Moshi. Ndege ya Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) iliyokuwa imebeba kamati ya usalama ya Mkoa wa Kilimanjaro imeshindwa kufika na kufanya tathimini ya athari ya moto katika eneo la Karanga Camp, mlima Kilimanjaro kutokana na hali ya hewa na moshi mzito.
Akizungumza leo Jumamosi Oktoba 22, 2022 baada ya kutoka katika eneo hilo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema walipofika eneo la mlima Kilimanjaro ndege ilizunguka zaidi ya mara mbili ili kujaribu kufika eneo lenye moto lakini ilishindwa kutokana na hali ya hewa na moshi mkubwa.
"Tumezunguka karibu mara mbili, mara tatu lakini hatukufika kabisa lile eneo la moto kwa sababu mawingu ni makubwa na moshi ni mkubwa, tukaamua turudi kwanza na hali itakapokuwa shwari ndipo tutarudi kuangalia.
Mwananchi
Moto huo ulianza kuwaka jana Oktoba 21 usiku katika eneo la Karanga kuelekea Baranko umbali wa mita 3,963 kutoka usawa wa bahari.
Mpaka sasa askari zaidi ya watu 320, kutoka Tanapa, Jeshi la Zimamoto, Polisi, Mgambo, Watumishi pamoja na wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori (Mweka) na wafanyakazi wa kampuni ya utalii wapo katika eneo hilo kudhibiti moto huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa awali na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjro, Nurdin Babu mpaka sasa hakuna madhara yoyote ya kibindamu yaliyojitokeza.