Nirahisi mno kusikia habari za watu kupoteza mali, pesa, marafiki au hata wapenzi wao, lakini ni jambo la kustaajabisha sana kusikia kwamba mtu anaweza akapoteza kiungo cha mwili wake, tena cha ndani katika njia tatanishi.
Ndio hali iliyompata mwanaume mmoja kutoka taifa jirani la Uganda ambaye sasa analilia haki baada ya kugundua kwamba figo yake moja haipo tena alipolazwa hospitalini. Kulingana na jarida la Daily Monitor, Muhammad Kabanda, mkazi wa kijiji cha Gangu nje kidogo ya jiji la Kampala anasemekana alitembelea kituo cha hospitali cha Old Kampala mnamo Septemba 24, 2022 kufuatia ajali ya bodaboda kwenye barabara ya Lukuli.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 25 alikuwa na majeraha mabaya kichwani ambapo alitakikana kulipia mamilioni ya fedha kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji. “Lakini operesheni hiyo ilipofanyika nilishtuka baada ya kugundua kuwa nilichanjwa chale mpya upande wa kushoto wa tumbo jambo ambalo halikuweza kuelezewa na madaktari wa kituo hicho wala uongozi wao. Nilikwenda na kufanya scans na ripoti za wataalamu wa radiolojia zilithibitisha kwamba figo yangu ya kushoto ilikuwa imetolewa. Uchunguzi wa CT Scan pia ulifanywa katika Hospitali ya Mengo na kuchapisha matokeo yaleyale,” Daily Monitor walimnukuu mwathiriwa Bw Kabanda.
Polisi katika jiji la Kampala walisema tayari wametoa wito kwa mamlaka ya hospitali hiyo kuandikisha ripoti kuhusu malalamishi hayo kabla ya uchunguzi kuanza rasmi.