Dar es Salaam. Biashara ya mirungi Mkoa wa Kilimanjaro imekithiri, huku ikisafirishwa mchana waziwazi kwa pikipiki.
Baadhi ya wasafirishaji wakubwa wa mihadarati hiyo wameunda magenge ya kihalifu ambayo hujihami kwa mapanga na hutumia pikipiki kusafirisha mirungi kwa mwendo wa kasi kutoka mpaka wa Kenya hadi katikati ya mji wa Moshi.
Waandishi wa gazeti hili waliorejea jijini Dar es Salaam kutokea Moshi walipokwenda kuchunguza biashara hiyo kwa siri, walibaini magenge hayo yanapita na mafurushi ya mirungi hadi barabara kuu ya Moshi-Himo.
Hata hivyo, wananchi wanayatupia lawama makundi matatu kugeuza biashara hiyo kama mradi wa kujiingizia fedha na hao ni baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji, wenyeviti wa Serikali za mitaa na mgambo wa maeneo husika.
Mbali na kundi hilo, baadhi ya askari polisi wasio waaminifu wanaokuwa kwenye magari ya doria na wale wa kitengo cha Intelijensia, wanadaiwa kuonekana wakiwakamata wahalifu lakini ndani ya muda mfupi huachiwa.
Mirungi hiyo ambayo ni biashara inayowapa utajiri baadhi ya wafanyabiashara, imekuwa ikiingizwa nchini kutoka Kenya kupitia maeneo ya Kitobo, Madarasani, Tarakea na Mnoa na kusafirisha hadi Moshi, Arusha na Babati na mikoa mingine.
Njia wanazotumia baada ya shehena kuvushwa katika mpaka, ni Taveta hadi barabara ya Soko na Lorii, Kijiji cha Ngasini hadi Kahe Wilaya ya Moshi Vijijini na baadhi husafirishwa kwenda Moshi Mjini kupitia Pasua na Bomambuzi.
Pikipiki nyingine hupita Barabara Kuu ya Himo-Moshi hadi eneo la Miwaleni, pia huingia barabara ya vumbi na kutokea barabara iliyopo jirani na Kanisa la Efatha KDC kabla ya kutawanyika kwenda Moshi mjini na nyingine Kiborlon.
Shehena hizo huhifadhiwa katika nyumba za baadhi ya wasafirishaji wanaojulikana kwa majina na hufungwa katika vifurushi vidogo vidogo.
Pia, pikipiki hizo zimekuwa zikiingiza shehena hizo katika nyumba za wauza mirungi maeneo ya Mtaa wa Chini Kata ya Bondeni, Njoro, Kiusa, Korongoni, Bomambuzi, Pasua, KDC, Mbokomu, Kiborlon, Soweto, Kibosho na Karanga.
Wananchi wafichua mazito
Timu ya waandishi wetu kutoka Dar es Salaam iliyopiga kambi maeneo ya Himo, Chekereni na Moshi mjini, zilielezwa baadhi ya polisi, mgambo na viongozi wa vijiji na mitaa kama wangetimiza wajibu wao, biashara hiyo ingetokomezwa.
“Hizi pikipiki mmeziona zimepita hapa speed (kasi) ziko ngapi? Si ziko karibia 10 zinafukuzana. Ina maana viongozi wa vijiji hawaoni, polisi hawawaoni, mgambo hawawaoni? Huko zinakokwenda hawaonekani?” alihoji mwananchi mmoja.
“RC Kilimanjaro (Nurdin Babu), DC (mkuu wa wilaya) na viongozi wetu wa Jeshi la Polisi kuanzia RPC (kamanda) na watu wa TISS (Usalama wa Taifa) wanafanya kazi kubwa sana, lakini wanaangushwa na huku chini,” alieleza mwananchi huyo.
“Hebu tuwaulize ninyi, mmetoka Dar es Salaam mkaja Moshi na mnaona mirungi inasafirishwa mchana kweupeee. Sasa kazi ya kile kitengo cha Intelijensia cha Polisi kinafanya kazi gani kama hawawezi kujua mirungi inaingia wapi,” alihoji.
Mwenyekiti wa kijiji kimoja ambaye hakutaka kutajwa jina kwa sababu za kiusalama, alidai baadhi ya polisi wanawaangushwa kwa kuwa wanatoa taarifa lakini gari inapokwenda ‘wanamalizana’ nao wanaondoka bila kuwakamata.
“Sasa hivi wala sijihangaishi tena kuwapigia simu, maana unakuwa kama unawatengenezea watu ulaji tu, bora tuendelee na majukumu mengine. Tunaweza kumlaumu RPC sijui DC, lakini ukweli ni kuwa tatizo liko hapo,” alidai.
Mkazi wa Mtaa wa Kwakangala huko Kahe Wilaya ya Moshi, alidai kushamiri kwa biashara hiyo kunatokana na mifumo ya kamati za usalama za vijiji na mitaa kutotimiza wajibu wao, kwani biashara zinafanyika waziwazi mitaani.
RC, RPC watoa msimamo
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu alisema kwa mujibu wa sheria za nchi, mirungi ni moja ya dawa za kulevya.
Aliwataka wanaofanya biashara hiyo kuacha na kutafuta biashara nyingine halali ya kufanya. “Nataka kutoa rai kwa wananchi wa Kilimanjaro kuheshimu sheria za nchi kwa sababu zinakataza suala zima la mirungi, yeyote atakayekamatwa atachukuliwa hatua za kisheria,” alionya Babu.
“Naomba waache biashara hii haramu watafute biashara nyingine halali ya kufanya, Kilimanjaro zipo biashara nyingi, tuna ndizi, kahawa, parachichi, viazi na mboga, hizi zote ni biashara halali wanaweza kuzifanya bila kificho.
“Wanatambua biashara ya mirungi ni haramu na wanapita njia za panya, halafu matokeo yake ni kukamatwa, watapata shida tu, ninawashauri waache biashara hiyo, watafute biashara nyingine, kwa kuwa tumejipanga vizuri kukabiliana na hili,” alisema Babu.
Akizungumzia vijiji vinavyolima mirungi ukanda wa milimani Same, Babu alisema anatarajia kuanza ziara wilayani humo na tayari ameongea na mkuu wa wilaya ampeleke huko ili kuona hali ilivyo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Yahaya Mdogo alisema wamejipanga kudhibiti wasafirishaji wa dawa za kulevya, ikiwamo mirungi na bangi kwa kuendelea kufanya operesheni.
“Tunaendelea na operesheni katika maeneo mbalimbali ya mkoa huu ili kudhibiti wasafirishaji na wafanyabiashara wote wa mirungi na bangi na tutahakikisha tunawakamata wale wote wanaokiuka sheria,” alisema Kamanda Mdogo.
“Lakini tunaomba wananchi watuunge mkono katika operesheni hii kwa kutupa taarifa za wale wanaosafirisha dawa za kulevya, ikiwamo bangi na mirungi. Tutakuwa tayari kupokea taarifa kutoka kwa wananchi na zitakuwa ni siri.”
Alisema wasafirishaji wa mirungi wamekuwa wakitumia njia nyingi na zaidi usafiri wa bodaboda na baadhi yao magari na kwamba kupitia operesheni inayoendelea, watahakikisha wanawakamata wote na hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yao.
Akizungumza kwa njia ya simu kuhusu malalamiko ya wananchi kwa jeshi hilo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhan Kingai alisema, “nashukuru kwa taarifa hizo. Nitazifanyia kazi. Wacha niwasiliane na watu wangu walioko huko.”