MAPEMA tu. timu ya taifa ya wanawake U-17, Serengeti Girls leo mchana ina jambo lake, wakati itakaposhuka uwanjani kuvaana Colombia kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la Dunia la Vijana.
Timu hiyo inayoshiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza imepania kuendelea kuwapa raha mashabiki kwa kuhakikisha inaimaliza mapema Colombia na kukata tiketi ya nusu fainali ya michuano hiyo inayofanyikia nchini India.
Mchezo huo unapigwa saa 8:00 mchana kwenye Uwanja wa Pandit Jawaharlal Nehru, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Bakar Shime akisema jeshi lake lipo kamili kwa ajili ya kuendeleza moto katika michuano hiyo.
Serengeti ilitinga hatua ya robo fainali baada ya kupata pointi nne katika hatua ya makundi ikifungwa 4-0 na Japan, ikishinda 2-1 dhidi ya Ufaransa na kutoka sare 1-1 na Canada.
Hii inakuwa ni robo fainali ya rekodi kwa pande zote mbili, kwani licha ya Tanzania kushiriki kwa mara ya kwanza imetengeneza rekodi yake ya kucheza robo fainali na upande wa Colombia wao mara nne wameishia hatua ya makundi na sasa imetengeneza rekodi nyingine ya kutinga hatua ya robo.
Colombia iliishia hatua ya makundi 2008, 2012, 2014 na 2018.
Kocha Shime akizungumzia mchezo huu alisema wataingia kuikabili Colombia wakiwa na nidhamu kubwa katika kujilinda na kushambulia ili kuwa salama.
U-23, NIGERIA VITANI
Wakati Serengeti ikiwa kazini nchini India, timu ya taifa ya vijana U23, yenyewe itakuwa bize jijini Dar es Salaam kuvaana na Nigeria katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya michuano ya kufuzu fainali za Afrika (Afcon) U23 2023.
Mechi ya timu hizo itapigwa kuanza saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na matokeo ya ushindi itaiweka timu hiyo katika nafasi nzuri kwa mchezo wa marudiano wiki ijayo.