Mwanafunzi wa darasa la 4 afikishwa mahamani kwa kumuua shemeji yake
Mwanafunzi mwenye umri wa miaka 14 wa darasa la 4 anayeshtakiwa kwa kumdunga kisu shemeji yake miezi mitatu iliyopita atasalia katika gereza la watoto kwa wiki tano zaidi.
Jaji Eric Ogola aliagiza kuwa mwanafunzi huyoaendelee kuzuiliwa katika kituo hicho kinachosimamiwa na serikali kwa usalama wake wa kibinafsi hadi itakapothibitishwa kuwa ni salama kwake kuachiliwa kwa bondi.
Mahakama kuu mjini Eldoret imetoa uamuzi huo siku ya Jumatano.
"Ninaagiza kwamba mshtakiwa wa kwanza azuiliwe katika gereza la wanawake la Eldoret GK akisubiri matokeo ya ripoti ya afisa wa uangalizi wa shule huku mtoto mchanga akizuiliwa katika makao ya watoto huku tukitathmini hali ilivyo kuhusu usalama wake," alisema Ogola.
Mtoto huyo anashtakiwa pamoja na dadake Lucy Njeri, 27 na mfanyabiashara wa chang’aa kwa kumuua shemeji yake kwa kutumia kisu cha jikoni.
Walishtakiwa pamoja kuhusiana na madai ya mauaji ya Jacob Kioni mnamo Agosti 7 katika mtaa wa Manyatta huko Moisbridge kaunti ya Uasin Gishu.
Mtoto huyo anasemekana kumdunga shemeji yake kwa kutumia kisu cha jikoni alipokuwa akijaribu kuwatenganisha marehemu na washtakiwa wenzake walipokuwa wakipigania kikombe cha chang'aa.
Juhudi za kuwaokoa marehemu hazikufua dafu kwani alifariki baada ya kuwasili katika hospitali ya Kaunti Ndogo ya Moisbridge.
Hakimu aliagiza kwamba suala hilo litajwe Novemba 17 wakati ripoti ya afisa wa uangalizi wa sheria itakapotolewa mahakamani.
Jaji Ogola aliagiza washukiwa hao wapelekwe katika Hospitali ya Rufaa ya Moi mjini Eldoret kufanyiwa uchunguzi wa kiakili na pia kutathminiwa umri kabla ya kuwasilisha ombi.
"Kwa hili ninaagiza washukiwa wapelekwe MTRH kwa uchunguzi wa kiakili na mtoto pia anapaswa kutathminiwa umri kabla ya kujibu," akaagiza Jaji Ogola. Wakati uo huo, mahakama iliamuru mtoto huyo azuiliwe katika kizuizi cha watoto Eldoret huku mshtakiwa mwingine akizuiliwa katika gereza la wanawake la Eldoret.