MSHAMBULIAJI wa Yanga SC, Fiston Mayele, amechaguliwa na mashabiki kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Septemba, mwaka huu, baada ya kupigiwa kura nyingi.
Zoezi hilo lililoendeshwa na Mtandao wa Foot Africa, limemfanya Mayele kuibuka kidedea mbele ya Boulaye Dia raia wa Senegal, Dango Ouattara (Burkina Faso), Seko Fofana (Ivory Coast) na Karl Toko-Ekambi (Cameroon).
Mayele kwa mwezi Septemba alifanya kazi nzuri ya kuivusha Yanga kutoka hatua ya awali na kuingia ya kwanza katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kupiga hat trick mbili mfululizo dhidi ya Zalan FC wakiiondosha timu hiyo kwa jumla ya mabao 9-0 yeye akifunga sita.
Kabla ya mechi ya jana Jumamosi dhidi ya Al Hilal katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya kwanza, Mayele alikuwa amefunga jumla ya mabao 11 msimu huu kwenye mashindano yote. Ligi Kuu Bara (3), Ligi ya Mabingwa Afrika (6) na Ngao ya Jamii (2).
Kwa mwezi Septemba pekee, Mayele amefunga mabao saba, sita kati ya hayo ni dhidi ya Zalan FC, moja mbele ya Mtibwa Sugar katika Ligi Kuu Bara.
Straika huyo wa zamani wa AS Vita ya DR Congo, baada ya mashabiki kupiga kura 202,130, yeye ameshinda kwa asilimia 37.05, sawa na kura 74,894. Anafuatiwa na mshambuliaji wa Salernitana ya Italia, Boulaye Dia (kura 69,075 sawa na 34.17%).
Wengine aliowashinda ni mshambuliaji wa Lorient ya Ufaransa, Dango Ouattara aliyepata asilimia 15.68 sawa na kura 31,689, wakati Seko Fofana kutoka Klabu ya Lens ya Ufaransa, akipata asilimia 7.20, sawa na kura 14,552 na Karl Toko-Ekambi wa Olympique Lyonnais ya Ufaransa, amepata kura 11,920 sawa na 5.90%.
STORI NA OMARY MDOSE