Dejan aibua kasheshe mpya Simba



STRAIKA Dejan Georgijevic aliyejiondoa ghafla Simba, ameshindwa kuondoka nchini juzi usiku kama alivyopanga kutokana na kushindwa kuafikina na mabosi wa klabu hiyo walioamua kujibu mapigo, lakini akifichua kuna uwezekano wa kukimbilia CAF na FIFA kama mambo yatakwama.

Dejan aliliambia Mwanaspoti kwamba amekwama kuondoka juzi kutokana na kushindwa kupatiwa nyaraka muhimu baada ya kusitisha mkataba kutokana na alichodai kukiukwa kwa baadhi ya vipengele alivyokubaliana na klabu hiyo kabla ya kusaini mkataba wa miaka mitatu.

Kabla ya kuwaeleza viongozi kuwa anataka kufanya uamuzi wa kusitisha mkataba, Dejan juzi asubuhi aliandika kwenye mitandao ya kijamii jambo ambalo viongozi wa Simba walieleza halikuwa sahihi kutokana na taratibu za kuvunja mkataba kama walivyokubaliana na wao kumchenjia.

Katika taarifa ya klabu kwa umma uongozi wa Simba umesema Dejan ndiye aliyevunja mkataba na kuamua kuondoka bila hata kuwataarifu na walikuwa wakiwasiliana na wanasheria wao kuhakikisha wanaipata haki yao wakati mchezaji huyo akikwama kuondoka nchini kama alivyopanga.


Sababu zilizomkwamisha Dejan kuondoka ni kutokana na kushindwa kukamilisha taratibu za kuachana na Simba ikiwemo kupatiwa barua ya kusitisha mkataba, barua ya kuonyesha ni mchezaji huru pamoja na mambo mengine ya msingi kwa pande zote mbili kama walivyokubaliana hapo awali.

Kutokana na hali ilivyo kama watashindwa kuafikiana pande zote mbili huenda wakafikishana hadi Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kwa kila mmoja kwenda kulalamika kuonekana mwenzake hakutenda haki kulingana na makubaliano ya mkataba wao.

Dejan huena akaibukia CAF, kueleza hakutimiziwa mahitaji yaliyokuwa katika mkataba wake wakati Simba wao huenda wakamshtaki mchezaji huyo amevunja mkataba nje ya taratibu ambazo walikubaliana.


“Ngoja tuone, lakini sijaondoka kwa sababu zilizo nje ya uwezo wangu,” alisema Dejan kwa kifupi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez kupitia ukurasa wa timu hiyo alieleza; “Uongozi wa Simba umepokea taarifa ya mchezaji Dejan ya kuvunja mkataba na klabu yetu. Hata hivyo tumesikitishwa na kitendo cha Dejan kuandika taarifa ya kuvunja mkataba kupitia mitandao ya kijamii bila hata ya kufanya mazungumzo na waajiri wake,” ilisomeka taarifa hiyo ya klabu ya Simba.

“Uongozi utachukua hatua stahiki juu ya mchezaji huyo kufuatia kuvunja mkataba bila kufuata utaratibu maalumu.”

Wakili msomi, Aloyce Komba alisema huenda kuna vitu kwenye mkataba wa Dejan havikutimizwa ndio maana mkataba huo ulikuwa umevunjika kutokana na kwenda tofauti ya makubaliano kabla ya kusainiwa.


“Huenda kuna maslahi ya mchezaji hayakwenda sawa ndio maana Dejan aliamua kufanya uamuzi huo na hata alichoandika kwenye mitandao wala hakikuwa na shida labda kuwe na katazo la kuzuiwa kuongea na vyombo vya habari katika mkataba wake,” alisema Komba.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad