NYOTA wa zamani wa Yanga, Mrundi Saidi Ntibanzokiza ‘Saido’ ambaye kwa sasa anakipiga Geita Gold ameweka wazi tofauti zilizopo kati ya chama lake hilo la zamani na timu nyingine za Ligi Kuu.
Saido ameeleza Yanga ina utofauti mkubwa na timu nyingine kutokana na namna inavyoendeshwa, uchezaji wake na mazingira ya wachezaji kuwa tofauti na hilo ndilo linaifanya iendelee kuonekana kubwa.
“Unaweza kusema timu zote ni sawa kwa kuwa zinacheza ligi moja, lakini ndani yake kuna utofauti mkubwa karibu wa kila kitu,” alisema Saido aliyeichezea Yanga msimu uliopita na kuongeza;
“Siwezi kuizungumzia sana Yanga kwa kuwa sasa nipo na timu nyingine, kipindi nipo pale mambo mengi yalikuwa ya kipekee na kwa ukubwa na ubora tofauti na timu nyingine zinavyoisha.”
Sambamba na hilo, Saido ameeleza ubora wa kikosi cha Geita kuimarika kila siku na kuwataka mashabiki wa timu hiyo kuwa watulivu kwani mambo mazuri yanakuja.
“Haukua mwanzo mzuri sana kwetu, tulikuwa tukitafuta uimara wa timu na kadri siku zinavyokwenda tunazidi kuzoeana na kujua tuchezeje ili kupata matokeo mazuri, hivyo wapenzi wa timu hii wawe na subra siku si nyingi wataanza kufurahi,” alisema.