MBUNGE wa Viti Maalum (CHADEMA), Grace Tendega, ameieleza Mahakama Kuu kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, alikwenda katika kikao akiwa na majina 10 ya wabunge wa viti maalum.
Katibu Mkuu wa chadema, John Mnyika.
Alidai kuwa katika kikao hicho, Mnyika alipendekeza kuwa katika majina ya wateule hao ni lazima kuwapo na jina la Nusrat Hanje, kwa sababu yuko mahabusu muda mrefu, hivyo anapaswa kutoka.
Tendega alidai hayo jana mbele ya Jaji Cyprian Mkeha wakati akiulizwa maswali na Wakili Ipilinga Panya, katika kesi ya kupinga kuvuliwa uanachama iliyofunguliwa na Halima Mdee na wenzake 18.
Alidai kuwa Novemba 7, 2020 akiwa ni kiongozi wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) alikuwa kwenye kikao na siku hiyo kulikuwa na vikao vingi vya kuchagua wabunge wa viti maalum.
Tendega alidai kuwa wakati wanaendelea na kikao hicho, aliingia Mnyika akiwa na majina 10 ya wateule wa viti maalum, huku akisisitiza katika wateule hao lazima liwapo na jina la Nusrat Hanje.
Hata hivyo, katika video ambayo imechezwa mahakamani hapo, ilionyesha Mnyika na Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Freeman Mbowe, wakidai kuwa Kamati Kuu ya CHADEMA haikuwahi kupitisha majina 19 ya wabunge hao.
Tendega alidai kuwa wito wa kuitwa makao makuu ya chama hicho aliyapata Novemba 27, 2020 ambayo yalitumwa kwake kwa njia ya mtandao wa kijamii wa WhatsApp, kwamba siku hiyo ndiyo kikao kilikuwa kinafanyika asubuhi.
Alidai kuwa njia hiyo ilimpa shaka licha ya kuwa Katiba ya CHADEMA inatambua teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kuwa ni njia ya mawasiliano huku akidai kuwa akiwa kiongozi ndani ya chama hicho hawajawahi kupitisha WhatsApp au Twitter katika mawasiliano yao.
Tendega aliomba ili kuthibitisha hilo, mahakama hiyo isome Katiba ya chama hicho ili aonyeshe wasiwasi wake alioupata katika taarifa ya wito aliyotumiwa kwa WhatsApp, na baada ya kusoma Katiba hiyo ilionesha barua pepe ndiyo inatambulika.
Pia aliondoa utata wa kutia saini kiapo chake kwa madai kuwa ni kweli Julai 18, 2022 alikuwa mkoani Dodoma na alitakiwa kutia saini kiapo hicho huku akidai kuwa alisafiri kutoka Dodoma hadi Dar es Salaam kwa ajili ya kutia saini.
Alidai kuwa uthibitisho wake kwamba alisafiri kwenda Dar es Salaam ni kiapo ambacho ameapa mahakamani na pia yeye ni Mkristo anayeijua dini, kwa hiyo hawezi kuleta shahidi wa kuthibitisha hilo.
Mdee na wenzake 18 walifungua kesi hiyo Julai 21, mwaka huu, dhidi ya CHADEMA, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wakipinga uamuzi wa Baraza Kuu la CHADEMA kuwavua uanachama, Mei 11, 2022.
Katika shauri hilo namba 36 la mwaka 2022, wabunge hao pamoja na mambo mengine, wanaiomba mahakama hiyo ipitie mchakato na uamuzi huo wa CHADEMA kuwafukuza, kisha itoe amri tatu.
Wabunge hao wanaomba mahakama itengue mchakato na uamuzi wa kuwavua uanachama, iwalazimishe CHADEMA kuwapa haki ya kuwasikiliza na amri ya zuio dhidi ya Spika wa Bunge na NEC kutokuchukua hatua yoyote mpaka malalamiko yao yatakapoamuriwa.
Mbunge wa chama hicho, Hawa Mwaifunga (46), aliieleza mahakama kuwa kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho, Kamati Kuu inaruhusiwa kutoa uamuzi bila mhusika kuwapo (kuhojiwa).
Akiendelea kujibu maswali ya Wakili wa CHADEMA, Peter Kibatala, Mwaifunga alidai kuwa hajawahi kufungua kesi ya malalamiko ya kupinga baadhi ya vifungu vya Katiba yao kwa sababu Kibatala hakumsaidia kufanya hivyo.
Pia alidai hakumbuki kama Zitto Kabwe mwaka 2011 alijadiliwa na kuondolewa uanachama na Kamati Kuu ya CHADEMA bila ya yeye kuwapo.
Alidai katika video mbili zilizochezwa mahakamani hapo ya Mnyika na Mbowe, hakuna aliyewaita wao ni wabunge COVID- 19 na kwamba katika kiapo chake yapo maneno hayo.