Serikali Yaigeukia Yanga Mechi CAF



WAKATI Yanga ikiendelea na maandalizi mazito kuelekea mechi yao ya mkondo wa pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal ya Sudan, serikali kupitia kwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa,...

YANGA SC.
...ameitaka timu kwenda kufanya kile walichokifanya watani wao wa jadi, Simba kwa kupata ushindi ugenini kwenye michuano hiyo.

Mwishoni mwa wiki Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya wenyeji wao, Primeiro de Agosto nchini Angola huku Yanga ikilazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Hilal katika mechi ya michuano hiyo iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo, Simba sasa inahitaji sare ya aina yoyote, ushindi ama kutokubali kufungwa zaidi ya mabao 2-0 ili kutinga hatua ya makundi, wakati Yanga yenyewe ikilazimika kushinda au kutoka sare ya zaidi ya mabao mawili ili kusonga mbele.

Mchengerwa alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana, wakati akikabidhi zawadi kwa Timu ya Taifa ya Soka ya Watu wenye Ulemavu (Tembo Warriors), kutokana na kuiwezesha Tanzania kuingia katika nafasi ya saba ya viwango vya dunia kwa mchezo huo ilipokuwa ikishiriki Kombe la Dunia nchini Uturuki.

Mchengerwa alisema Simba wamefanikiwa kuipeperusha vema bendera ya Tanzania katika michuano ya kimataifa kwa kupata ushindi ugenini na Yanga iliyoanzia nyumbani sasa inatakiwa kwenda kupambana na kushinda mechi hiyo ya ugenini mwishoni mwa wiki hii.

Alimuagiza Rais wa Yanga, Hersi Said, timu yao kwenda kupambana nchini Sudan kwa ajili ya kupata matokeo na kwamba anaamini wachezaji wakijitoa watafanikiwa kupindua meza.

"Klabu zinapofanya vizuri katika michezo hii, sifa inakuwa kwa taifa, tumeona Simba ilivyofanya nchini Angola na sasa tunataka Yanga waende kufanya kile kilichofanywa na 'Wekundu wa Msimbazi," alisema Mchengerwa.

Aidha, waziri huyo aliwataka viongozi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) na wengine kushirikiana na klabu zinazokwenda kushiriki michuano ya kimataifa kwa kuwasaidia mbinu ili kulitangaza taifa.


Alisema msaada huo ni pamoja na kuweka mikakati itakayosaidi kupiga hatua bila kubagua.

"Serikali ina mpango wa kuandaa michuano ya AFCON na ili kufanikisha hilo lazima klabu zetu zifanye vizuri waonekane na muwatie moyo," alisema Mchengerwa.


Hata hivyo, wakati Mchengerwa akiyasema hayo, Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, amesema mafanikio yao yametokana na maandalizi makubwa waliyoyafanya mwanzoni mwa msimu.

"Tulijiandaa mapema kucheza mechi za kimataifa, tulikwenda nchini Misri kuweka kambi ya mwanzo wa msimu, tukacheza mechi mbalimbali ikiwamo dhidi ya Haras El Hodood, hatukwenda huko kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu au Ngao ya Jamii, baadaye tukaenda Sudan kucheza dhidi ya Al Hilal na Asante Kotoko.

"Ili kucheza mechi za kimataifa inafaa ucheze mechi za kirafiki za kimataifa ili ujione wapi ulipo na upandishe kiwango au kukirekebisha, lakini ukijifungia na kucheza mechi unazotaka mwenyewe ili uzifunge, ufurahishe mashabiki wako, matokeo yake yanakuja kuonekana wakati kama huu," alisema Ahmed.

Katika hatua nyingine Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, ameanza kuwapa mpango mpya wachezaji wake lengo likiwa ni kuhakikisha anapata matokeo chanya katika mechi dhidi ya Al Hilal itakayopigwa nchini Sudan Jumapili wiki hii.

Akizungumza na gazeti hili jana, Nabi alisema maandalizi wanayofanya ni kufanyia kazi mapungufu yao katika kila safu ikiwamo ya ulinzi na ushambuliaji, kujilinda na kutafuta ushindi ugenini.

Alisema mechi itakuwa ya ushindani mkubwa na mikakati inapangwa kuelekea mchezo dhidi ya Al Hilal kwa sababu kila mmoja wao anahitaji kupata ushindi ili kufuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo.

"Tumepata sare nyumbani mechi ya kwanza haina maana tumeondolewa, bado tuna nafasi ya kufanya vizuri katika dakika 90 za kipindi cha pili, tunaendelea na mipango yetu ya kuandaa kikosi kutafuta matokeo mazuri nchini Sudan," alisema.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad