Dar es Salaam. Kwa siku tatu mfululizo maofisa elimu wa Wilaya Chalinze na Mkoa wa Pwani, wapo kwenye mahojiano na uongozi wa Shule ya Chalinze Modern Islamic Pre and Primary ya mkoani humo na wazazi wa mwanafunzi, Iptisum Slim aliyelalamika kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi kwa namba isiyo yake.
Sakata la Iptisum lilianza kusikika Oktoba 14, baada ya kusambaa kwa video inayomuonyesha akiomba msaada kwa Serikali, akihofia kupoteza haki yake ya kusoma, baada ya kupewa namba ya mtu mwingine na kuifanyia mtihani huo.
“Baada ya mtihani kuisha baadhi ya wanafunzi tuliitwa na mwalimu mkuu tukaambiwa yale yaliyotokea yasisikike sehemu nyingine yaishie palepale.
“Naomba msaada nisaidiwe kisheria kupata haki, majibu yangu yarudi kwenye namba yangu kwa sababu mtoto niliyemfanyia mtihani anashika nafasi ya chini na mimi nashika nafasi za juu, hata mtihani wa moko wilaya nilishika nafasi ya kwanza,” alieleza mtoto huyo.
Mama wa mwanafunzi huyo, Atwiya Mohamed akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, alisema wanaendelea na mahojiano na anaamini haki ya mwanaye itapatikana.
“Kwanza niwashukuru waandishi wa habari mmenisaidia kwa kiasi kikubwa, nimehakikishiwa haki ya mwanangu itapatikana. Tangu Jumamosi tumeanza kuhojiwa na leo (jana) naenda huko,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shule ya Chalinze Modern Islamic, Omary Swedi alisema tayari jambo hilo linafanyiwa uchunguzi na vyombo vya sheria, hivyo hawezi kulizungumzia.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Francis Michael alisema bado uchunguzi wa sula hilo unaendelea kupitia Baraza la Mitihani la Taifa (Necta).
Hali ilivyokuwa
Iptisum ambaye alifanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba Oktoba 5 na 6, alisema namba yake halali ilikuwa 40, lakini alipewa namba 39 na alipohoji aliambiwa asiwe na wasiwasi afanye mtihani, kwani jambo hilo ni dogo la lingepatiwa ufumbuzi na Necta.
Kauli hiyo ilimshangaza na kuona haki yake inapotea, kwani siku ya mwisho ya mtihani mwanafunzi huyo alirejeshwa kwenye namba yake halali, jambo lililomfanya kuangua kilio.
Alipofikisha malalamiko yake kwa uongozi alidai wanafunzi wote waliokuwa kwenye darasa hilo walionywa juu ya kutoboa siri ya kile kilichotokea.
Mama mzazi wa mwanafunzi huyo alisema Oktoba 8 alipofika shuleni kwa ajili ya mahafali alimkuta Iptisum kwenye huzuni na aliwataka wazazi wake waanze safari ya kurudi Kimara, Dar es Salaam nyumbani wanakoishi.
Wakiwa safarini, mama huyo alishangazwa na kilio kisichoisha cha mtoto huyo na kila alipomuuliza hakutaka kuzungumza mpaka siku chache zilipopita alipoamua kusimulia mkasa huo.
Licha ya mama huyo kudai kutafuta msaada kwa shule husika, alikatiwa simu na baada ya siku chache kupita alifuatwa na uongozi wa shule hiyo kuombwa msamaha akitakiwa tukio hilo liishe na atapewa fidia.