa mara Djuma Shabani kwanza ananenepa sana amekuwa mzito, hawezi kucheza mechi ngumu kama na Al Ahly, Esperance, Wydad. Djuma hana tena speed kama atakutana na winga ana akili sana hawezi kugusa mpira hata mara moja.” amesema Zahera
Djuma Shaban alikua sehemu ya kikosi cha Young Afrcans kilichocheza Michezo ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Mabingwa wa Sudan Al Hilal Jumapili (Oktoba 08) na (Oktoba 16), ambayo ilishuhudia Mwananchi aking’olewa kwenye Michuano hiyo kwa ushindi wa jumla wa 2-1.