Kocha Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nassredine Nabi (kulia) akiongea jambo.
KOCHA Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nassredine Nabi, amekiri kuwa, leo Jumapili huenda kukawa na mabadiliko kutoka katika kikosi kilichocheza mchezo wa kwanza wa ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal.
Yanga leo Jumapili itarudiana na Al Hilal katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Al Hilal, Sudan ambapo mshindi atafuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo kufuatia sare ya 1-1 mechi ya kwanza.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Dar wikiendi iliyopita, kikosi cha Yanga kilichoanza kilikuwa hivi; Djigui Diarra, Djuma Shaban, Kibwana Shomari, Dickson Job, Yannick Bangala, Khalid Aucho, Jesus Moloko, Feisal Salum, Fiston Mayele, Stephane Aziz Ki na Bernard Morrison.
Mchezaji wa Yanga, Jesus Moloko.
Kuelekea mchezo wa leo unaotarajiwa kuanza saa 3:00 usiku kwa saa za hapa nyumbani, Nabi amesema mchezo wa ugenini upo tofauti na wa nyumbani jambo ambalo linaweza kupelekea mabadiliko ya kikosi, huku akimini wachezaji wote wapo tayari kwa ajili ya mapambano ya kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.
“Mchezo wetu wa sasa ni wa ugenini, mara zote kuna utofauti mkubwa wa michezo ya ugenini na ile ya nyumbani, hivyo hata kama kutakuwa kuna mabadiliko basi litakuwa ni jambo la kawaida.
“Mashabiki wa Yanga tunafahamu ni kwa jinsi gani wanatamani kuona mabadiliko makubwa ya wachezaji kutokana na matokeo ya kwanza, lakini kama timu ingepata matokeo mazuri yote hayo yasingetokea.
“Matarajio ya wachezaji wetu kutupa kile tunachokihitaji ni makubwa, tunaamini kila kitu kitaenda sawa,” alisema kocha huyo.
STORI NA MARCO MZUMBE