Simba ilivyopangua mitego ya Agosto





MKUBWA ni mkubwa tu na ndicho kilichojidhihirisha katika safari ya Simba wikiendi iliyopita kwenda Angola kucheza dhidi ya Primiero de Agosto katika mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwanza ilituma mashushushu wake jijini Luanda, Angola wiki tatu nyuma ambao walipata taarifa za kutosha juu ya wapinzani wao Agosto, pia mazingira halisi ya Angola yalivyo.

Ripoti hiyo ya watu hao ambao iliyowaagiza Angola ndio iliyochangia kwa kiasi kikubwa Simba kuamua kuelekea nchini humo kwa ndege ya kukodi ambayo ilitua siku moja kabla ya mechi na kisha kuwarudisha mara baada ya mchezo kumalizika usiku wa jana.

Lakini kama hiyo haitoshi, Simba iliamua kuwapima kipimo cha Uviko-19 wachezaji na maofisa wake wa benchi la ufundi ili kuwaepusha na usumbufu wa kulazimishwa kupima katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Luanda kwa vile vipimo walivyofanya nyumbani, vinadumu kwa muda wa saa 72.


Iwapo vipimo vingefanyika katika Uwanja wa Ndege wa Luanda, Simba iangelazimika kutumia muda mrefu zaidi jambo ambalo lingewafanya wachezaji kuathirika kisaikolojia.

Mara baada ya kufika uwanjani hapo, walikutana na basi kubwa la kubebea abiria ambalo waliandaliwa na wenyeji wao, lakini Simba waliamua kutolitumia na badala yake wakatumia lingine lililoandaliwa na wao wenyewe Simba huku lile la mwanzo wakipakizwa mashabiki walioambatana na Simba hapa.

Hotelini, Simba iliweka ulinzi mkali katika vyumba vya wachezaji na hata chakula cha wachezaji kilipikwa na wao wenyewe kupitia mpishi waliyeambatana naye.


Baada ya mchezo wa jana Jumapili, Simba na Agosto zitarudiana wikiendi hii katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo mshindi wa jumla ataingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na atakayekwama atashuka kwenda kucheza play-off ya Kombe la Shirikisho Afrika michuano ambayo Simba msimu uliopita ilifika robo fainali kabla ya kung’olewa.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad