Dodoma. Waliowahi kuwa makocha wa klabu ya Simba,Dyran Kerry na Goran Kopunovic ni sehemu ya zaidi ya makocha 20 walioomba kibarua cha kuifundisha Dodoma Jiji.
Mbali na makocha hao pia aliyewahi kuwa kocha wa Coastal Union Melis Medo naye anatwaja kuomba nafasi hiyo.
Kerry amewahi kuinoa Simba msimu wa 2015-2016 huku Kopunovic akiifundisha msimu wa 2014-2015.
Mapema leo uongozi wa Dodoma Jiji umetangaza kuachana na benchi zima la ufundi la klabu hiyo lilokuwa likiongozwa na Masoud Djuma na sababu zikitajwa ni matokeo mabovu ya klabu hiyo.
Mbali na Djuma wengine waliotupiwa virago ni kocha msaidizi Mohammed Muya na kocha wa makipa,Adam Meja ambaye inadaiwa amejiunga na Simba Queens.
Februari 24 mwaka huu uongozi wa klabu hiyo ulimtangaza Djuma kuiongoza timu hiyo akichukua nafasi ya Mbwana Makata ambaye aliyetupiwa virago.
Kocha huyo ameiongoza klabu hiyo katika michezo 21 ikifungwa 10, sare mitano na kushinda sita.
Mchezo wake wa kwanza ulikuwa dhidi ya Ruvu Shooting mtanange ulifanyika Mabatini mkoani Pwani na timu hizo zilitoka sare ya kufungana bao 1-1 huku wa mwisho ukiwa dhidi ya Simba ambao ulimazika kwa kukubali kichapo cha mabao 3-0.
Msimu huu ameiongoza klabu hiyo katika michezo sita na imeshinda mechi moja na kutoa sare miwili huku ikipoteza michezo mitatu na katika msimamo inashika nafasi ya 14.
Akizungumza na Mwanaspoti leo Oktoba 10 Jijini hapa,Kaimu Katibu Mkuu wa timu hiyo,Fredrick Mwakisambwe amesema zaidi ya makocha 20 wameomba nafasi hiyo wakiwemo makocha hao.
“Makocha walioomba ni wengi mno hata makocha wa zamani wa Simba wameomba.Yule aliyekuwa Coastal Union Medo nae ameomba pamoja na wazawa wengi, tunapitia CV zao na tutamtangaza kocha ambaye tutakuwa naye,”amesema Mwakisambwa.
Hata hivyo Mwanaspoti inajua tayari uongozi wa klabu hiyo unakaribia kumtangaza Medo kuchukua nafasi ya Djuma.