Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imemhukumu mfanyabiashara, Hemed Ally kunyongwa hadi kufa, baada ya kupatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia Farihani Maluni.
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatatu Oktoba 17, 2022 na Hakimu Mkazi Mkuu, Joyce Minde, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutokewa hukumu.
Ally ametiwa hatiani kumuua kwa kukusudia Maluni na kisha mwili wake kuuzika mbele ya nyumba yake ambayo alikuwa anaishi eneo la Ilala Sharif Shamba, wilayani Ilala.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Minde amesema kuwa amemtia hatiani mshtakiwa kama alivyoshtakiwa.
"Upande wa mashtaka ulileta mashahidi 12 kuthibitisha shtaka linalokukabili na ushahidi wa kimazingira umekutia hatiani kwa kosa la kufanya mauaji ya kukusudia ya kumuua Farihan Malum, hivyo Mahakama inakuhukumu kunyongwa hadi kufa" amesema hakimu Minde.
Muda mfupi baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Farihani Maluni, akiwemo mke wake, Tatu Ali waliangua kilio mahakamani.
Tatu alilia mahakami hapo huku akisema mahakakam imetenda haki dhidi ya mauaji ya mume wake.
"Malipo ni hapa hapa duniani" alisikika Tatu akiwaambia ndugu zake na huku akilia.
Ally alimuua Maluni Juni 12, 2014.
Katika ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na Shahidi wa 11 wa upande wa mashtaka ulieleza kuwa Farahin aliuawa baada ya kukosa pumzi kulikotokana na kuzibwa mdomo kwa kutumia plasta.
Shahidi huyo, Innocent Mosha, ambaye ni daktari Bingwa wa Uchunguzi wa Magonjwa mbalimbali ya binadamu na vifo vya Mashaka kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alidai alipofanya uchunguzi wa mwili Maluni.
Alibaini kuwa plasta kubwa waliyoikuta kwenye fuvu la marehemu huyo ilitumika kumziba pumzi na kusababishia kukatisha uhai wake.
Dk Mosha alisema walipoufukua walikuta mabaki ya mwili ikiwemo fuvu la kichwa likiwa na plasta huku mikono yake ilifungwa na kamba kutokana na hali hiyo plasta hiyo ilitumika kumziba mdomo ili marehemu huyo asipate pumzi.
"Chanzo halisi ya kifo chake inawezekana alizibwa pumzi na plasta iliyokutwa kwenye fuvu la kichwa huku mikono yake iilikuwa imefungwa na kamba,"alidai Dk Mosha.