Sababu ya Mgawo wa Maji Dar es Salaam



Pwani. Wakati Serikali ikitangaza kuanza kwa mgawo wa maji jijini Dar es Salaam, sababu ya kutokea shida ya maji kila unapofika mwisho wa mwaka imeelezwa.

Juzi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla alitangaza kuwepo kwa mgawo huo baada ya kutembelea vyanzo vya kuzalisha maji vya Ruvu Chini na Ruvu Juu na kujionea upungufu katika uzalishaji wa maji kulikosababishwa na ukame.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Makalla, aliyewawakilisha pia wakuu wa mikoa ya Pwani na Morogoro alisema hali si nzuri, kwani kina cha maji cha vyanzo hivyo kimepungua, huku uzalishaji ukipungua kutoka lita za ujazo milioni 466 kwa siku hadi kufika lita milioni 300 sawa na asilimia 64 ya uzalishaji wote wa maji.

“Naomba niwaambie wananchi kuwa mgawo haupekuki kutokana na ukame ambao tayari TMA (Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini) ilishatangaza kuwepo kwa hali hii muda mrefu kulikosababishwa na kunyesha mvua chache msimu wa mvua uliopita na kuchelewa kunyesha kwa mvua katika msimu huu wa vuli.


“Pia watu waelewe hali hii haisababishwi na Serikali wala sera za CCM, bali ni mipango ya Mungu, hivyo asitokee mtu huko akaanza kupotosha. Kikubwa tuendelee kumuomba Mungu atuletee mvua za vuli na vyanzo vyetu vya maji viweze kujaa,” alisema Makalla.

Kutokana na hali ya kupungua kwa kina cha maji, Makalla alisema mgawo wa maji katika jiji hilo hauepukiki, licha ya jitajada ambazo Serikali inaendelea kuzichukua, ikiwemo kukamilisha ujenzi wa mradi wa kisima cha maji Kigamboni unaotarajiwa kuanza kutumika mwisho mwezi huu.

Makalla alisema kamati zote za ulinzi na usalama za Mkoa wa Morogoro, Pwani na Dar es Salaam zimewadhibiti watu wote waliokuwa wakichepusha maji na sasa kisingizo cha kuwa ni wao wanaosababisha uhaba wa maji hakipo.


Pia aliwaomba wakazi wa Dar es Salaam na Pwani kutumia vizuri maji yanayopatikana, ili yaweze kuwafaa kwa kipindi hiki.

Katika ziara hiyo, Makalla aliongozana na bodi ya Dawasa pamoja na wakuu wa wilaya wanne ambao ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng`wilabuzu Lubigija, Mkuu wa Wilaya Kigamboni, Fatma Almas, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Heri James na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe.

Kwa upande wake, ofisa mtendaji wa Dawasa, Cyprian Luhemeja alisema watatoa ratiba za mgawo huo siku chache zijazo.

Kwa mujibu wa Dawasa, maji yanayohitajika katika jiji la Dar es Salaam kwa siku ni lita za ujazo milioni 500, hivyo kufanya kuwa na uhaba wa lita 200 kwa sasa.


Alipotafutwa Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi kuzungumzia mikakati ya Serikali kukabiliana na adha hiyo inayoonekana kuanza kuwa sugu katika miezi ya mwisho wa mwaka alijibu kwa kifupi, “kama ulimsikiliza vizuri aliyetangaza hiyo, majibu yako wazi hiyo ni natural calamities (majanga ya asili), hata hivyo nipo kikaoni,” alisema na kukata simu.

Novemba 8 mwaka jana, Dawasa ilitangaza kuanza kwa mgawo wa maji katika Mkoa wa Dar es Salaam uliosababishwa na upungufu wa maji katika Mto Ruvu, ambako uzalishaji ulifikia lita milioni 460 kutoka lita milioni 520 kwa siku sawa, na upungufu asilimia 12.

Novemba 22, 2021, Makalla alitembelea mto huo na kukiri kwamba hali bado si shwari na kilichopo ni kuomba kudra za Mwenyezi Mungu, kwani mkoa wake unategemea maji kutoka Mto Ruvu Chini uliopo Bagamoyo na Mto Ruvu Juu uliopo Kibaha.

“Yale ya kibinadamu tumeshafanya kwa uwezo wetu, ikiwamo kuwasaka wachepushaji maji, kilichobaki ni kudra za Mungu. Tumekuja hapa kuona hali halisi ili mkoa uwe mabalozi wazuri wa kuwaeleza wananchi nini kinachoendelea, kwani ukiona kitu kwa macho ni rahisi kuwaeleza watu kuliko kuelezewa,” alisema Makalla.


Taarifa ya mgawo wa maji iliyotolewa jana imekuja wakati ambao tayari wakazi wa jiji hilo walishaanza kupata machungu ya kukosa huduma hiyo, huku wengine wakitumia mitandao ya kijamii kuhoji kinachoendelea.

Kupitia ukurasa wa Instagram, mfanyabiashara Resty Kweka aliandika, “jamani maji tunapata wapi wiki nzima hayatoki, hivi kweli familia ikikosa maji wiki nzima kuna maisha? Dawasa toeni tamko maisha bila maji ni magumu.”

Naye Emmanuel Michael akaandika, “hili suala la maji limeshakuwa tatizo sugu, ni vema tukaelezwa wazi kuna shida gani, haiwezekani mnakaa siku mbili hakuna maji, huu si mwanzo wa kutokea magonjwa ya mlipuko, maana kuna uwezekano tukapata maji yasiyo salama, lakini kwa sababu ya shida tutatumia,” alisema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad