YANGA walikuwa kwenye hatua za mwisho za kuachana na Kocha Nasredine Nabi, lakini habari za ndani ambazo Mwanaspoti imezipata jana ni kwamba tajiri wa timu hiyo, Ghalib Said ‘GSM’ amezuia asiondoke.
Yanga tayari ilishafanya mazungumzo na kumtumia mkataba Kocha raia wa Brazil, Robert Oliveira ‘Robertinho’ anayeinoa Vipers ya Uganda lakini tajiri akasema kila kitu kitulie kwanza baada ya presha kuwa kubwa kutoka kwa wanachama na mashabiki.
Habari za ndani zinasema kwamba Yanga walishakubaliana kufanya uamuzi huo kutokana na sintofahamu zilizokuwa zikiendelea kwenye benchi la ufundi na kwa wachezaji. Habari zinasema kwamba juzi Jumatatu Nabi alimsaka kigogo huyo kutaka kujua hatma yake baada ya kuona upepo haueleweki kwa baadhi ya viongozi haswa baada ya tetesi za kufukuzwa kumfikia, lakini jana akamwambia aendelee na kazi mpaka atakapomwambia vinginevyo.
Lakini habari za ndani zinasema miongoni mwa sababu tano zilizoifanya Yanga kufikiria kumng’oa Nabi, miongoni mwake mastaa wamo.
Licha ya kwamba mashabiki wengi wameonekana kuhofia mabadiliko hayo yanayokwenda kimyakimya, Mwanaspoti limeambiwa haya ndiyo yanayomng’oa Nabi;
MASTAA, CHUMBA CHA KUBADILISHIA
Habari zinasema licha ya kwamba Yanga inashinda, lakini katika miezi ya hivi karibuni kumeibuka mgawanyiko miongoni kwa wachezaji wa timu hiyo wengine wakiwa kwa Nabi na baadhi kwa Kaze, jambo ambalo limekuwa likiibua mkanganyiko wa kimamlaka.
Habari zinasema kuna wakati mmoja wao amekuwa akitoa maelekezo nje ya uwanja lakini mwingine anayafuta na kuibua mkanganyiko miongoni mwa wachezaji ingawa wao kwa wao wamekuwa wakikutana chemba na kuyajenga lakini tayari wachezaji wanakuwa wameshapata picha tofauti.
Habari zinasema hali hiyo imesababisha hata kwenye vyumba vya kubadilishia baadhi ya wachezaji nidhamu zao zimeshuka hususan wale wa kigeni kutoka DR Congo ambao wako karibu na viongozi wa juu na wamekuwa na visingizio vingi ambavyo vimekuwa vikiathiri hata utendaji wao mazoezini kwani wamepunguza kujituma.
MZOZO WA KAZE, NABI
Licha ya kwamba ipo ndani sana lakini moja ya sababu ambayo inawafanya viongozi wa Yanga kufikia uamuzi wa kuvunja benchi hilo la ufundi ni kupishana kauli mara kadhaa baina ya Nabi na Kaze ambao wameshakutanishwa na kuyajenga lakini bado inaonekana kuna kitu hakijakaa sawa. Habari zinasema wawili hao mara kadhaa Nabi amekuwa akifanya uamuzi bila kumshirikisha msaidizi jambo ambalo viongozi wanaona halina afya kwa maendeleo ya klabu na huenda Kaze akapelekwa kwenye programu za vijana hivi punde huku Nabi ataonyeshwa mlango wa kutokea.
NABI HASHAURIKI
Mabosi wa Yanga wanadai Nabi amekuwa hashauriki kwa baadhi ya mambo ikiwemo ishu ya timu kukaa kambini kwa muda mrefu huku kocha naye akiwa na mfumo wake wa kuingia kambini siku tatu kabla ya mechi kitu ambacho amekuwa akikifanya hata kabla ya Yanga kuchukua mataji yote msimu uliopita.
Nabi naye amekuwa na malalamiko yake katika hilo akieleza mabosi hao wamekuwa hawataki kumsikiliza huku viongozi wakidai wachezaji kukaa kwenye familia zao muda mrefu ni tatizo kiufundi huku baadhi wakitolea mfano wachezaji walioongezeka uzito na kushuka ubora wao.
Habari zinasema kitendo cha baadhi ya wachezaji kuruhusiwa kwenda majumbani kwao wakati wengine wakiwa kambini imeibua pia minong’ono ya chinichini kwa wachezaji.
TAJIRI NA KUTOLEWA CAF
Habari za ndani zinadai kitendo cha Nabi kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na tajiri Ghalib Said na kuwaruka baadhi ya viongozi kwenye mambo kadhaa imewakera kwani wanataka afuate utaratibu ingawa watu wake wa karibu wanadai anahisi hasikilizwi.
Lakini kushindwa kuwa na mbinu za kuipeleka Yanga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kimewachefua viongozi wengi ambao wanadhani Nabi hakushirikiana vizuri na timu yake ya ufundi kutekeleza jukumu hilo lililowapa Simba cha kuongea mitaani.
YANGA KUPUNGUA MAKALI
Ingawa haijapoteza mechi yoyote kwenye ligi ya ndani mpaka sasa, lakini mabosi wa Yanga wanaona kuna shida katika eneo la mazoezi ya timu yao.
Licha ya kwamba haijionyeshi moja kwa moja, uwajibikaji na ushirikiano duni baina ya Kaze na Nabi umekuwa ukiibuka mpaka katika eneo la mazoezi, wachezaji wamekuwa wakidai kocha wao amekuwa akiongea sana na kumnyima Kaze nafasi ya kufanya lolote akiona kama msaidizi wake anataka kuchukua nafasi yake.
Hatua hiyo imekuwa ikipunguza muda wa kufanyika mazoezi na hata mchango wa Kaze ukionekana duni. Hiki kimechukuliwa kama sababu ya kupunguza ubora wa Yanga uwanjani msimu huu. Lakini habari zinadai hata Kaze na mwenyewe amekuwa hafurahii kazi ya ukalimani.
Mwanaspoti