Maswali Matano Mazito Yaibuka Katibu wa Masanja Kujinyonga Dar


Tukio la Katibu wa Kanisa la Feel Free Church la nchini Tanzania linaoongozwa na Mchungaji Emmanuel Mgaya almaarufu Masanja Mkandamizaji aitwaye Joas Steven la kujiua kwa kujinyonga, limeacha maswali matano mazito, IJUMAA linaripoti.

Hii ni baada ya Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kupitia kwa kamanda wake, ACP Jumanne Muliro kusema kuwa, uchunguzi wa awali umeonesha kwamba marehemu Joas na mke wa Masanja, Monica Mgaya hawakuwa na uhusiano wa kimapenzi kama iliyoenezwa mitandaoni.


Oktoba 4, 2022, Kamanda Muliro alieleza kuhusu uchunguzi wa jeshi hilo kufuatia tukio hilo ambalo limeibua hisia tofauti kwa wananchi.

“Ni kweli uchunguzi wa awali unaonesha mawasiliano yanaonesha huyo marehemu akiwa anaomba, akiwa anataka, anaomba mahusiano ya kimapenzi na mtu ambaye inadaiwa ni mke wa Masanja.

“Ni kweli pia kabla ya tukio mke wa Masanja akiwa na mama mwingine walikwenda nyumbani kwa marehemu kumueleza kwamba yule mke hataki meseji za namna ile na hataki mahusiano na yeye.

“Ni kweli pia yule mtu alifadhaika baada ya kuelezwa waziwazi kwamba yule ni mke wa mtu na hataki mahusiano naye, sasa mtitiriko wa visa hivyo unatoa nafasi ya kutokuwa na shaka na mazingira ya kifo kile.

“Bila shaka atakuwa amejinyonga kwa sababu mbalimbali za fikra zake au sababu nyingine yoyote, lakini hata hivyo, bado Jeshi la Polisi haliwezi likaishia kwenye ushahidi wa awali ambao umeonekana….mwisho huwa ni kufanya uchunguzi wa kitaalam,” alisema Kamanda Muliro.


MASWALI TATA

Wakati tukio la Joas kudaiwa kujiua linajiri, Masanja ambaye alikuwa karibu mno na jamaa huyo alikuwa nchini Marekani kikazi, lakini hakuonesha kuguswa na tukio hilo la mtumishi wa kanisani kwake hivyo kuibua maswali matano tata kama ifuatavyo;

SWALI LA KWANZA

Miongoni mwa maswali yaliyokuwa yakiulizwa kuanzia nyumbani kwa marehemu ulipowekwa msiba maeneo ya Mbezi-Beach jijini Dar hadi katika Makaburi ya Kondo-Kunduchi ulipolazwa mwili huo, ni juu ya kwa nini Masanja hakuonesha mshtuko, zaidi ya kulichukulia poa tukio hilo kubwa huku akimkingia kifua mkewe akisema hata kama atamfumania laivu hawezi kuachana naye?

“Nisikilizeni wanangu, tuweke kanisa na uchungaji pembeni, hata ikitokea nimemfumania mke wangu na mwanaume mwingine ile paaah face to face wanapiga game simuachi mke wangu maana upendo wangu kwake hauna kipimo. Namshika mke wangu mkono halafu nampimia huyo jamaa kama nammudu nammaliza…” Alisema Masanja na kuibua gumzo linguine jipya.

SWALI LA PILI

Swali lingine walilokuwa wakijiuliza wafiwa ni kwa nini Masanja hakutoa tamko lolote la kusikitishwa na kifo cha katibu wake chenye utata?


Walisema kuwa, Masanja alipaswa kuonesha thamani ya uhai wa binadamu mwenzake kwa kuwa kupoteza uhai ni jambo kubwa mno, lakini hakufanya hivyo!

SWALI LA TATU

Swali lingine ambalo wengi walitamani kupata majibu yake ni juu ya familia ya Joas na hasa mkewe wanasemaje?

Hata hivyo, jambo hilo limefanywa siri kwani hata mwandishi wa gazeti hili alipojaribu kumsogelea mjane wa marehemu alikatazwa na ndugu kiasi cha kutaka kuchafua hali ya hewa msibani.

SWALI LA NNE

Miongoni mwa maswali muhimu zaidi ni juu ya mke wa Masanja wa upande wake anasema kuhusu tuhuma na maelezo ya Polisi kwamba alikwenda nyumbani kwa Joas na je, walizungumza nini?

Maelezo ya Kamanda Muliro ni kwamba, mke wa Masanja na mwanamke mwingine walikwenda nyumbani kwa Joas kumtaka aache kumsumbua Monice kwani ni mke wa mtu!

SWALI LA TANO

Swali la mwisho wanalojiuliza wengi ni kwamba, je, Masanja ndani mwake anajisikiaje juu ya kufiwa na mtu wake wa karibu sana; yaani Katibu wa Kanisa lake tena kwa kujinyonga?

Wengi wanasema kuwa, sisi sote ni wanadamu na tunajua uzito wa kufiwa hivyo haiwezekani Masanja akawa yupo sawa kisaikolojia akijua amempoteza mtu wake wa karibu huku nyuma akitajwa mkewe.

Kwa wanaomfuatilia Masanja wanasema kuwa ameonesha kuumizwa zaidi na tuhuma dhidi ya mkewe, lakini jambo zuri ni kwamba ametangaza kumsamehe.

PONGEZI KWA MASANJA

Hata hivyo, katika ulimwengu ambao kila kukicha yanasikika matukio ya kutisha kutokana na wivu wa kimapenzi na usaliti, Masanja anapongezwa na wanaume wote wanaombwa kuwa kama yeye kwa namna alivyopokea tukio hilo bila na yeye kusababisha sintofahamu, badala yake ameonesha thamani, maana na heshima ya ndoa.

MKE WA MTU NI SUMU

Bila kuhusisha tukio hilo, lakini wanaume wamekuwa wakikumbushana kwamba mke wa mtu ni sumu hivyo inafaa aheshimike kama mtu anavyomuheshimu dada yake.

Wanaume wanakumbushana kutotamani na kumtaka wala kuwa na uhusiano na mke wa mtu kwani hata kama mtajidai kufanya siri, hakuna siri ya milele, kuna siku isiyojulikana mambo yatakuwa wazi.

Wanaume wanahojiana kuwa, hivi inakuwaje mtu unajua kabisa f’lani ni mke wa mtu kisha unamtaka kimapenzi na wengi unakuta ni wake wa rafiki zako?

Wanawake hao wana lao la kujiuliza kuwa, inakuwaje unajijua ni mke wa mtu, halafu unatakiwa kimapenzi na rafiki wa mumeo na unaendelea kucheka naye?

Wake wa watu wanajiuliza wenyewe kwamba, inawezekanaje kujenga mazoea na mtu mpaka iwe rahisi kwake kukutaka kimapenzi kwa sababu inajulikana kabisa kwamba mpaka mtu akutake, basi lazima tu kutakuwa mazoea ya ajabuajabu yamejengeka!

MARAFIKI WASALITI

Baadhi ya watu wanasema kuwa, siku zote katika maisha mtu anapaswa kuwa makini mno na wale anaowaita marafiki na watu wa karibu maana maadui wabaya ni miongoni mwao au ni wao wote huku wale unaoatazama kama maadui wakiwa ndiyo marafiki wa kweli.

Wanasema kuwa, tafsiri ya maisha ipo katika matendo ya mtu ayatendayo na siyo katika maneno na tabasamu la usoni.

Wanamalizia kusema kuwa, mambo mengi yenye kuleta vicheko, furaha, tabasamu na maneno matamu ni feki na yasiyo na maana.

Kwa wale Wakristo wanakumbushana kuwa, hata Yesu alisalitiwa na watu aliowapenda sana; Yuda na Petro ambao kila wakati walimuambia tuko pamoja nawe au tupo nyuma yako!

Stori; Richard Bukos, Dar

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad