MABOSI wa Simba wamepanga kuongeza majembe mawili mapya dirisha dogo, huku beki wa kati, Mohamed Ouattara akihesabiwa siku kabla kuonyeshwa mlango wa kutokea.
Za Ndaani Kabisa, zinasema Simba inataka kuleta straika mkali wa kutupia zaidi ya Moses Phiri ambaye kiasili ni kiungo mshambuliaji ili kuiongezea nguvu timu, huku nafasi nyingine ikiwa ni beki wa pembeni na nafasi hizo zitapatikana kwa kupunguza nyota wa kigeni akiwamo Ouattara baada ya awali Dejan Georgijevic kujiondoa mwenyewe mwishoni mwa mwezi uliopita.
Za Ndaani Kabisa zinasema mabosi wa Simba wamepanga kufanya maamuzi magumu dhidi ya beki huyo aliyesajiliwa kutoka Al Hilal ya Sudan aliyesajiliwa kwa shinikizo la Kocha Zoran Maki aliyeitumikia timu hiyo kwa siku 67 kabla ya kutimka kwenda Al Ittihad ya Misri.
Inalezwa Ouattara anaweza kutemwa kwenye dirisha dogo ili Simba kupata nafasi ya kusajili mchezaji wa kigeni kama malengo yao na sababu za kumtema ni kushindwa kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza kama ilivyokuwa wakati kocha Maki.
Kutokana na kushindwa kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza mbele ya Joash Onyango, Henock Inonga na muda mwingine Kennedy Juma, mabosi wanataka kutumia dirisha dogo litakalofungwa Januari kumpiga chini.
Awali beki huyo alimchomoa Onyango kikosini chini ya Zoran, kiasi cha Mkenya huyo kukimbilia TFF kutaka avunjiwe mkataba ili akakipige Singida Big Stars, lakini kuondoka kwa kocha huyo, kulileta afueni kwa beki huyo kisha Outtara sasa kusugua benchi tangu alipopata majeraha.