Kwanini Tunashobokea Wachezaji Waliowahi Cheza Ulaya?


KUNA ujinga mmoja unaendelea katika timu zetu kubwa nchini. Bahati mbaya unazidi kukua kila msimu. Ni hii tabia ya kushobokea wachezaji waliowahi kucheza Ulaya.

Tuliona pale Yanga ilianza na Saido Ntibazonkiza. Alionekana ana kitu mguuni, lakini umri umekwenda. Alishatumika kwenye nchi zaidi ya tano Ulaya na ubora wake ulikuwa unaelekea ukingoni. Yanga wakamsajili kwa pupa.

Nini kilitokea? Hadi Saido anaondoka Yanga hakuwahi kuwa mchezaji wa kutisha sana. Kwanini? Nyakati zake zilishapita. Ndio maana amekubali kucheza Geita Gold sasa, ambako pia hajafanya maajabu yoyote hadi sasa.

Yanga ikarudia tena kosa lile lile. Ikamsajili Gael Bigirimana. Mchezaji aliyewahi kucheza Newcastle United miaka mingi iliyopita. Huyu naye hata kwa kumtazama tu usoni, anaonekana jua linazama. Ana akili kubwa ya mpira, lakini hana kasi tena.

Umri wa Bigirimana umesogea na ndiyo sababu hata pale Yanga anapata wakati mgumu kucheza. Kwanini Yanga ilimsajili? Ni kwasababu aliwahi kucheza Ulaya.
Azam nao imefanya kosa hilo hilo. Imesajili kipa raia wa Comoro kisa tu amewahi kucheza Ufaransa. Nini kimebadilika? Anapigwa kama ngoma tu.

Hakuna ubora mkubwa alioonyesha kuwazidi kina Aishi Manula na Djigui Diara. Kwa kifupi ni ikipa mzuri wa kawaida tu. Ila amesajiliwa Azam kwa kigezo cha kuwahi kucheza Ufaransa. Kwanini tunapenda kuwashobokea wachezaji waliowahi kwenda Ulaya?

Kwa Simba tumeona juzi kati tu ilimleta Dejan Georgijevic kutoka Serbia, kwa vile amecheza Ulaya na pia ni mzungu, lakini alichokionyesha kwa muda aliokuwapo kikosini, kimemfanya mwenyewe ajishtukie na kususa ghafla kabla ya kuondoka kurudi alikotoka. African Lyon nayo ikiwa Ligi Kuu ilimsajili mchezaji kutoka Ulaya, aliwafanyia nini? Ifike mahali klabu zikajishtukia zisiingizwe mkenge.

Mwananchi

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad