YANGA sasa ina mtihani mmoja tu kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuitoa Al Hilal ya Sudan. Kuna mawinga wao watatu wanapigishwa tizi la hakuna kulala huko kambini Kigamboni Bernard Morrison aliyesimamishwa kucheza mechi tatu za ligi,Tuisila Kisinda na Jesus Moloko ambao wote wamekabidhiwa kwa Mtunisia Helmy Gueldich.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi alisema kuna ubora anautaka kutoka kwa Morrison, Moloko na Kisinda lakini ni lazima washibe pumzi na stamina.
Nabi alisema mawinga hao wanapata ratiba maalum ya mazoezi nje ya ile ambayo wanaipata na wenzao kambini ikiwa ni hatua ya kuwaweka tayari kwa ajili ya Al Hilal wanatua kesho Dar es Salaam.
Kocha huyo alisema kuwa ingawa imekuwa ratiba ngumu inayowachukiza wachezaji hao lakini faida yake itawabeba dhidi ya Wasudan hao ambao watakutana nao Jumamosi Oktoba 8, Uwanja wa Mkapa.
“Tunahitaji mawinga watakaokuwa tayari muda wote kushambulia kwa nguvu na kusaidia kupokonya mipira pale tunapopoteza mipira.
“Tunamjumuisha pia Tuisila (Kisinda) pamoja na Moloko ili tuangalie nani atatusaidia zaidi katika mechi hii inayokuja ukiachana na mechi za kirafiki tulizopata,”alisema Kocha huyo anayefahamu nje ndani soka la Afrika.
“Sio kitu rahisi kwao kukubalika katika kutekeleza ratiba kama hii lakini nimezungumza nao wote hasa Morrison nimemwambia kama atafanya vizuri ataona jinsi atakavyoisaidia sana timu na kuwafurahisha mashabiki wa hii timu, namuamini sana Morrison.
“Nimemwambia nataka kumuona yule Morrison wa ile mechi dhidi ya Kaizer Chiefs lakini ili tumuone Morrison yule ni lazima awe tayari kupambana kwa nguvu kwa kuwa sasa hivi hawezi kucheza mechi za ligi kuwa sawa na wenzake,” alisema Nabi ambaye moja ya mtihani wake kibaruani msimu huu ni kuitoa Al Hilal ya Florent Ibenge na kufuzu makundi