Ilikuwa ngumu sana kwa mashabiki wa Manchester United kuamini baada ya timu yao kupokea kichapo cha mabao 6-3 katika mechi ya Manchester Derby iliyopigwa kweye dimba la Etihad, jana Jumapili.
Mabao matatu matatu kutoka kwa Haaland na Foden yalitosha kabisa kuizamisha kimiani klabu ya Manchester United. Hat-trick hizo zimesababisha Erling Haaland na Phil Foden, kuweka rekodi yakuwa wachezaji wawili waliofunga hat-trick kwenye mechi moja tangu 2019.
Mastaa wengine waliowahi kuweka rekodi hiyo ni Jermaine Pennant, Robert Pires waliofanya hivyo kwenye mechi kati ya Arsenal dhidi ya Southampton Mei 2003 kabla ya Ayoze Perez na Jamie Vardy kufanya hivyo kwenye mechi ya Leicester na Southampton, Oktoba 2019.
Aidha, Haaland ameweka rekodi ya kufunga hat-trick ya tatu kwa muda mfupi zaidi katika Ligi Kuu ya Uingereza akifanya hivyo kwenye mechi nane akiivuka rekodi ya Michael Owen ambaye alifanya hivyo kwenye mechi 48.