Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amezungumzia suala la mikutano ya vyama siasa, akisema inaleta ushindani, afya na demokrasia kwa Taifa.
Mwaka 2016 Serikali ilipiga marufuku mikutano ya hadhara, baada ya kumalizika kwa uchaguzi ukuu wa mwaka 2015 ikieleza kuwa siasa hufanywa wakati wa uchaguzi.
Nape ambaye pia ni mbunge wa Mtamba mkoani Lindi ameyasema hayo leo Jumatatu, Oktoba 17, 2022 katika mahojiano maalumu katika kipindi cha ‘Joto Kali la Asubuhi’ kinachorushwa na E-TV, Dar es Salaam, akieleza pia utendaji wake alipokuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM.
Ameeleza hayo baada ya kuulizwa kama anatamani kuona mikutano ya hadhara ikiendelea kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, ambapo viongozi wa vyama vya upinzani na CCM walikuwa wakikabiliana kwa hoja katika majukwaa.
Katika majibu yake, Nape amesema anaamini pia mikutano ya vya vyama vya siasa ingeimarisha CCM zaidi kuliko hali ilivyo na kwamba mtu akiwa ananaogoza bila kuwa na anayemsema ni rahisi kujisahau.
“Watu wakiwa wanawasema sema, mara hili jambo sio sawa mnarudi ndani mnakaa. Yapo mambo CCM tumeyabadilisha kwa kuwasikiliza jamaa wanavyopiga kelele, wanapiga kelele mnawabishia, lakini mkirudi ndani mnasema hili linafikirisha lifanyiwe kazi,” amesema Nape.
Mbali na hilo, Nape amesema “Mimi ni kati ya wale tunaoamini tangu mwanzo kabisa ni vema tufungue watu wafanye siasa. Kama unataka kujipima, usijipime wakati mwanzako kafungwa mikono, nendeni mkashindane na kujenga hoja.
“Isipokuwa jambo la msingi kuliko lote hapa ni kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ameshaunda kikosi kazi kitakachotoa mwelekeo wa namna bora kufanya. Kwa sababu hamuwezi kufanya siasa, kwamba uchaguzi umekwisha basi mikutano, operesheni na watu kuandamana jambo lililoleta shida kidogo.
“Namshukuru Rais Samia, mwenzake (hayati John Magufuli) alifunga kabisa, lakini yeye amefungua kwa kutengeneza utaratibu kwa watu kukaa, kuzungumza na kukubaliana. Mimi ni muumini na ukiwa na mwanasiasa lazima ukubali kuwa ngozi ngumu na waruhusu watu wakuseme,” amesema Nape.
Kutishiwa bastola
Akizungumzia tukio la kutishiwa bastola lilitokea Machi 23, 2017 wakati akitaka kuzungumza na waandishi wa habari nje ya Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam, Nape amesema kila jambo linatokea kwa kupangwa, lakini amewasemehe wote waliomtishia, waliowatuma hadi waliopanga huku akibainisha kuwa amejifunza kupitia tukio hilo.
Kufuatia tukio hilo, Nape aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo alienguliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Dk Harrison Mwakyembe.
“Hakuna hata mmoja niliyewaza kumlipiza kisasi, sina sababu kwa sababu nilisamehe toka wakati ule. Mfano yule aliyetoa silaha hadharani sidhani kama alitumwa kufanya vile bali alitumwa kumzuia Nape.”
Bei ya vifurushi
Kuhusu bei ya vifurushi inayolalamikiwa na wananchi, Nape amesema kuwa mwaka huu inafanyika tathimini kuhusu mwenendo wa bei za vifurushi kuanzia mwezi hadi Machi mwakani, akisema kuna kila dalili bei za vifurushi kupungua kutokana na kusambaa mkongo wa Taifa na kupunguza baadhi ya kodi.
Akizungumzia ujumbe wa kitapeli katika simu za kiganjani, Nape amesema hivi karibuni Serikali itasaini kanuni ya usajili wa laini za simu ili kudhibiti na kurebisha changamoto hiyo. Amesema lazima kusafisha mtandao ili kupata laini za simu kulingana hali i