Mo Dewji aamua kukomesha, mastaa wapagawa



BAADA ya kuwaondoa Primiero de Agosto kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika wachezaji wa Simba wameanza mazoezi kujiandaa na mechi ya Yanga Jumapili.

Lakini kabla hawajatia mguu uwanjani akaunti zao zitakuwa zimetuna. Bilionea, Mohammed Dewji ‘Mo’ ameamua kukomesha baada ya kuhakikisha akaunti wachezaji zinanona kabla ya kufikia jioni ya leo, kutokana na ushindi bao 1-0 dhidi ya Agosto uliowapeleka kwa kishindo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Awali juzi jioni kwenye Uwanja wa Mkapa, Kocha Juma Mgunda alitajirika baada ya kupewa minoti na wadau mbalimbali wa Simba wakiwemo wajumbe wa bodi ambao walifurahishwa na mzuka wake.

Siku moja kabla ya kucheza na Agosto, viongozi wa Simba zaidi ya kumi walitembelea kambi iliyokuwa kwenye moja ya hoteli ya kifahari katikati ya Jiji la Dar es Salaam na kuwaambia wachezaji kwamba bonasi ya Mo Dewji ni Sh100 milioni lakini wao wataongeza nyingine Sh100 milioni kwa kushirikiana na wadau na wadhamini wa Simba.

Miongoni mwa viongozi waliozungumza na wachezaji hao ni wajumbe wa bodi ya Wakurugenzi wakiongozwa na Mwenyekiti, Salim Abdallah ‘Try Again’ pamoja na Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez.

Shirikisho la Soka Afrika (CAF), litaipa Simba Dola za Kimarekani 550,000 si chini ya Sh1.3 Bilioni kwa pesa za Kitanzania kama fungu ya kufuzu hatua ya makundi.

Kwa mujibu wa mtandao wa CAF, umeweka kiasi cha pesa kwa timu zote 16, zilizotinga hatua ya makundi na mkwanja huo huwa unazidi kadri ambavyo timu inakwenda hatua ya mbele zaidi.


PHIRI ATAMBA

STRAIKA wa Simba, Moses Phiri amesema timu yake kutinga hatua ya makundi kuna maana kubwa kwao wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki wote kwani ni miongoni mwa mafanikio kwenye msimu huu na wataongeza nguvu zaidi.

“Hili la kufunga mabao matano kwenye mechi nne, nililiweka moyoni katika malengo yangu na limetimia ingawa naamini nilikuwa na nafasi ya kufunga mengine zaidi ya hayo,” alisema Phiri na kuongeza;

“Mabao matano ya kwenye hatua ya awali yamepita tayari, tunakwenda kucheza mechi nyingine ngumu sita hatua ya makundi na huko nahitaji kufanya vizuri zaidi ya hatua iliyopita na hilo naamini linawezekana,”

“Kufanya vizuri kwenye nafasi yangu hakuna jambo lingine zaidi ya kufunga mabao na kama nikishindwa kufanya hivyo natakiwa kuwa msahada kwa wengine kufunga mabao.

“Haikuwa kazi rahisi kufunga hayo mabao bila ya ushirikiano kutoka kwa wachezaji wengine na naamini hilo tutakwenda nalo hadi katika hatua ya makundi pamoja na mashindano ya ndani.”

MO AFUNGUKA

“Tunafuraha kwasababu tumetinga hatua ya makundi tukiwa na kocha mzawa sio rahisi lakini imewezekana ninaimani na kocha wetu na nipo tayari kwa ushirikiano wa hali na mali ili kuweza kufikia mafanikio,” alisema na kuongeza;

“Tunaelekea kwenye hatua ngumu zaidi tunaenda kukutana na wazoefu wa mashindano tunahitaji kujipanga na kutengeneza timu ya ushindani ni muhimu sana kukaa pamoja na kocha ili kuandaa mipango itakayotuvusha zaidi.”

“Tulianza kwa kuchechemea tulianza tukiwa wadogo kwenye mashindano sasa ni wakubwa tunaenda kukutana na wakubwa wenzetu tunatakiwa kujipanga zaidi ili kwenda kuonyesha ubora bado naamini Simba siku moja itatwaa ubingwa wa Afrika,” alisema na kuongeza;


“Nahitaji kuonana na Mgunda nina mazungumzo naye na nataka kumsikiliza ni nini anataka kwa hapa tulipofikia ili tufanyie kazi mapema kabla ya kuanza hatua nyingine ngumu,” alisema MO na kuongeza kuna dirisha la usajili mbele kama atahitaji kuongezewa nguvu wako tayari.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad