OKTOBA 22 kwenye ukurasa wa pili wa Mwanaspoti kuna kitu tulikudokeza lakini tukakusisitiza usimwambie mtu. Unakumbuka?
Sasa ni rasmi unaweza kumwambia tu. Mwanaspoti limejiridhisha kwamba Yanga imeachana na ‘Profesa’ Nabi Nasreddine Mohammed pamoja na msaidizi wake, Cedrick Kaze.
Na kocha mpya ni raia wa Brazil, Roberto Oliveira anayeinoa Vipers ya Uganda.
Kocha huyo ndiye aliyeifunga Yanga kwenye kilele cha Siku ya Mwananchi jijini Dar es Salaam lakini juzijuzi aliiondosha TP Mazembe nyumbani kwao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika tena akiipigia mpira mwingi kwa kutumia kikosi chenye thamani ambayo haifikii ile ya Yanga.
Kwa mujibu wa mwandishi wa Mwanaspoti jijini Kampala, Oliveira kwenye wiki za hivikaribuni alikuwa akiwindwa na viongozi wa Simba lakini baadaye wakaamua kumkaushia baada ya kuridhishwa na mzuka wa kocha mzawa Juma Mgunda.
Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti limezipata ni kwamba Yanga imeamua kuachana na Nabi na Kaze kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa timu hiyo kwa maana ya uwajibikaji wa wachezaji lakini kubwa jingine ikiwa ni kushindwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mbali na hayo, lakini kingine kinachowatemesha mzigo ni maelewano yasiyoridhisha baina yao ambayo yamekuwa yakiathiri afya ya timu hiyo iliyowekeza fedha nyingi kwenye mastaa wengi wa kigeni wanaozungumza Kifaransa.
Inadaiwa kwa muda sasa imekuwa ni jambo la kawaida wawili hao kujibizana pale mmoja wao anapokuwa haridhishwi na jambo, lakini za ndani kabisa zinasema kuna kazi ambazo Nabi amekuwa akimpa Kaze na yeye kuzikataa kwa madai haziendani na hadhi ya kocha msaidizi ikiwemo ile ya kutafsiri mbele ya waandishi wa habari wakati anajua Kingereza.
Habari zinasema maamuzi hayo ya Yanga yamefanyika huku kukiwa na mjadala baina ya wanachama waandamizi wa Yanga ambapo baadhi wanataka Nabi aendelee kuwepo kwa kutafutiwa msaidizi mwingine wakihofia ataibukia Simba huku wakidai rekodi zake hazionyeshi kuwa ni mbovu.
Lakini wengine wanataka Kaze abaki aletetwe kocha mwingine na kubadilishiwa majukumu. Habari zaidi zinasema Kaze imeamuliwa kuwa atapewa jukumu la kusimamia programu za vijana jukumu alilokuwa nalo Mwinyi Zahera.
Habari zinasema hata Nabi angeifunga Simba juzi Jumapili bado isingekuwa salama yake kwani uamuzi ulishafanyika hata kabla hajatua nchini akitokea Sudan kucheza na Al Hilal. Mechi ya juzi iliisha kwa sare ya bao 1-1.
Tayari kocha mpya inaelezwa Yanga ilitaka atue nchini haraka juzi awepo kwenye dabi lakini aliwagomea akiwataka wao kufanya maamuzi kwa kuwa tayari anaijua Yanga na hata ubora wa timu pinzani.
Kwenye Uwanja wa Mkapa juzi, jukwaani alionekana Kocha wa Timu ya Taifa ya Uganda, Sredejovic Milutin ‘Micho’ habari zikazushwa kuwa ndiye anayepewa Yanga lakini wengine wakamhusisha na Simba kuwa bosi wa Mgunda.
“Mi nimekuja kumuangalia Khalid Aucho, ingawa pia nimefurahishwa na kiwango cha Stephen Aziz KI ndiye mchezaji bora wa mechi hii,” alisema Micho ambaye ni mzoefu wa soka la Afrika akifundisha Tanzania, Sudan, Ethiopia, Uganda, Rwanda na Afrika Kusini.
REKODI ZA NABI MBABE WA SIMBA
Kocha Nabi amekuwa mbabe kwa Simba ambapo katika mechi nane za mashindano tofauti walizokutana, ameshinda mara nne, kutoka sare tatu na kupoteza mechi moja.
Rekodi hiyo imemfanya Nabi awe kocha wa Yanga aliyeifunga Simba mara nyingi zaidi ndani ya muda mfupi kuliko mwingine tangu ilipoanzishwa mwaka 1935. Hivyo kocha huyo anaondoka huku akiwa ametengeneza rekodi yake ya kibabe kwenye mechi za dabi.
MECHI 43 BILA KUFUNGWA
Kocha huyo amedhihirisha umwamba mwingine kwa kuiongoza Yanga kuvunja rekodi ya Azam FC ya kucheza mechi 38 mfululizo za Ligi Kuu bila kupoteza.
Nabi yeye ameiongoza Yanga kwenye mechi 43 za Ligi Kuu tu na hajapoteza mchezo wowote ule.
Azam ambayo wakati inaweka rekodi ya kutopoteza mechi 38 ilikuwa chini ya makocha wawili tofauti.
Wakati Azam inacheza mechi 38 bila kupoteza, ilianza kunolewa na Kocha Mwingereza, Stewart Hall ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Mcameroon, Joseph Omog.
Hall aliiongoza Azam kucheza michezo 21 bila kupoteza kabla ya kutimuliwa Novemba, 2013 ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Omog ambaye chini yake, Azam ilicheza mechi 13 za Ligi Kuu bila kupoteza hadi Oktoba 25, 2014 walipofungwa bao 1-0 nyumbani na JKT Ruvu ambayo sasa ni JKT Tanzania. Katika mechi 43 ambazo Nabi ameiongoza Yanga ameshinda 31 na sare 12.
UGENINI SAFI
Upande wa mechi za ugenini bado Nabi anashikilia rekodi ya kibabe kwani amecheza mechi 23 na hajapoteza hadi anaondoka.
Awali Simba na Azam zilikuwa zikishikilia rekodi ya kucheza michezo mingi mfululizo Ligi Kuu ugenini bila kupoteza ambapo kila moja ilicheza mechi 17 nyakati tofauti.
MZEE WA KUPINDUA MEZA
Kitendo cha kutoka nyuma dhidi ya Polisi Tanzania (Msimu huu) na kushinda (come back) kumeifanya Yanga itimize mechi ya nane ya mashindano chini ya kocha Nabi kufanya hivyo.
Kabla ya mchezo huo, Yanga ilitoka nyuma baada ya kutanguliwa na kuibuka na ushindi dhidi ya Simba (Ngao), Geita Gold, Tanzania Prisons, Biashara United, Azam na Coastal Union, Ruvu Shooting.
MAKOMBE
Yanga ikiwa chini ya Nabi imechukua Kombe la Ligi Kuu mara moja tu huku ikichukua Ngao ya Jamii mara mbili na zote akiifunga Simba.
Kwa maana hiyo Nabi anaondoka huku akiwa ana taji la Ligi Kuu baada ya Simba kuchukua mara nne mfululizo na yeye akavunja huo mfupa.
Mshambuliaji wa zamani Yanga, Hery Morris alisema kama Nabi anaondoka sio kitu kibaya lakini uongozi inabidi wamlete kocha ambaye atakuwa na uwezo zaidi yake.
Wakati huo huo mchezaji wa zamani Simba na Yanga, Zamoyoni Mogela alisema uongozi wa Yanga una malengo yao kwahiyo inawezekana wapo sahihi kwa maamuzi waliyochukua.
“Sio mbaya na Nabi amejitahidi kwa upande wake kwa alichokifanya Yanga, nadhani malengo ya Yanga nilisikia ni kwenda makundi katika Ligi ya Mabingwa kwahiyo inawezekana wanaachana naye kwa sababu hiyo.”