Padri atuhumiwa kumbaka mtoto aliyekwenda kuungama



PAROKO wa Parokia Teule ya Mtakatifu Dionis Aropagita ya Jimbo Katoliki la Moshi, Padri Sosthenes Bahati (41), amesomewa maelezo ya awali ya kesi anayotuhumiwa kubaka mtoto katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi mkoani Kilimanjaro.

Akisomewa maelezo hayo, alikiri kutambuliwa kwenye gwaride maalumu la utambuzi na kukana kutenda kosa hilo.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi, Salome Mshasha, Wakili wa Serikali Mwandamizi Kassim Nasri, aliyeambatana na Wakili Sabitina Mcharo alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo Agosti 12, mwaka huu, mtoto alipokwenda mbele yake kuungama.

"Agosti 12, mwaka huu, mtoto huyo alikuwa kwenye Kanisa Katoliki la Mtakatifu Dionis Aropagita, Kawawa kwa lengo la kushiriki mafundisho ya Kipaimara kama inavyotakiwa na alirudi jioni kwa ajili ya kuungama dhambi zake.

Wakati wa maungamo alimkuta mshtakiwa (padri) amekaa kwenye kiti chake, naye alipiga magoti na kuanza kuungama dhambi zake, kwa kuzitaja moja moja, wakati wa kupokea kitubio, mshtakiwa alianza kumtomasa sehemu mbalimbali za mwili wake hadi sehemu za siri,” alidai.


Wakili Nasri alidai baada ya kumtomasa alimvua nguo na yeye kupandisha kanzu yake na kumfanyia ukatili wa kumwingilia kimwili.

"Mtoto alipofika nyumbani kwenye mazungumzo ya mama na mwana, alimsimulia mama yake kilichotokea ndipo mama huyo alipokwenda kutoa taarifa polisi,” alidai na kuendelea “uchunguzi wa awali ulionyesha mtoto huyo ameingiliwa na lilipofanyika gwaride la utambuzi alimtambua mshtakiwa huyo.”

Upande wa Jamhuri katika kesi hiyo una mashahidi 10, wanne kati yao wataletwa kutoa ushahidi wao mfululizo.


Wakili Nasri alidai kuwa upande wa Jamhuri ulikuwa tayari kuendelea na kesi hiyo ingawa wakili wa utetezi, Edwin Silayo, aliiomba mahakama hiyo kutosikilizwa kwa kesi hiyo ili kumpa nafasi ya kukatana na mteja wake.

Alidai pia wana mpango wa kuegemeza utetezi kwa kuleta ushahidi wa mshtakiwa kutokuwapo eneo la tukio siku ya tajwa.

Hakimu Mshasha aliahirisha kesi hiyo hadi kesho.

Padri Bahati alifikishwa mahakamani Septemba 26, mwaka huu, akikabiliwa na kesi za ubakaji tatu za watoto walio chini ya umri wa miaka 12, mbili zikiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi na moja katika Mahakama ya Wilaya ya Moshi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad