KUWA bora kunawezekana kwa kushindana na aliye bora. Wikiendi iliyopita klabu nne za Tanzania zilikuwa viwanjani kujaribu kudhihirisha ubora wao barani Afrika. Ni Simba pekee iliyoweza kupata ushindi wa 1-3 dhidi ya CD Primier de Agosto ya Angola. Yanga ilitoka sare ya 1-1 na Al Hilal ya Sudan, Kipanga FC ya Zanzibar ikatoka suluhu na Club Africain ya Tunisia na Azam ikafungwa 3-0 na Al Akhdar ya Libya.
Kwa mara ya nyingine, unaonekana msisimko mkubwa kwa mashabiki hapa nchini kuanza kufuatilia kwa karibu ushiriki wa klabu zao barani Afrika. Zinaweza kuwepo sababu nyingi zinazowafanya Watanzania kufungua macho yao kimataifa. Huko nyuma timu za Tanzania zilikuwa na ushindani mkali kwenye mashindano ya Kagame ya klabu za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa clubs championship). Kwa sasa mashindano haya hayatabiriki, ni kama hayapo au yamekosa fedha za uendeshaji na zile za zawadi.
Pia, timu za Tanzania hazioni wapinzani ndani ya Afrika Mashariki na kati bali barani Afrika.
Kumekuwa na ongezeko la urushaji wa mechi hizi mubashara kwenye runinga kupitia Azam. Zamani ilikuwa vigumu kufuatilia mubashara hasa timu ziliposafiri kwenda nje. Kwanza televisheni hazikuwepo hapa nchini lakini hata baada ya televisheni kuwepo hazikuwa na miundombinu ya kifedha na kiufundi kutangaza michezo hiyo.
Mafanikio ambayo klabu ya Simba imeyapata hivi karibuni kwa kufika robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika. Kwa sababu ya Simba kufika mbali katika mashindano ya Afrika, mechi nyingi zilizochezwa hapa na nje zimeifanya michuano ya klabu kuingia kwenye ratiba na utamaduni wa mpira wa hapa Tanzania.
Wanasema pesa ni sabuni ya roho. Mshindi wa Ligi ya Mabingwa anapata takribani Sh 6 bilioni na Sh 1.5 bilioni zinapatikana kwa kuingia makundi. Kiu ya fedha zinazotolewa na CAF inazisukuma klabu kucheza si kwa kutafuta sifa tu, bali pia kutia kifurushi cha maana kibindoni. Na kwa kujua kuna mapato yanatokana na kufanya vizuri, klabu sasa ziko tayari kutumia fedha kununua wachezaji wazuri nchini na hata wageni wanaoweza kufikia 12. Fedha hizi na zile zitolewazo kwenye ligi zinafanya kuwepo kwa mvuto na ushindani hapa nchini katika kuwania kuwakilisha nchi kimataifa.
Yanga bado ina nafasi
Mashabiki wa Yanga wamekatishwa tamaa na matokeo ya 1-1 nyumbani dhidi ya Al Hilal.Kwa kuangalia mchezo wa kwanza ulivyokuwa, bado nawapa yanga nafasi 50/100 kutinga hatua ya makundi. Katika mchezo wa kwanza Yanga ilikuwa bora kwa zaidi ya dakika 55. Bao la kusawazisha liliwashtua wachezaji na benchi la ufundi. Hata hivyo, kwenye mchezo wa marudiano Al Hilal watakuwa na presha kama ya Yanga au zaidi kwani watacheza na tahadhari ya kutoruhusu bao nyumbani. Yanga wanayo rekodi ya kufanya vizuri hasa wanapokumbana na changamoto kubwa ugenini.Yote kwa yote ni lazima kukumbana au kushindana na aliye bora ili kuwa bora.Msimu uliopita Simba ilitolewa katika hatua hii na kuangukia Kombe la Shirikisho. Bila shaka Yanga ingependa kufanya vizuri kwani hata huko kwenye Kombe la Shirikisho kuna changamoto ya michezo miwili migumu kabla ya kuingia makundi. Sare ya zaidi ya bao moja au ushindi wowote utaipeleka Yanga hatua ya makundi ambayo ilicheza mara ya mwisho mwaka 1998.
Simba mguu mmoja makundi
Msimu uliopita Simba ilitolewa katika hatua hii na kuangukia Kombe la Shirikisho ambako ilifanya vizuri na kufika ngazi ya robo fainali. Safari hii inaonekana kuwa vizuri na hata kupandisha kiwango katika michezo ya ugenini. Ushindi wa ugenini wa mabao 1-3 dhidi ya De Agosto ya Angola umewaweka Simba katika nafasi nzuri ya kuingia hatua ya makundi na hivyo kuendeleza mkakati wa kufika nusu fainali au zaidi kwenye ligi hiyo ya mabingwa. Mechi ya marejeano dhidi ya De Agosto haiipi Simba presha ingawa umakini unatakiwa kwani imewahi kufanya vizuri ugenini na kuharibu nyumbani jambo ambalo ni somo. Naipa Simba zaidi ya 75/100 kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Azam shughuli pevu
Ikiwa Libya dhidi ya Klabu ya Al Akhdar ya Bayda Elbeida, Azam ilizidiwa sana kwa mbinu na maarifa.Ilianzia raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho lakini matokeo ya kupoteza 0-3 hayakutegemewa na wengi.Usajili wao wa msimu huu uliashiria kwamba Azam inataka kitu katika mashindano ya Afrika.
Mpira una maajabu yake na Azam inaweza kufanya hayo maajabu. Inatakiwa kufunga zaidi ya mabao 3 bila kuruhusu bao. Nawapa nafasi 25/100 kuweza kutinga hatua makundi ya Kombe la Shirikisho. Iko mifano mingi ya timu zilizowahi kupindua matokeo kibabe.Azam itakuwa imeandika historia ikiweza kufanya hivyo dhidi ya wapinzani wake kutoka Libya ambao uwezo wao ulionekana dhahiri kwenye mchezo wa kwanza.
Kipanga ijinoe kutakata ugenini
Ukiondoa ukweli kwamba Kipanga ya Zanzibar ilikuwa na faida ya kuwa nyumbani dhidi ya Club Africaine ya Tunisia, wengi waliipa nafasi ndogo ya kutoka bila kufungwa.Wengi waliangalia viwango vya klabu za Tanzania na hasa Zanzibar dhidi ya klabu za Tunisia. Labda rekodi nzuri zaidi ya timu ya Zanzibar dhidi ya timu ya Tunisia ni mwaka 1995 pale Malindi FC ilipoifunga Etoile Du Sahel 1-0 lakini ikafungwa kwa idadi kama hiyo ugenini na kisha kutolewa kwa mikwaju 4-3 ya penati katika nusu fainali ya kombe la CAF.
Bado Kipanga ilipambana na kutoka suluhu ya bila kufungana. Hata hivyo, michezo dhidi ya Waarabu nyumbani kwao haijawahi kuwa rahisi. Kipanga inatakiwa kushinda au kutoka sare ya idadi yoyote ya mabao ili kusonga mbele.Nawapa kipanga nafasi 50/100 kusonga mbele.
Kila la kheri kwa timu zetu nne. Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania.