Moshi. Katika hali ya kustaajabisha mzee wa miaka 70, mkazi wa kijiji cha Uru Shimbwe, mkoani Kilimanjaro, Uruban Paul amevamiwa nyumbani kwake usiku na watu wasiojulikana na kisha kumkata sehemu zake za siri.
Akielezea tukio hilo lililotokea Oktoba 16, mzee huyo alisema kuwa alikuwa akitoka kwenda kujisaidia na kukutana na watu hao ambao baada ya kumfanyia kitendo hicho walikuwa wakikinga damu yake.
Hata hivyo, alipotafutwa kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Asteriko Maiga alisema tukio hilo halifahamu lakini atalifuatilia kujua ukweli wake.
“Hili tukio silifahamu, naomba nilifuatilie maana nilikuwa sipo kwenye hii ofisi, ninamshikia RPC ambaye yupo nje ya mkoa kikazi,” alisema Maiga.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Alexanda Temba alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. “Nilionana na huyo mzee pamoja na ndugu zake, kwa kweli ni tukio la ajabu,” alisema.
Akizungumza na Mwananchi jana, mzee huyo alisema: “Kabla tukio halijatokea, nilikuwa na ndugu zangu muda wa jioni, niliagana nao nikarudi nyumbani kwangu ninapoishi, wakati natoka ndani kwenda kujisaidia usiku ghafla nikavamiwa na watu walionikaba na kunifunga na kitu usoni nisione, wakaniingiza ndani wakanivua nguo na wakati huo nilikuwa siwezi kupiga ukunga kuomba msaada kwa majirani zangu, walinilaza chini wakaanza kunikata sehemu ya uume wangu, nilipata maumivu makali sana.
“Nilijitahidi kujiburuza kutoka nje kuomba msaada, bahati nzuri kuna jirani yangu alikuwa akipita akaniona nikiwa chini nikitapatapa kwa maumivu, aliniangalia nilivyofanyiwa ukatili ule akaogopa kwa sababu damu zilikuwa zimetapakaa. Alimtafuta jirani mwingine wakaja kunisaidia, usiku uleule walimpata ndugu yangu wakanichukua na kunipeleka hospitali,” alisimulia Paul.
Hata hivyo, alisema hivi sasa anaendelea vizuri baada ya kupata matibabu japokuwa bado anasikia maumivu ya nyuzi alizoshonwa.
“Ninaiomba Serikali inisaidie ili waliofanya tukio hilo wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema.
Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa wananchi wa kijiji hicho, Francis Kinyaia alisema kijiji hicho kimekuwa na matukio mengi ya ukatili na hilo si la kwanza, huku akilihusisha na imani za kishirikina.
“Kwenye hiki kijiji hatuko salama, hatujui nani atafuata kwa sababu hatujajua nia yao ni nini, huyu mzee hapa kijijini tunamfahamu sana sio mgomvi, wala mhuni useme labda alitembea na mwanamke wa mtu.
“Huyu mzee hana mtoto na hajawahi kuoa, ingekuwa mzururaji tungesema labda ni mtu ana visa naye, tuna imani kwamba hili tukio ni la kishirikina kwa sababu alidai walivyomkata walikuwa wanakinga damu yake,” alisema.
Alisema kipindi cha mwisho wa mwaka kijijini hapo huwa na matukio mengi ya kikatili, hivyo ataitisha mkutano wa kijiji kulijadili hilo.