WAKATI viongozi na mashabiki wa Yanga wakiumiza vichwa kuona namna ya kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi ameutaka uongozi kuhakikisha wanamtuma mtu mapema kwenda nchini Tunisia ili kuweka mambo sawa ikiwemo kumletea mbinu za kuwaua Club Africain.
Novemba 2, mwaka huu, Yanga itakutana na Club Africain ya Tunisia kwenye mchezo wa mtoano wa Kombe la Shirikisho Afrika, utakaopigwa Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, kisha marudiano ni Novemba 9 nchini Tunisia. Mshindi wa jumla atafuzu makundi ya michuano hiyo.
Chanzo chetu kutoka Yanga, kimeliambia Spoti Xtra kuwa: “Nabi amedhamiria kushinda mchezo wetu dhidi ya Club Africain, maana tayari ameutaka uongozi kuhakikisha wanamtafuta mtu anayeweza kwenda Tunisia mapema kuwashuhudia wapinzani wetu ili kuleta mbinu ambazo zitasaidia kuwamaliza.
“Tayari maagizo yake yamefanyiwa kazi na kwamba wamemtaka kukaa naye chini baada ya mchezo dhidi ya KMC, kisha wapange kama ni kocha wa viungo au msaidizi atakayeenda huko Tunisia kuifanya kazi hiyo,” kilisema chanzo hicho.
Kwa upande wa Nabi, amesema: “Tunaelewa kuwa ratiba yetu imebana, tunafanya kila jitihada ili kuendana na hali halisi tunayokabiliana nayo kwa sasa. “Lengo kubwa ni kuhakikisha tunashinda pamoja na kwamba tuna mechi ngumu mbele yetu, huo ndio ukweli tunaopaswa kukabiliana nao ili tufanikiwe.
Stori na MUSA Mateja