HATIMAYE aliyekosa sifa za kuwa mgombea urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ally Mayay Tembele ameenda kuwa bosi wa shirikisho hilo pale Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Maisha ni mzunguko ambao hakuna anayejua kesho yake.
Watu wanaweza kukunyima ndizi, kesho Mungu akakupa mkungu mzima wa ndizi. Kwenye uchaguzi mkuu wa TFF, Mayay alienguliwa kugombea nafasi hiyo kutokana na kile kilichoelezwa kwamba alikosa vigezo vilivyowekwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, lakini Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mohammed Mchengerwa amemteua kuwa kaimu mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini. Kwa uteuzi huo Mayay anakwenda kuwa bosi wa TFF na vyama vyote vya michezo nchini. Ndivyo mzunguko wa maisha ulivyo. Kuna kitu cha kujifunza hapa. Kuna watu unawaona leo wakiwa chini usiwadharau kwa sababu hakuna anayejua kesho yao.
Kuna watu wako chini yako leo, kesho ni mabosi wako. Kaa kwa kutulia. Jitahidi kuwa mtu wa haki kila upatapo nafasi. Maisha yanabadilika ndani ya muda mfupi. Kutoka juu kwenda chini ni sawa na kutoka chini kwenda juu. Tumia wakati wako vizuri. Saidia watu hasa waliopo chini lakini tenda haki kwa wote. Ni vigumu sana nchini kumpata mtu ambaye hafungamani na Simba na Yanga. Wanaweza kuwepo, lakini ni wachache sana. Tanzania tunahitaji watu waadilifu kwenye michezo. Mayay ni mwanachama wa Yanga, lakini huenda ni moja kati ya watu wachache wanaoheshimiwa sana na watu wa Simba.
Mayay anabebwa zaidi na uadilifu wake. Hii nafasi aliyopewa na Mchengerwa ni nafasi nyeti sana. Ndiyo inayotoa dira na mwelekeo wa michezo nchini. Sio mpira wa miguu tu, ni michezo yote. Kwa sasa Mayay ni bosi wa michezo yote. Kwa sasa Mayay ni bosi wa TFF. Kuna wakati Mungu anakunyima ndizi ili akupe mkungu mzima.
Moja kati ya kazi kubwa za Kurugenzi ya Michezo ni kutunga sera zinazoendana na wakati uliopo na kuangalia mahitaji ya wakati ujao. Bado sera zetu za michezo hazizungumzii michezo kwenye mtazamo wa kiuchumi. Bado hazizungumzii michezo kama ajira. Haya ndiyo maeneo ya kwanza ambayo nadhani Mayay atakwenda kuanza kushughulika nayo.
Pamoja na kustaafu kucheza soka muda mrefu Mayay bado ameendelea kuiishi michezo. Ni sehemu yake ya maisha. Kuifuatilia kila siku na kuichambua kila siku, lakini pia kuisoma kila siku. Huu ni moja ya uteuzi bora kufanywa kwenye michezo katika kipindi cha hivi karibuni. Kukosa sifa za kugombea urais wa TFF na upande wa pili kuteuliwa kuwa bosi wa TFF kuna ujumbe hapa tunapatiwa. Bado mifumo ya kuwapata wataalamu kwenye mpira wetu imejaa uhuni. Mchakato wa kupata viongozi bora pale TFF na vyama vingine vya michezo ni umafia.
Tunapoteza wataalamu wengi kwa sababu ya mifumo mibovu ya kupata viongozi. Watu kama kina Mayay wapo wengi tu kwenye ngumi, riadha, kikapu na maeneo mengine. Hatuwapati kuja kutuongoza kwa sababu ya ubabaishaji mkubwa uliopo kwenye michakato yetu ya uchaguzi.
Mtu kama Mayay alipaswa kuwa rais wa TFF muda mrefu sana, lakini mifumo ya uchaguzi ikakataa. Nafasi ya juu kabisa imekuja ni muda wake sasa kuthibitisha uwezo wake. Jukumu zito sasa limekuja ndiyo wakati wake kuonyesha weledi. Pamoja na kucheza mpira kwa mafanikio Mayay alipata pia nafasi ya kwenda shule.
Kuhitimu shahada ya uzamili kwa mwanamichezo sio jambo dogo. Sio watu wote wanaweza kusoma na kucheza kwa wakati mmoja. Tuna wanamichezo wengi ambao shule hawakwenda. Ni ngumu kwa mfumo wetu kucheza mpira na kusoma. Ukimuona mwanamichezo aliyecheza kwa mafanikio na kubahatika kwenda shule kama Mayay umheshimu.
Nampongeza Mayay kwa uteuzi huo, lakini nadhani ni wakati wake pia wa kutengeneza kurugenzi iliyojaa wataalamu pale wizarani. Moja kati ya michezo yenye wapenzi wengi nchini ni ngumi. Huku kumejaa usela mwingi. Bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kusafisha ngumi za Tanzania. Sera za kisasa ni muhimu ili kupunguza usela na uhuni. Kama mipango mathubuti itawekwa huku kuna pesa nyingi tutaitengeneza kama nchi. Ngumi huenda ndiyo mchezo namba mbili nyuma ya soka kwa wapenzi nchini. Riadha nako kiwango kinashuka siku hadi siku. Wakimbiaji wakubwa nchini wamebaki kutoka kwenye majeshi tu. Hatuoni shule zikizalisha damu changa. Ni lazima kutengeneza sera za michezo ambazo zitakwenda kushirikisha Wizara ya Elimu kwa utekelezaji. Haiwezekani nchi ikawa inategemea wakimbiaji kutoka jeshini. Lazima riadha iweze kuwapa vijana ajira.
Lazima riadha iweze kujitosheleza. Kuna mbio tunakosa washiriki kwa sababu wanakuwa na kozi jeshini. Sio mwelekeo mzuri kwa riadha. Tunahitaji kugeuza riadha kuwa ajira rasmi. Jukumu la kutuandalia sera na kwenda kusimamia utekelezaji wake sasa lipo chini ya Mayay. Hongera sana bosi mpya wa TFF, nenda ukasimamie kurugenzi na kuleta utofauti.