Kwa mziki huu mtapigwa kama ngoma, ushindi uko hapa




YANGA ina dakika 90 muhimu za ama kukata mnyororo unaoitesa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ama kuuacha uendelee wakati itakapoikaribisha Al Hilal ya Sudan kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 10:00 jioni.

Ushindi wa utofauti mkubwa wa mabao katika mchezo huo wa nyumbani leo, hapana shaka utaiweka Yanga katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya makundi ya mashindano hayo makubwa zaidi kwa ngazi ya klabu Afrika msimu huu.

Na ikiwa hiyo, Yanga itavunja rasmi unyonge ulioisumbua kwa miaka 23 wa kutoingia hatua hiyo tangu ilipofanya hivyo mwaka 1998 ambapo baada ya hapo haikuweza tena ingawa mwaka 2016 na 2018 iliingia katika hatua hiyo kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Hata hivyo, mashabiki wa klabu hiyo wana mzuka mwingi baada ya kukichungulia kikosi na kuona ni mziki mnene ambao kama Al Hilal itakaa vibaya itapigwa kama ngoma, licha ya ukweli kwamba pambano hilo ni gumu kutokana na aina ya timu inayokabiliana nayo Kwa Mkapa.


USHINDI UKO HAPA

Jeuri kubwa ya Yanga katika mchezo wa leo ni safu zake za kiungo na ushambuliaji ambazo zimekuwa chachu kwao kufanya vyema katika mashindano mbalimbali ambayo imekuwa ikishiriki siku za hivi karibuni.

Uwezo wa viungo wa Yanga katika kuchezesha timu, kupiga pasi za mwisho, kufunga mabao na kuilinda safu ya ulinzi, umeifanya timu hiyo inayonolewa na kocha Nasreddine Nabi kuzitawala timu pinzani katikati mwa uwanja, jambo ambalo limeifanya kupata ushindi mara kwa mara na kucheza soka la kuvutia.

Kazi hiyo ya viungo wa Yanga imekuwa ikinakshiwa vyema na wachezaji wake wa safu ya ushambuliaji ambao wamekuwa wakizitumia vyema nafasi wanazopata kufunga mabao wakiongozwa na mkali wa kufumania nyavu, Fiston Mayele.


Udhaifu wa walinzi wa pembeni wa Al Hilal katika kukabiliana na mawinga wenye kasi, unaweza kuwa silaha kubwa kwa Yanga kupata ushindi leo, ikiwa nyota wake watakaopangwa katika nafasi hizo watatimiza vyema majukumu yao.

Hata hivyo, Yanga inapaswa kuwa makini zaidi katika safu yao ya ulinzi ambayo katika siku za hivi karibuni imekuwa ikifanya makosa ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakichangia wapinzani kupata mabao.

Katika mechi nane za mashindano tofauti msimu huu, tayari Yanga imesharuhusu mabao matano, tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita.

KIKOSI CHA USHINDI

Kikosi cha Yanga leo kinaweza kuundwa na Diarra Djigui, Djuma Shaban, Kibwana Shomary, Dickson Job, Yannick Bangala, Khalid Aucho, Bernard Morrison, Feisal Salum, Fiston Mayele, Stephane Aziz Ki na Tuisila Kisinda.


Uwepo wa nyota hao, hapana shaka utaifanya Yanga kwa kiasi kikubwa itumie mfumo wa 4-2-3-1 ambao imekuwa ikipendelea kuutumia ingawa inaweza kucheza pia mfumo wa 4-3-3.

HAKUNA MNYONGE

Matokeo ya mechi za nyumbani katika mashindano ya klabu Afrika yanaweza kuwapa wasiwasi Yanga, lakini yale ya Al Hilal ugenini, hapana shaka yatawafanya wawakilishi hao wa Tanzania kuingia wakiwa na hali ya kujiamini ambayo inaweza kuwa na faida kwao kumaliza mechi nyumbani.

Ukilinganisha matokeo ya mechi 10 za wenyeji walizocheza nyumbani na idadi kama hiyo ya michezo ambayo Al Hilal wamecheza ugenini, Yanga wanaonekana kufanya vizuri kuliko wapinzani wao.

Katika mechi 10 zilizopita za mashindano ya Klabu Afrika, Yanga imepata ushindi mara tatu, kutoka sare tatu na kupoteza mechi nne huku ikifunga mabao 15 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 12.


Hilal wao wamekuwa na wakati mgumu zaidi ugenini kwani katika michezo yao 10 za Afrika iliyocheza nje, imeshinda mara moja tu, ikitoka sare tatu na kupoteza sita huku ikifunga mabao manane na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 13.

MAKOCHA VITANI

Kocha wa Al Hilal, Florent Ibenge alisema kuwa wamekuja kusaka ushindi dhidi ya Yanga.

“Itakuwa ni mechi ngumu sio tu kwa sababu tunacheza na Yanga bali pia wana timu nzuri na wachezaji wazuri. Itakuwa ni mechi ngumu ya kusaka kwenda hatua ya makundi. Hata hivyo, tunajiamini kwamba tutapata matokeo mazuri,” alisema Ibenge.

Kocha wa Yanga, Nabi alisema wamejipanga vilivyo kuhakikisha wanapata ushindi mnono nyumbani.

“Ni mchezo ambao hautakuwa rahisi lakini inawezekana tukapata matokeo mazuri nyumbani ambayo yatatupa urahisi katika mechi ya ugenini. Wachezaji wangu wapo tayari kwa mechi na maandalizi yamekwenda vizuri.”


“Jambo la msingi ni mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuwapa hamasa wachezaji. Nina imani kubwa uwepo wao utawafanya wachezaji kujituma zaidi,” alisema Nabi.

AZAM, KIPANGA NAO

Kwenye Uwanja wa Martyrs da Benina, Benghazi, Libya, Azam FC itakuwa kibaruani kukabiliana na wenyeji wao Al Akhder ikisaka historia ya kuingia kwa mara ya kwanza katika hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika.

Wawakilishi wengine wa Tanzania, Kipanga FC wao watakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar kucheza na Club Africain ya Tunisia.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad